MWENYEKITI WA KITUO CHA DEMOKRASIA (TCD) JOHN CHEYO AWAELEZA UKAWA KUWA WAKWELI NA KUWAPIGA KIJEMBE, BUNGE LA KATIBA HALIENDESHWI NA AMRI ZA WATU WALIOKO BARABARANI
John Cheyo
MWENYEKITI wa Kituo cha Demokrasia (TCD), John Cheyo amewataka wanasiasa wenzake wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambao wanashinikiza Bunge Maalumu la Katiba (BMK) liahirishwe, wawe wakweli.
Amesema kuwa Bunge hilo, haliendeshwi kwa amri za watu walioko barabarani. Pia, Cheyo amesema Rais hana mamlaka ya kusimamisha Bunge hilo; kwani linaendelea kisheria na litakoma Oktoba 4, mwaka huu.
Amesisitiza kuwa katika majadiliano yaliyokuwa yanafanywa kati ya viongozi wa vyama vya siasa na Rais Jakaya Kikwete, waliafikiana mambo hayo na sio vinginevyo.
“Kama wanabisha, tumwombe Rais aruhusu majadiliano hayo yaoneshwe kwenye Kipindi Maalumu ili kila mtu aonekane mambo aliyokuwa anayasema kwenye kikao hicho…waungwana na sio kwenda kupotosha watu,” alisema Cheyo wakati anatoa mchango wake bungeni mjini hapa jana.
Cheyo aliliambia Bunge hilo, kuwa hakuna makubaliano mengine katika mazungumzo hayo, zaidi ya yale ambayo aliyasoma mbele ya waandishi wa habari mwanzoni mwa wiki hii, likiwemo suala la BMK kuendelea na kazi zake ili kukamilisha kazi zake hadi Oktoba 4 mwaka huu.
Akionesha kuchukizwa na kitendo cha viongozi wenzake wa vyama kumruka Cheyo kuwa walikubaliana Bunge lisitishwe, Cheyo alisema kama Ukawa hawafurahishwi na hatua ya BMK kuendelea shauri yao, kwani sheria ndiyo inalipa haki Bunge hilo.
Aliwahakikishia Watanzania kuwa wajumbe waliobaki ndani, watawapatia Watanzania Katiba nzuri yenye kujali maslahi ya wananchi, kama wakulima, wavuvi na wafugaji.
“Hapa tutaandika Katiba ambayo itapendekezwa kwa wananchi, kama mtu yuko nje na anakerwa sisi kuwepo hapa ndani shauri yake…naamini kuwa humu kuna bongo barabara za watu watakaowakabidhi Watanzania Katiba nzuri inayopendekezwa na Bunge,” alisema mwanasiasa huyo.
Cheyo alisisitiza kuwa Katiba inayotungwa ni ya maridhiano na kwamba sio kundi kung’ang’ania upande wao, badala yake akasema pande zinatakiwa kutafuta vitu ambavyo wanaweza kukubaliana navyo na vitu ambavyo vinaweza hata kuwekwa pembeni kwa sasa, wakubaliane kwamba baadaye vikashughulikiwa kwa mazingira ya wakati huo.
Alisema hilo amejifunza wakati wanazungumza na Rais Kikwete juu ya mchakato wa Katiba na uchaguzi wa mwaka 2015. Alisema Rais amekuwa mfano mzuri wa kusikilizana, licha ya kuwa halazimishwi kufanya hivyo na mtu yeyote, badala yake alijishusha akakaa na viongozi wa TCD na wale wanaojiita Ukawa.
Alisema kikao cha kwanza kilidumu kwa saa 4 na kikao cha pili kilidumu kwa saa zaidi ya nne. Alisema miongoni mwa makubaliano yao ni BMK ipate Katiba inayopendekezwa kwa wananchi na wakakubaliana kuwa kwa hali halisi ya muda uliopo haiwezekani mchakato huo ukamalizika kwa Katiba hiyo kupigiwa kura ya maoni na wananchi.
Cheyo alisema sababu ya kufanya hivyo ni kutoahirisha uchaguzi wa mwakani, ambao wote hawakutaka jambo hilo lijitokeze.
“Rais mwenyewe alikataa kuwa tusimtwishe mzigo wa kuahirisha uchaguzi huo na akasisitiza kuwa utaratibu uliopo, uendelee kuwepo na ndio maana tukakubaliana kuwa Bunge limalize kazi yake,” alisema.
Mwanasiasa huyo alisisitiza kuwa Bunge hilo, haliendeshwi kwa amri za mtu aliyeko barabarani, bali linaendeshwa kwa sheria na sheria iliyopo ni GN 254 ambayo inasema Bunge lisitishe shughuli zake Oktoba 4.
“Itoshe mimi kusema yale niliyotangaza kwenye vyombo vya habari ndio makubaliano yetu, hakuna makubaliano mengine, ukisema sikusaini mazungumzo… jamani sio lazima kusaini kila kipengele, bali makubaliano ni matokeo ya mazungumzo na ndicho nilichofanya,” alisema mwanasiasa huyo
. Aliwataka wabunge wajiamini kuwa Katiba itakayotolewa na waandishi, ndio itakuwa Katiba inayopendekezwa kwa ajili ya kwenda kupigiwa kura, hivyo wasisikilize kelele za watu walio nje ya Bunge hilo.
Cheyo alilazimika kutoa tamko hilo bungeni, kutokana na tamko walilolitoa viongozi wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR Mageuzi kwamba hawakubaliani Bunge hilo liendelee, bali lisitishwe kwani kukubali liendelee ni kuvujisha fedha za walipa kodi.
`Urais wa kupokezana ni hatari’
Katika hatua nyingine, Brigedia Jenerali mstaafu Hassan Ngwilizi ameonya kuwa kuingiza kwenye Katiba urais wa kupokezana, kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, ni hatari kwa nchi, kwani kunaifanya nafasi ya rais ionekane kuwa ni ya kugawana madaraka kati ya pande mbili za Muungano.
Akichangia bungeni jana, Ngwilizi alisema hoja zinazotolewa na baadhi ya wajumbe kuwa Urais wa muungano uwe wa kupokezana kati ya Bara na Zanzibar, hazina tija kwani rais anayechaguliwa lazima awe amevuka ukereketwa wa Bara na Zanzibar, badala yake awe ni Mtanzania.
“Rais tunayemchagua ni wa Tanzania, sio wa upande mmoja wa muungano, hatutarajii rais aingie akiwa ni Mtanganyika na Mzanzibar, fikra za namna hiyo zinazidi kutugawa,” alisema Jenerali Ngwilizi.
Alisema hata upande mmoja ukitoa rais kwa miaka 20 mfululizo, kwake anaona ni sawa ili mradi kiongozi anayechaguliwa, anafaa na ni Mtanzania halisi na sio vinginevyo.
Alisema kwamba nchi ikimpata kiongozi bila kuwepo na mvutano wa upande gani ametoka rais huyo, hapo hakuna wasiwasi kwani kiongozi huyo ataongoza nchi kizalendo na kujiamini kuwa ni Mtanzania halisia.
Mwanasiasa huyo pia aliunga mkono kundi ambalo linataka kuwepo na makamu wawili wa Rais, kwa maelezo kuwa makamu wa kwanza awe ni Rais wa Zanzibar na makamu wa pili awe Waziri Mkuu wa Tanzania.
Kwa upande wa Jeshi, Ngwilizi alisema Jeshi pekee la Wananchi lina sehemu tatu za Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ), askari wastaafu ambao wanawajibika kupigana vita inapoingia na mgambo, ambao ni raia wa kujitolea.
Alisema kama kuna vyombo vingine ambavyo itaonekana ni muhimu kushiriki kwenye ulinzi wa nchi, Rais anayaandikia makundi mengine ambayo yamelelewa kwa nidhamu za kijeshi, kama polisi, magereza na KMKM.
“Makundi hayo hayashiriki vita hadi yaandikiwe barua na Amiri Jeshi Mkuu,” alisema Ngwilizi. Alisema Katiba lazima itaje chombo cha ulinzi ambacho ni jeshi na alionya kuwa bila kufanya hivyo, Katiba itapoteza dhana ya Jeshi.
Alisema nchi nyingine zinaishangaa Tanzania kuwa ina majeshi mangapi, kutokana na kila kundi lenye nidhamu ya kijeshi kuitwa Jeshi wakati nchi inakuwa na jeshi moja tu.
Kingunge na Katiba ya kiuchumi Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru amewataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, kuhakikisha kuwa Katiba wanayoiandika, inaisaidia nchi kujikomboa kiuchumi, badala ya kuandika Katiba yenye haki lukuki zinazowanufaisha kundi dogo la watu ambao ni wanasiasa na wafanyabiashara.
Kingunge ambaye ni Mjumbe wa Bunge hilo, alisema jana kuwa haki zinazopigiwa kuwemo kwenye Katiba, nchi zote za Afrika zinazo lakini wanaofaidi haki hizo ni wenye nacho, huku wananchi masikini wakiendelea kuogelea kwenye dimbwi la umasikini.
Alitoa mfano kuwa haki ya kuishi, masikini ambaye hana uhakika wa chakula hiyo haki anafaidikaje nayo.
Alionya kuwa bila kujenga Katiba ambayo inatambua harakati za kuleta mageuzi ya kiuchumi kupitia elimu, kilimo na viwanda, Katiba hiyo haitakuwa na lolote kwa mwananchi wa kawaida.
Alitoa mfano kuwa licha ya Tanzania kuwa na wahandisi lukuki, lakini wanatumika kukarabati vifaa vilivyotengenezwa na wahandisi wa nchi nyingine. Alisema suala hilo lisipoangaliwa, Watanzania wataendelea kuvaa na kutumia bidhaa zilizotengenezwa nje ya nchi.
“Nashangaa Watanzania tumeridhika kwa kuwa watu tunaokula makombo,” alisema Kingunge na aliwataka wajumbe hao wadhamirie kuandika Katiba mpya, ambayo itaondoa na unyonge wa Watanzania kama zilivyofanya nchi za Asia.
Alisema Katiba mpya, lazima itambue kuwepo kwa matumizi ya sayansi na teknolojia, mambo ambayo alisema ndio pekee ambayo yanaweza kuleta ukombozi wa wanyonge wa Watanzania.
Alisema kama uamuzi huo utakubaliwa, utakuwa ndio njia pekee ya kuendesha kilimo cha kisasa na ujenzi wa viwanda kwa kutumia maarifa ya watu wetu.
Katika mapendekezo yake aliyoyatoa kwa Bunge hilo, mkongwe huyo alitaka lengo kuu la Katiba, iwe kujenga uchumi wa kisasa wa taifa linalojitegemea kwa kulifanya taifa lijikite kwenye mchakato wa kutumia maarifa ya kisasa, yaani sayansi na teknolojia katika nyanja zote za shughuli zake za kiuchumi na kijamii.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment