MAJAMBAZI WATEKA KITUO KIKUU CHA POLISI WILAYA KISHA KUUA ASKARI WAWILI NA KUIBA SILAHA NA KUTOWEKA NAZO.
Kamishna wa Polisi Operesheni na Mafunzo, Paulo Chagonja akitoa taarifa za awali za tukio la kuvamiwa kituo cha Polisi Ushirombo mkoani Geita kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana. (Picha na Mroki Mroki).
WATU wanaodaiwa kuwa ni majambazi wamevamia Kituo Kikuu cha Polisi cha Wilaya ya Bukombe kilichopo Ushirombo, mkoani Geita na kuua askari wawili na kuiba silaha za moto.
Taarifa za awali za tukio hilo zimethibitishwa na Kamishna wa Polisi, Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema uvamizi huo unatajwa kufanywa majira ya saa 9 usiku katika kituo hicho mkoani Geita, ambapo inadaiwa wahalifu hao ambao idadi yao inakadiriwa kuwa zaidi ya kumi, walivamia kituo wakiwa na silaha za kivita.
Alisema mazingira ya tukio hilo inaelezwa kuwa majambazi hao walipofika kituoni hapo, walitupa bomu la mkono katika chumba cha mashitaka na kusababisha vifo vya askari wawili wenye namba G.2615 Dunstan Kimati na WP 7106 Uria Mwandiga huku wawili wengine wakijeruhiwa.
“Walifika katika kituo hicho wakiwa na silaha nzito za kivita, wamesababisha vifo vya askari wawili, lakini wawili wengine wanaendelea na matibabu hospitalini,” alisema Chagonja.
Alisema baada ya kuwaua na kuwajeruhi askari hao waliharibu taa na kusababisha giza kutawala kituoni hapo, ambapo walivunja chumba cha kuhifadhia silaha na kutoweka na baadhi ya silaha.
“Majambazi hao walivunja na kuchukua baadhi ya silaha ambazo zilikuwepo kituoni hapo, ambazo mpaka sasa idadi yake haijajulikana,” alisema Chagonja.
Chagonja alisema idadi ya silaha hizo haijajulikana kutokana na operesheni mbalimbali zilizokuwa zikiendelea wilayani humo, hivyo silaha zilikuwa zikiingia na kutoka.
Chagonja alisema, kutokana na tukio hilo Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Ernest Mangu yuko katika eneo la tukio akiwa amefuatana na Mkurugenzi wa Upelekezi na Makosa ya Jinai (DCI) Isaya Mngulu na timu ya wataalamu wa upelelezi na operesheni ili kuhakikisha wahusika wa tukio hilo wanakamatwa.
Hata hivyo, aliwataka wananchi kuwa watulivu akisema Jeshi la Polisi litahakikisha wahusika wa tukio hilo wanakamatwa na sheria kuchukua mkondo wake, lakini pia aliwataka wananchi wenye taarifa muhimu zitakazosaidia kuwakamata wahalifu hao wazitoe ili zifanyiwe kazi.
Kwa mwaka huu tukio kama hilo la kuvamiwa kwa Kituo cha Polisi na kuuawa kwa askari na majambazi kuchukua silaha ni la pili ambapo la kwanza lilitokea Juni, mwaka huu katika Kituo kidogo cha Polisi cha Mkamba, wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani ambako majambazi walimuua askari mmoja na kuwajeruhi wengine watatu na kupora silaha tano zenye risasi ambazo ni SMG mbili na Shot gun tatu.
Hata hivyo, wahalifu waliohusika na tukio hilo walikamatwa na kesi yao bado inaendelea. Ingawa taarifa ya Chagonja haikueleza idadi ya silaha zilizoibwa, taarifa za ndani ambazo gazeti hili inazo zinasema majambazi hao wameiba bunduki kumi, risasi na mabomu ya mkono, kisha kutokomea.
Imeelezwa kuwa baada ya kufika kituoni hapo, majambazi hao walizingira kituo hicho hadi eneo la mapokezi na kuanza kuwamiminia risasi za moto askari waliokuwa zamu.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Dk Honoratha Rutatinisibwa amekiri kupokea miili ya askari wawili wa kike na kiume. Waliojeruhiwa wamefahamika kuwa ni askari mwenye namba E.5831 David Ngupama Mwalugelwa aliyejeruhiwa kichwani na usoni na kwamba ameumizwa vibaya sehemu za mdomo wake huku meno mawili yaking’oka.
Mwingine ni Mohammed Hassan Kilomo aliyejeruhiwa kifuani na mguu wa kulia uliovunjika mfupa kwa kupigwa risasi. Dk Rutatinisibwa alipoulizwa juu ya hali za majeruhi hao, alisema ni mbaya na kwamba walilazimika kuwahamishia Hospitali ya Rufaa ya Bugando, jijini Mwanza kwa matibabu zaidi.
Hilo ni tukio la pili kwa askari wa kituo hicho kuuawa na majambazi ambapo Juni 28, 2009 kundi la majambazi saba wenye silaha za moto aina ya SMG, yaliteka magari manne ya mizigo katika pori linalounganisha maeneo ya Lunzewe, Matabi na Buselesele lililopo Bukombe na kumuua askari Pascal wa Kituo hicho cha Polisi Bukombe.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment