MBINU MBADALA SASA ZITUMIKE KUKABILIANA NA AJALI ZA BARABARANI.
KATIKA siku za hivi karibuni kumetokea mfululizo wa ajali za barabarani, zikihusisha mabasi ya abiria kugongana yenyewe kwa yenyewe, kupinduka au kugongana na malori ya mizigo na kusababisha vifo vya makumi ya watu.
Mathalani, hivi karibuni kulitokea ajali mbaya katika eneo la Sabasaba mjini Musoma, ikiyahusisha mabasi ya J4 na Mwanza Express, moja likielekea Mwanza kutokea Musoma na lingine likielekea Musoma kutokea Mwanza, ambapo watu takribani 39 walipoteza maisha.
Juzi pia kuliripotiwa ajali nyigine za basi la Air Bus likitoka Dar es Salaam kwenda Tabora kupinduka nje kidogo ya Mji wa Gairo, Morogoro na kusababisha vifo vya watu wanne. Hizo ni baadhi tu ya ajali zilizotokea na kuripotiwa ambazo zimeleta maafa makubwa kwa Watanzania wasio na hatia kwa kusababisha vifo na majeraha huku baadhi ya waathirika wakipata ulemavu wa kudumu.
Matukio haya ni ya kutisha. Ni matukio ambayo hayawezi kuendelea kuvumilika kutokana na ukweli kwamba mengi ya matukio hayo yanatokana na uzembe wa madereva, ambao kwa makusudi huendesha mabasi kwa mwendo kasi na baadaye kuwashinda na kupinduka au kugongana.
Matukio ya ajali za barabarani, hayajaanza jana wala juzi, ni matukio ya muda mrefu sasa. Ni matukio ambayo mamlaka husika zimekuwa zikijaribu kukabiliana nayo kwa kutumia njia na mbinu mbalimbali, lakini bila mafanikio au kupata mafanikio kidogo.
Kwa mfano katika kukabiliana na matukio hayo ya ajali za barabarani hasa kwa mabasi ya abiria, Serikali iliamua kupiga marufuku mabasi kusafiri usiku. Lakini pia kwa lengo na azma hiyo hiyo, Serikali pia iliwahi kuamuru mabasi kufungwa vidhibiti mwendo.
Jitihada zote hizi hazikufua dafu, ajali ziliendelea. Hata hivyo, bado hatua zinaendelea kuchukuliwa ili kukabiliana na ukubwa wa tatizo.
Mfano hivi karibuni kumekuwepo na ongezeko la askari wa Usalama Barabarani wenye tochi zinazopima mwendokasi wa magari barabarani na wahusika wamekuwa wanachukuliwa hatua kadhaa.
Wakati mikakati hiyo ikiendelea, tunachukua nafasi hii kuwaasa wadau wa sekta ya usafirishaji, kuunganisha nguvu pamoja ili kuangalia mbinu mbadala zinazoweza kusaidia kumaliza janga hilo na kunusuru maisha ya wananchi wasio na hatia.
Tuonavyo sisi, njia na mbinu ambayo itasaidia kumaliza tatizo hilo ni kutoa elimu ya kubadili fikra na mtazamo wa madereva na hasa wa mabasi ya abiria na abiria wao ili sasa wajue kitu muhimu kufungwa gavana si magari bali ufahamu wao.
Kama gavana zitafungwa kwa madereva na abiria wao, kazi ya kudhibitiana sasa itaanza kufanywa na wao wenyewe wawapo safarini, bila kumsubiri askari wa Usalama Barabarani afanye kazi hiyo. Kwa kifupi ni kwamba ni lazima madereva na abiria wao sasa wajitambue.
Tunafahamu fika kuwa kama madereva watakuwa na ufahamu mkubwa wa kuelewa madhara ya mwendo kasi na uzembe wawapo barabarani, lakini pia abiria wao wakafahamu hatua za kumdhibiti dereva mzembe na anayekwenda mwendo kasi bila ya kumsubiri askari, ajali hizo zitapungua sana au kuisha kabisa.
Ni lazima sasa tukatae ule mtindo wa abiria wa kutoa ushuhuda wa mwendo kasi aliokuwa nao dereva, wakiwa hoi hospitali baada ya ajali kutokea, ili abiria hao sasa waanze kuwaripoti madereva wao wazembe na waenda kasi kabla ya ajali.
Tunaamini kuwa kama tutafanya hivyo, bila shaka ajali za barabarani zitapungua kwa kiasi kikubwa kuliko ilivyo sasa na tutaokoa kwa kiasi kikubwa nguvu kazi ya taifa.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment