Na Renatus Mahima, MTWARA
SIMBA SC imepata sare ya kwanza chini ya kocha Mzambia, Patrick Phiri baada ya kutoka 0-0 na Ndanda Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
Katika mchezo huo, refa David Paul aliyesaidiwa na Mohammed Kayanda na Sawa Omar, wote wa hapa, timu zote zilishambuliana kwa zamu vipindi vyote.
Jacob Masawe aliifungia bao Ndanda dakika ya 51 ambalo hata hivyo, refa David Paul alilikataa kwa kuwa mfungaji alikuwa ameotea kabla ya kufunga, uamuzi ambao haukuwaridhisha wenyeji.
Emmanuel Okwi jana alicheza mechi yake na Simba SC bila kufunga bao.
Katika mchezo huo uliohudhuriwa na Rais wa Simba SC, aliyeongozana na Mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, mshambuliaji Emmanuel Okwi alitokea benchi dakika ya 60 kuchukua nafasi ya Abdallah Seseme, lakini hakuonyesha cheche zake.
Huo unakuwa mchezo wa sita kwa Phiri tangu arejee Simba SC mwezi uliopita, akirithi mikoba ya Mcroatia, Zdravko Logarusic baada ya awali kushinda 2-1 na Kilimani City, 2-0 na Mafunzo, 5-0 na KMKM, 3-0 na Gor Mahia na kufungwa 1-0 na URA.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Hussein Sharrif ‘Cassilas’, Nassor Masoud ‘Chollo’, Abdi Banda, Abdul Azizi, Joram Mgevege, Said Ndemla, Ibrahim Twaha, Amisi Tambwe, Abdallah Seseme, Ibrahm Ajibu, Ramadhani Singano ‘Messi’.
Ndanda; Salehe Malande, Shukuru Chachala, Paul Ngalema, Ernest Joseph, Cassian Ponela, Amir Msumi, Jacob Masawe, Hamisi Salehe, Omar Nyenge, Gideon Benson, Nassor Kapama.
0 comments:
Post a Comment