UKAWA WAZIDI KULITESA BUNGE MAALUMU LA KATIBA LICHA YA KUSUSIA VIKAO DODOMA.
Fahmy Dovutwa
Mjadala unaoendelea katika Bunge la Katiba mjini hapa, unadhirisha wazi kuwa nguvu ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), bado unalisumbua bunge hilo kufuatia muda mwingi kutumiwa na kiti kuelekeza mashambulizi dhidi yao.
Kiti jana kilitumia nafasi yake kuwashambulia Ukawa huku kikitoa muda mwingi kwa mjumbe wa Kituo cha Demokrasia (TCD), Fahmy Dovutwa, kuwashambulia Ukawa ndani ya bunge hilo. Pia nafasi kama hiyo ya mashambulizi ilitolewa kwa Hamad Rashid kumshambulia Maalim Seif Hamad hivi majuzi.
Mwenyekiti wa Bunge hilo, akionyesha kuendelea kukerwa na Ukawa kukaa nje ya bunge, alisema wameendelea kubadilika badilika huku wakitaka bunge hilo liahirishwe akidai ni kinyume na walivyokubaliana na Rais Jakaya Kikwete katika mkutano na wajumbe wa Kituo cha demokrasia Tanzania(TCD).
Akiongea kwa mifano, Mwenyekiti huo wa bunge alisema ndani ya siku 18 tangu kuanza kwa Bunge hilo mwaka huu, wajumbe wa kundi hilo walikuwa wakionyesha vituko.
“Tulipoanza Bunge la Katiba, kulikuwa na mjadala mkubwa kura za wazi au za siri, wao walitaka kura za siri, tulipokubali kura zote zitumike, za wazi na za siri, wao wakapinga za wazi,” alisema kiongozi huyo.
"Sijui kama wenzangu mnaona kile ninachokiona, baadhi ya viongozi hawa wa Ukawa wana kipaji cha uigizaji, waigizaji wazuri sana” alisema.
Alisema baada ya muda wajumbe hao walitoa hoja ya kutaka hati ya Muungano, baadae wakatoa hoja binafsi kwamba Bunge hilo lisiendelee hadi hati ya Muungano ipelekwe.
“Ilipopelekwa nakala ya hati hiyo kwa wajumbe, walikataa na kupelekea serikali kuonyesha hati halisi. Baada ya kuonyeshwa hati halisi ambayo inahifadhiwa kwa uangalifu mkubwa, wenzetu wakasusia Bunge hadi leo,” alisema.
WATAHADHARISHWA
Aliwataka viongozi wa umoja huo kusubiri uchaguzi mkuu wa mwakani waone watakavyoanguka kwenye uchaguzi huo na kurudi kwenye kazi yao ya usanii.
Aidha, alisema katika tukio la hivi karibuni Rais Kikwete alipokutana na viongozi hao na kufikia makubaliano na baada ya siku moja kukana maafikiano hayo, ni mwenendo wa uigizaji wanaofanya.
“Mheshimiwa Rais alikutana nao mara mbili kwa muda wa saa saba, walifikia maafikiano, walipotoka siku moja baadaye walikana yote, hivyo wananchi waendelee kuwapima…mimi nawashauri tu watakaposhindwa vibaya uchaguzi mkuu ujao, warudi na kujikita zaidi kwenye fani yao ya uigizaji” alisema kiongozi huyo.
DOVUTWA ATISHIWA MAISHA
Mjumbe wa Kituo cha Demokrasia (TCD), Fahmy Dovutwa, aliwavaa viongozi wa Ukawa kwa kuwaita wapotoshaji wa makubaliano kati yao na Rais.
Kauli ya Dovutwa imekuja siku moja baada ya Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo, kuwashutumu viongozi hao kuhusu ukweli wa makubaliano hayo.
Akizungumza wakati wa mjadala wa sura mbalimbali za Rasimu ya Katiba Mpya, bungeni Dodoma jana, Dovutwa, alisema upotoshaji huo unafanywa kwa makusudi kwa ajili ya kuleta uchonganishi na kuhatarisha amani ya nchi.
Alisema katika kikao cha Rais na TCD ambacho yeye alihudhuria, walikubaliana kuwa mchakato wa kutengeneza Katiba mpya uendelee hadi Bunge Maalum litakapotoa Katiba inayopendekezwa, tofauti na kauli ya viongozi wa Ukawa kuwa hakukuwa na makubaliano hayo.
Alisema kikao hicho kilifanyika Septemba 8, mwaka huu, Ikulu ndogo ya Kilimani, Dodoma na viongozi wa vyama vinavyounda Ukawa ni wenyeviti na makatibu wakuu kutoka vyama vya CCM, CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi, UPDP na UDP.
“Nashangaa hawa Ukawa walikuwa na nafasi ya kukataa na kumwambia Rais awape muda warudi ili wajadiliane, lakini hawakufanya hivyo, walikubali na Rais kumuomba Mwenyekiti wetu (John Cheyo, ) pamoja na sisi viongozi wenzake tukatangaze kwa wananchi”:
“Kitendo cha kukubali na kisha kujitoa ni hatari na uchonganishi kwa wananchi,” alisema.
Alisema kutokana na jina lake (Dovutwa) kuhusishwa na usaliti, maisha yake yapo hatarini baada ya kupokea simu tatu zikimtishia maisha.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, jina langu ni sehemu ya walengwa, Katibu wa CUF, Maalim Seif Hamad ananishutumu eti mimi ni kibaraka wa CCM jambo ambalo nashangaa, Dovutwa miye na chama changu nawezaje kuhujumu CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi,” aliongeza.
Alisema ndani ya kikao hicho kulizuka mvutano kati ya Rais Kikwete na Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu, baada ya kumtaka Rais kusitisha Bunge.
“Kilichotokea ndani ya kikao, Lissu alimuomba Rais alivunje Bunge, lakini Rais alimwambia bwana Lissu wewe ndiye ulisimamia rais asiwepo kwenye Bunge....kwa sasa hakuna mwenye mamlaka ya kufanya hivyo, Lissu alishindwa kujibu,” alisema.
Dovutwa alisema ushauri wa Lissu wa kutaka kuvunjwa chombo hicho hauwezekani kwani kipo kwa mujibu wa sheria, kwani hatua pekee iliyobaki ambayo Rais anaweza ni kuvunja Bunge la Muungano na kutangaza hali ya hatari, jambo ambalo ni hatari kwa nchi.
Akizungumzia tuhuma kwamba wamekataa kusaini nyaraka za makubaliano, Dovutwa alisema wamefanya hivyo kutokana na kupewa nyaraka hizo na wenzao mlango wa kuingilia Ikulu ili wasipate muda wa kuisoma na kuelewa vizuri.
LUSINDE
Naye, mjumbe, Livingstone Lusinde maarufu Kibajaji, alipingana na mapendekezo ya baadhi ya wajumbe wanaotaka sifa ya elimu ya mtu anayetaka kugombea ubunge kuwa kidato cha nne, na badala yake ibaki kujua kusoma na kuandika, akisema itawanyima watu wengi haki ya kikatiba ya kuchagua viongozi na kuchaguliwa.
Lusinde ambaye pia ni Mbunge wa Mtera alisema badala ya suala la elimu kuwa kigezo kikuu cha mgombea wa ubunge, kiwekwe kipengele cha uadilifu.
“Nashangaa sana kwani darasa la saba, na kidato cha nne aliyepata ‘divisheni 0’ wanatofauti gani kama sio walitofautiana kwenye majibu tu? Kinachotakiwa ni uadilifu ndio jambo la msingi, kwani mtu hata akiwa msomi kama sio muadilifu ni kazi bure,” alisema.
“Suala la nani awe kiongozi tuwaachie wananchi wachague wao ndiyo wanajua nani anawafaa awe amekwenda shule ama la, na si tuwanyime haki zao ambazo ni za msingi,” alisisitiza Lusinde.
Alisema elimu kisiwe kigezo kikuu cha kuwanyima haki ya kugombea wale ambao hawajasoma na kutoa nafasi hizo kwa wasomi kuja na mabegi ya vyeti ili waweze kuonyesha, wakati kuna watu ambao hawajasoma lakini wana uwezo mkubwa kuliko maprofesa.
Mjumbe huyo alitaka matajiri ambao wanamiliki mali nyingi na siyo watawala wafuatiliwe na kueleza mali hizo wamezipataje badala ya kuwabana madiwani na viongozi wengine pekee.
Imeandikwa na Moshi Lusonzo, Jacqueline Massano na Abdallah Bawazir.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment