HUKUMU YA KURA YA MAONI YA KATIBA MPYA SASA KUFANYIKA MACHI 30, 2015.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema
Dar es Salaam. Kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa itafanyika Machi 30 mwakani, gazeti hili limethibitisha.
Hayo yalisemwa jana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema ambaye hata hivyo, alimwambia mwandishi wetu kwamba kabla ya kura hiyo, “lazima daftari la kudumu la wapigakura liboreshwe kwanza” ili kuwapa fursa wapigakura wapya ambao hawamo kwenye daftari hilo.
“Kuboreshwa kwa daftari la wapigakura ni lazima kwa sababu kuna watu wengi wamefikisha umri wa kupiga kura tangu tulipofanya uchaguzi mkuu na hawamo kwenye daftari hilo, kwa hiyo hatuwezi kuwanyima fursa ya kupiga kura kwa sababu ni haki yao kikatiba,” alisema Jaji Werema na kuongeza:
“Lakini lazima tujue pia kwamba kuboreshwa kwa daftari hilo kunahitaji fedha, kwa hiyo kuboreshwa kwake kutategemea kama Serikali itatoa fedha kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili kazi hiyo iweze kufanyika, tusipoboresha daftari tutasababisha kelele na malalamiko mengi”.
Msimamo wa Jaji Werema ni sawa na ule wa Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva ambaye amesisitiza mara kadhaa kwamba tume yake haitoandaa uchaguzi wowote pasipo daftari la kudumu la wapigakura kuandikwa upya.
Jaji Werema alisema ikiwa Serikali itatoa fedha, uboreshaji wa daftari unaweza kukamilika ifikapo Februari 2015 na kwamba inatarajiwa kwamba Machi 30, mwakani kura ya maoni itapigwa kama kila kitu kitakwenda kama kilivyopangwa.
Alisema upigaji kura utatanguliwa na kampeni ambazo zitafanyika kwa siku 30 kuanzia mwanzoni mwa Machi ili kushawishi Katiba inayopendekezwa iungwe mkono au kinyume chake kwa makundi yanayoipinga.
Hadi sasa gharama za kusimamia kura ya maoni kwa ajili ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa zimeendelea kuwa kitendawili.
Jana, Jaji Lubuva alisema asingeweza kuzizungumzia kwa kuwa yuko Dodoma kikazi na kuelekeza taarifa hizo zinaweza kupatikana kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Julius Malaba.
Hata hivyo, alipotafutwa Malaba alisema anaweza kuzungumzia suala hilo katika mkutano na waandishi wa habari anaotarajia kuuitisha wiki hii.
“Wiki hii nitaitisha mkutano na waandishi wa habari kuhusu daftari la wapigakura. Nadhani itakuwa vyema suala hilo likiibuliwa kupitia mkutano huo ndipo majibu yanapoweza kupatikana,” alisema.
Marekebisho ya sheria
Jaji Werema alisema ili kuwezesha utekelezaji wa kura ya maoni, Sheria ya Kura ya Maoni ya 2013 itapelekwa katika kikao kijacho cha Bunge kufanyiwa marekebisho.
“Katika kuwezesha hayo, tutaipeleka sheria katika kikao kijacho cha Bunge ili kufanyia kazi baadhi ya masuala ya kiufundi kwa lengo la kuwezesha kura hiyo kufanyika,” alisema.
Bunge la Muungano linatarajiwa kuanza mkutano wake wa Novemba 5. Hata hivyo, Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alisema jana kwamba ofisi yake ilikuwa haijapokea taarifa kutoka serikalini kuhusu marekebisho ya sheria hiyo.
“Bado sijapokea taarifa yoyote kuhusu kusudio hilo ila kama marekebisho hayo yanatakiwa kufanywa basi wakiyaleta tutayapokea na kama ni hivyo lazima itakuwa chini ya hati ya dharura,” alisema Joel.
Sheria ya Kura ya Maoni ya 2013 katika sehemu ya pili inamtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar, ndani ya siku 14 baada ya kupokea Katiba Inayopendekezwa, kwa amri itakayochapishwa kwenye Gazeti la Serikali, kuielekeza NEC kuendesha kura ya Maoni
Amri ya kuitisha kura ya maoni imeainishwa katika fomu namba moja ya jedwali la kwanza la sheria husika ikimwelekeza Rais kuainisha Katiba Inayopendekezwa itakayoamuliwa, muda utakaotumika kwa ajili ya kampeni ya kura ya maoni na kipindi ambacho kura hiyo itafanyika.
Kwa kuzingatia maelekezo hayo ya kisheria, Rais Kikwete anapaswa kutoa maelekezo kwa NEC kuhusu kura ya maoni si zaidi ya kesho Oktoba 22, mwaka huu ambayo ni siku ya 14 tangu alipokabidhiwa Katiba Inayopendekezwa Oktoba 8 mjini Dodoma.
Makubaliano na TCD
Uamuzi kuhusu kufanyika kura ya maoni mwakani, umekuja kukiwa na makubaliano baina ya Rais Kikwete na vyama vya upinzani kupitia Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) ambayo yalifikiwa Septemba 9, mwaka huu.
Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo alipozungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma alisema walikuwa wamekubaliana kwamba kura ya maoni ifanyike mwaka 2016 ili kutoa fursa ya kufanyika kwa marekebisho kadhaa katika Katiba ya sasa kwa ajili ya kuwezesha uchaguzi mkuu wa mwakani.
Hata hivyo, jana Werema alisema mchakato wa Katiba Mpya kwa mujibu wa makubaliano hayo, ungesimama tu iwapo theluthi mbili isingepatikana ndani ya Bunge Maalumu.
“Sasa theluthi mbili imepatikana pande zote za Muungano kwa hiyo kwa mujibu wa sheria lazima mchakato uendelee,” alisema Werema.Hata hivyo, alisema hata Katiba Inayopendekezwa ikipitishwa haitaweza kutumika kwa ajili ya uchaguzi ujao. “Kwa hiyo baada ya kumaliza kura ya maoni tunaweza kuangalia hayo marekebisho ambayo tunaweza kufanya kwenye Katiba yetu ya sasa na inaweza kuwa Mei hivi,” alisema.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment