MASHOGA, WATOAJI MIMBA NA WANANDOA WALIOTALIKIANA WAGONGA MWAMBA MBELE YA MAASKOFU WAKATORIKI, MSIMAMO MKALI WA KANISA WAENDELEA KUSIMAMA IMARA.
MAASKOFU wa Kanisa la Katoliki juzi waligoma kupitisha mabadiliko makubwa ya kihistoria kuhusu msimamo wao mkali dhidi ya masuala ya ushoga, utoaji mimba na wanandoa waliotalikiana.
Uamuzi huo,ulifichua uwapo wa pengo kubwa ndani ya kanisa hilo mwishoni wa mkutano huo wa wiki mbili.
Maaskofu wa kanisa hilo walikuwa wamekutana kujadili jinsi mafunzo ya kanisa hilo yanavyoweza kufanyiwa mageuzi ili kuambatana na maisha ya kisasa.
Hiyo ni pamoja na kukaribisha ‘zawadi na sifa’ za mashoga Wakatoliki na mwito kwa mapadri kuepuka lugha au tabia yoyote inayoweza kuwanyanyapaa Wakatoliki waliotalikiana.
Wakati lugha kuhusu mashoga ikiwa imelegezwa wakati wa siku za mwisho za majadiliano hayo, waraka wa mwisho uliopendekezwa ulishindwa kupata theluthi mbili ya kura zilizohitajika.
Hata hivyo,maaskofu walisifu upendo wa kweli katika ndoa ya kawaida, wakiita moja ya miujiza mizuri zaidi na inayokubalika.
Kwa kushindwa kukubaliana kwa kauli moja, kunamaanisha kushindwa kwa kauli za kipatanishi za Papa Francis tangu achaguliwe upapa zaidi ya mwaka mmoja uliopita.
Mwaka jana, Papa Francis aliwafurahisha wanaharakati za ushoga wakati alipoonekana kulegeza msimamo wake.
Alipoulizwa swali iwapo mashoga wanapaswa kuwa Wakristo wazuri, alijibu kwa kuuliza, ‘Mimi ni nani hata nihukumu?
Hata hivyo, baada ya viongozi wa Katoliki kupiga kura hiyo, Papa Francis aliwaonya maaskofu dhidi ya ‘ukali lugha’ wakati wa kujadili masuala tete yanayolikabili kanisa hilo.
Msemaji wa Vatican, Federico Lombardi alipoulizwa kuhusu kilichofikiwa katika mkutano huo, alisema waraka uliopo ni mwongozo kwa maaskofu katika utumishi wao na unaweza kujadiliwa tena mwaka ujao.
“Si muhimu kwenda mbali zaidi kuuchambua. Kifupi ni kwamba maaskofu wa sinodi hawakufikia uamuzi wa mwisho kuhusu waraka huo.”
Hatua ya maaskofu kukataa kufanya mageuzi imepokewa kwa ghadhabu na makundi ya kikatoliki yanayopigania haki za wapenzi wa jinsia moja.
Hata hivyo, kundi la kutetea haki za wapenzi wa jinsia moja nchini Marekani la New Ways Ministry, limesema hatua ya maskofu hao kuamua kujadili suala hilo ni matumaini ya siku za usoni.
0 comments:
Post a Comment