BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

HALIMA MDEE JAMANI NI SHIDA KWELI KWELI.

http://freemedia.co.tz/daima/wp-content/uploads/2014/10/halima2.jpg
MWENYEKITI wa Taifa wa Baraza la Wanawake CHADEMA Taifa, (Bawacha), Halima Mdee, amesababisha kusimama kwa muda shughuli mbalimbali Mwanza wakati akiingia jijini humo na kupokewa na msururu mrefu wa magari na pikipiki.

Aidha, mara baada ya kumaliza mkutano kwenye viwanja vya Furahisha, barabara ya Airport ilishindwa kupitika kwa zaidi ya nusu saa na kusababisha msururu mrefu wa magari kutokana na wananchi waliokuwa kwenye mkutano huo kuamua kumsindikiza kwa maandamano hadi kwenye ofisi za chama hicho zilizopo eneo la Kona ya Bwiru.

Msafara huo wa Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe jijini Dar es Salaam, ulipokewa majira ya saa 8:00 mchana eneo la Usagara lililopo kilometa zaidi ya 20 kutoka katikati ya Jiji, ambako pikipiki pamoja na magari hayo yalikuwa yakishangiliwa na kupungiwa na wananchi kwenye maeneo mbalimbali waliyopita kabla ya kwenda kwenye viwanja wa Furahisha.

Msafara huo ulilakiwa kwa shangwe na wananchi waliokuwa wamefurika kwenye viwanja hivyo, ambako Mdee na ujumbe wake walifanya mkutano wa uzinduzi wa ziara yao ya kuzunguka mikoa yote ya Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kujiandikisha kwa ajili ya chaguzi za serikali za mitaa.

Aidha, mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo, wananchi waliusindikiza msafara huo huku wakiimba nyimbo za hamasa kuikataa Katiba iliyopendekezwa mpaka kwenye ofisi za Mkoa za CHADEMA.

AMSHUKIA CHENGE
Akihutubia kwenye mkutano huo uliohudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi wa Mwanza na vitongoji vyake, Mdee aliwataka waipigie kura ya hapana Katiba pendekezwa kwa kile alichowaeleza kuwa, mbali ya maoni ya wananchi kupuuzwa lakini inalinda maslahi ya mafisadi.

“Chenge (Andrew), alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, (AG), katika kipindi hicho mikataba mingi mibovu iliingiwa na mpaka leo inawaumiza Watanzania, mikataba ya madini, dhahabu, mikataba ya rada yote aliisimamia, yaani haijawahi kutokea mikataba mibovu kama hiyo popote duniani …

“Leo tunaambiwa ndiye mtu aliyependekezwa kuongoza Kamati ya Uandishi wa Katiba pendekezwa, kwenye rasimu iliyowasilishwa na Tume ya Jaji Warioba, (Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba), aliweka maoni yenu wananchi mliyotaka kuwe na uwazi, uwajibikaji na uadilifu katika uongozi ili kudhibiti mali za umma, lakini Kamati ya Uandishi wakaona kitawabana, wakakiondoa,” alisema Mdee.

Alisema kuwa mapendekezo mengine yaliyoondolewa ni zuio la viongozi wa umma kuwa na akaunti nje ya nchi, ambako ilipendekezwa kama ni muhimu basi iwepo sheria kali kuzidhibiti, jambo alilodai kuwa ilionekana kuwa mwiba kwa viongozi wengi wa CCM wakaamua kuitupa.

“Wananchi walichoshwa na tabia ya wale wanaoona muda wa uchaguzi umekaribia wanakuja kutafuta kura, wakishachaguliwa wanabeba mabegi yao wanarudi mjini…

“Wananchi walitaka wapewe mamlaka ya kuwawajibisha kwa kuwaondoa wawakilishi ambao hawaonekani jimboni badala ya kusubiri kwa miaka mitano, lakini Chenge na wenzake wakaona itawabana wakatupilia mbali,” alisema Mdee.

Alisema kuwa suala la ardhi si la Muungano na Katiba ya Zanzibar iko wazi kwenye hilo, kwani Mtanganyika haruhusiwi kumiliki ardhi lakini jambo la kushangaza ni kuwa masuala ya ardhi yameingizwa katika Katiba pendekezwa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Bawacha Taifa, Hawa Mwaifunga, aliwataka wananchi kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la mkazi siku 21 kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Desemba 14 mwaka huu.

“Hao wanaopita kwa sasa na madaftari huko kuandikisha majina ni wazushi tu, msikubali wawaandikishe kwa sababu hii kazi inatakiwa kufanywa na Ofisa Mtendaji wa serikali na si mabalozi wa CCM, wakataeni tena siku za kujiandikisha zimeainishwa kabisa bado hazijafika,” alisema Mwaifunga.

Kwa upande wake, Katibu wa Bawacha, Grace Tendega, alisema kuwa Serikali inapaswa kuelewa kuwa wananchi wameamka vya kutosha, hivyo hata mbinu zozote za kutaka kuchakachua kura kwenye serikali za mitaa hazitafanikiwa.

Aliongeza kuwa uamuzi wa kusema kuwa kwenye zoezi la upigaji kura wananchi watapaswa kuchora nembo ya chama kwenye karatasi hizo, halina nia njema hata kidogo huku akionya kuwa hila hizo haziwezi kufanikiwa.

Viongozi hao wa Bawacha wako kwenye ziara ya mikoa ya Kanda ya Ziwa, ambako wamepanga kuwahamasisha wananchi kupiga kura ya hapana dhidi ya Katiba pendekezwa na kuwahamasisha kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Desemba 14 mwaka huu.TANZANIA DAIMA
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: