BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

NYUMBA YA SH 89/- MIL YAMCHANGANYA MKUU WA WILAYA IGUNGA, INA VYUMBA VIWILI NA SEBULE TU, NI FEDHA ZA UFADHILI WA BENKI YA DUNIA.


MIRADI ya ujenzi katika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, imeghubikwa na tuhuma za ufisadi, ambapo hivi karibuni imekabidhiwa nyumba ya mwalimu yenye vyumba viwili vya kulala na sebule, ikitajwa kugharimu sh. milioni 89, jamba ambalo limeibua utata na kumlazimu Mkuu wa wilaya hiyo, Elibariki Kingu kuingilia kati.

Gharama ya ujenzi wa nyumba hiyo katika shule ya sekondari Ichama kata ya Chabutwa ni sehemu ya matumizi ya kiasi cha sh. milioni 219 zilizotolewa na Serikali kuu kupitia mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.

Uchunguzi wa Tanzania Daima Jumatano, umebaini kuwa mbali na kiasi hicho pia katika muendelezo wa matumizi ya fedha hizo, sh. milioni 8.6, zimetumiwa kwa ajili ya kujenga tanki la kuvunia maji ya mvua katika nyumba hiyo, hali inaibua maswali kwa wakazi wa Chabutwa kutokana na ubora wa nyumba yenyewe na gharama zinazotajwa kutumika.

Kutokana na utata huo, tayari mkuu wa wilaya ya Igunga, Elibariki Kingu, ameingilia kati na kutaka malipo ya mradi huo yasitishwe huku akiagiza wataalam wa halmashauri kufanya tathmini upya kuthibitisha kama thamani ya fedha inalingana na ubora wa nyumba.

Oktoba 8 mwaka huu, wakati kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Rache Kasanda akiikagua nyumba hiyo ya mwalimu baada ya kuifunga, alisikika akisifia kuwa ni bora kwa kile alichoeleza kuwa haina dalili yoyote ya nyufa.

Gazeti hili lilipomhoji juu ya gharama zilizotajwa katika taarifa ya halmashauri kama zinarandana na ubora wa nyumba, Kasanda alisema wahusika walimueleza kuwa gharama zilizoandikwa katika taarifa zilikuwa zimekosewa na kwamba nyumba imegharimu sh. milioni 38 na si 89 iliyosoma kwake.

“Wasaidizi wangu ulioongea nao awali waliniambia juu ya hilo na nikafuatilia na mkurugenzi ameniambia walikosea katika kuandika na kwamba gharama zake ni sh. milioni 38,” alisema Kasanda akiwa katika kata ya Simbo.

Nyumba hiyo ina vyumba viwili vya kulala visivyokuwa na vyoo vya ndani, sebule moja pamoja na madirisha manne yaliyowekwa nondo na nyavu, huku sakafu yake ikiwa ya kawaida ya saruji na kuezekwa kwa bati.

Kwa mujibu wa taarifa fupi ya ujenzi iliyosomwa kwa kiongozi wa mbio za mwenge, mbali na sh milioni 89 gharama za nyumba hiyo, pia zimetumika sh .milioni 58.5 kwa ajili ya ujenzi wa chumba cha maabara, sh. milioni 38.8 kwa ajili ya vyumba viwili vya madarasa na sh. milioni 23.9 kwa ununuzi wa samani.

Mmoja wa maofisa wa Kampuni ya ukandarasi ya Elisha & Son Ltd ya mjini Igunga, iliyopewa kazi ya ujenzi wa majengo hayo, alipoulizwa gharama za nyumba ya mwalimu alisema hazizidi sh. milioni 50 na si chini ya milioni 40.

“Kama wanasema ni sh. milioni 89 sasa unanifumbua macho labda kuna mkataba unaotuhusu sisi na ule unaohusu taarifa zao mbele ya umma lakini hizo gharama za nyumba hazifiki huko,” alisema.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Igunga, Rustruka Turuka alipoulizwa gharama halisi ya jengo hilo, alielekeza swali hilo kwa Afisa Elimu Sekondari, Aloyce Kaziyareli ambaye alisema gharama zilizosomwa siku ya uzinduzi ndizo zinapaswa kufuatwa.

“Gharama ni hizo hata hiyo nyumba ndiyo gharama yake, sasa ukitaka kujua zimefikaje hayo ni maswali ya Mkandarasi,” alisema Kaziyareli.

Jana, mkuu wa wilaya ya Igunga, Elibariki Kingu, alizungumza na gazeti hili na kukiri kuwaita badhi ya maofisa wa halmashauri katika ofisi yake kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa ubora wa mradi huo na fedha zilizotumika.

Alisema baada ya kuongea nao aliwaagiza kusitisha malipo kwa mkandarasi na kisha mthamini wa ujenzi wa halmashauri awasilishe taarifa yake ya kukubali jengo hilo la walimu kuwa na thamani ya sh. milioni 89.

Kwa mujibu wa Kingu, baada ya hatua hiyo wataalam mbali mbali wataenda kufanya tathmini upya kuthibitisha kama nyumba iliyojengwa ina thamani ya fedha iliyotajwa.

Huyu aliyepitisha BOQ ya fedha hizo tunamtaka ajieleze kwa kuwa jengo halilingani na thamani ya fedha iliyotajwa,” alisema Kingu.TANZANIA DAIMA
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: