BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

TAHADHARI YA EBOLA: MKOA WA KILIMANJARO YATENGA VITUO VINNE VYA EBOLA.

Kilimanjaro yatenga vituo vinne vya ebola
MKOA wa Kilimanjaro umetenga vituo vinne kwa ajili ya karantini ya wagonjwa wa ebola iwapo watathibitishwa kitaalamu kwamba wanaugua ugonjwa huo ili kuepuka madhara zaidi kwa jamii inayowazunguka.

Vituo hivyo vimetajwa kuwa ni katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (Kia), Holili,Tarakea wilayani Rombo pamoja na Shirimatunda iliyopo katika manispaa ya Moshi kama tahadhari za jinsi ya kukabiliana na tishio la ugonjwa huo kama utaingia mkoani humo.

Mkuu wa mkoa huo, Leonidas Gama alisema hayo wakati akitoa ufafanuzi wa hofu iliyokuwa imewakumba wakazi wa Manispaa ya Moshi kufuatia taarifa za kuwapo kwa mtu aliyekuwa akidhaniwa anaugua ugonjwa huo.

"Niwatoe hofu wakazi wa mkoa huu kwamba, hivi vituo vinne nilivyovitaja, havijatengwa leo au jana, hii ni tangu taarifa za awali kuripotiwa kwamba ugonjwa huu upo katika baadhi ya nchi za Afrika Magharibi,"alisema.

Alisema kutengwa kwa vituo hivyo, ni kutokana na ukweli kwamba mkoa huo upo mipakani na nchi jirani ikiwamo Kenya na kuwapo kwa uwanja wa ndege wa Kia ambao unaingiza wageni wengine kutoka mataifa mbalimbali duniani kwa ajili ya shughuli za utalii na biashara.

"Mkawatoe hofu wananchi kwamba hadi sasa haijathibitika kimaabara kwamba ugonjwa wa ebola umeingia Tanzania hususani mkoa wa Kilimanjaro kama ambavyo wasiwasi uliwakumba wananchi, watalii waendelee kuja mkoani kwetu," alisema.

Wiki iliyopita serikali mkoani hapa iliwaweka karantini, watu watano akiwamo mgonjwa anayehofiwa kuwa na ugonjwa huo, wauguzi na wataalamu wengine wa afya wanne wa zahanati ya Shirimatunda, manispaa ya Moshi kupisha vipimo ili kuchunguza kama ni ugonjwa huo au la.

Hata hivyo, uchunguzi wa awali umebainisha kuwa mgonjwa huyo aliyetokea nchini Senegal kibiashara, anasumbuliwa na malaria kali na tayari sampuli za vipimo zimechukuliwa kupelekwa Nairobi nchini Kenya, kuangalia kama malaria hiyo haijaambatana na ugonjwa wa ebola.

Gama alisema wataalamu wa afya katika manispaa hiyo walimgundua mgonjwa huyo Oktoba 22 mwaka huu kulingana na maelezo binafsi aliyoyatoa ingawa sasa ametibiwa na afya yake inaonekana kuanza kuimarika.

Naye Mganga Mkuu wa mkoa huo, Dk Mtumwa Mwako alisema wataalamu wa afya katika zahanati hiyo wataendelea kuwa katika karantini bila kufika katika familia zao hadi hapo itakapothibitishwa kwamba mgonjwa wanayemhudumia haugui ebola.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: