BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KAULI YA "WAPIGWE TU" YAJIRUDIA WAKATI HOJA YA PROF LIPUMBA IKIJADILIWA BUNGENI DODOMA.

Spika wa Bunge, Anna Makinda akifafanua jambo bungeni. 

Bunge la Jamhuri ya Muungano leo limejadili kitendo cha uvunjifu wa amani uliotokea kwenye maandamano ya CUF yaliyoongozwa na Profesa Ibrahimu Lipumba jijini Dar es Salaam


Katika mjadala huo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mathias Chikawe aliomba suala hilo kupewa muda wa kufanyiwa uchunguza yakinifu na vyombo husika, wakati Mwanasheria Mkuu George Masaju akitaka suala hilo lisijadiliwe bungeni kwa kuwa tayari limeshafikishwa Mahakamani.


Kabla ya mjadala huo Waziri Chikawe alisoma taarifa yake ya kile kilichotokea kwenye vurugu hizo huku akieleza kuwa taarifa za uchunguzi wa ndani ndizo zililishawishi jeshi la Polisi kuwaomba Cuf kutofanya maandamano yao.


Waziri Chikawe amelieleza Bunge kuwa baada ya taarifa za polisi kutolewa wafuasi wa Chama hicho hawakutaka kutii amri hiyo, hivyo ili kunusuru uvunjifu mkubwa wa Amani ambao ungeweza kutokea walilazimika kutumia nguvu kuwatawanya wafuasi hao wa CUF waliokuwepo.


“Nchi yetu inaongozwa kwa mujibu wa sheria na kanuni, haitakuwa busara kila mtu kujifanyia mambo yake anayotaka bila kuzingatia sheria, nimeagiza vyombo husika kuchunguza suala hili, na ikibainika kuwa polisi walitumia nguvu kubwa watawajibishwa kwa mujibu wa sheria. Amesema Chikawe.


Baada ya kauli hiyo ndipo Mwanasheria Mkuu wa Serikali alipolieleza bunge kuwa tayari kesi hiyo imeshafikishwa mahakamani, hivyo kujadili suala hilo bungeni ni kukiuka sheria ya mgawanyo wa madaraka katika mihimili ya dola,jambo ambalo lilipingwa na idadi kubwa ya wabunge.


Pamoja na hayo Spika Anna Makinda alitoa muda wa dakika 10 kwa wabunge kujadili suala hilo huku mbunge Tundu lissu akilaani vikali kutokea kwa vurugu hizo na akitaka kuwajibika kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Mwanasheria Mkuu pamoja na waziri Chikawe kwa kuwa vitendo vinavyoendelea vinashabihiana kabisa na kauli yake ya ‘wapigwe tu’.


Aidha wabunge wengi wa kambi ya upinzani wakichangia hoja hiyo kwa jazba walionyesha kukerwa na kuzilaani vurugu hizo, huku wabunge wa CCM wakitaka kusimamiwa kwa sheria bila kupendelea mtu yeyote.


Pamoja na hayo mtoa hoja ambaye ni Mbunge na Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi James Mbatia amesema kuwa suala la Amani ya nchi ni suala la kitaifa na halitakiwi kuingizwa kwenye siasa, hivyo aliwasihi wabunge kuwa makini na suala hilo


“Amani na usalama wa nchi yetu ni kitu muhimu sana katika ustawi wa taifa letu, kila siku tunashuhudia kuendelea kuporomoka kwa amani na usalama, ninawasihi wabunge wenzangu, tunapojadili suala kama hili lazima tuweke kando itikadi zetu, lengo likiwa kuliponya taifa, Amesema Mbatia.


Naye Spika Makinda alihitimisha kwa kusema kuwa anaiagiza Serikali kufanya uchunguzi kupitia vyombo vyake, pia bunge litachunguza sheria ambazo zinatoa mwanya wa vurugu ili kudhibiti vitendo hivyo.


Kwa habari Zaidi usiache kusoma gazeti lako la Mwananchi kesho, ama jiunge na Epaper www.epaper.mcl.co.tz
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: