BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

EFD YACHONOA WAFANYABIASHARA TENA NA KUZALISHA MGOMO TANZANIA.

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhAB2hdwStqDW9tr0NupHdrij-W3bb6M4vssJeLefabywPK4Q-cU7Cozi-7lEV3_EGsuy2qLaFXiyochtQcBibFyMFUg-82N6dwhg5rSXyHK0uq_14riffjtY-tIM8CKiURQicUpiq1DI5b/s1600/efd-machine.jpg
WAKATI Mwenyekiti wa Jumuia ya Wafanyabiashara Tanzania, Johnson Minja (34) akipandishwa jana kizimbani, mgomo wa wafanyabiashara umesambaa katika maeneo mbalimbali nchini, kama njia ya kushinikiza kuachiwa kwa kiongozi wao huyo.

Hadi jana gazeti hili lilithibitishiwa kuwa licha ya Dar es Salaam, ambako mgomo huo ulianza juzi, sasa umesambaa katika mikoa ya Tanga, Iringa, Dodoma na Mwanza, hali ambayo imefanya upatikanaji wa huduma usiwepo katika mikoa hiyo.

Minja apanda kizimbani Dodoma
Minja ambaye ni mkazi wa Kinondoni Jijini Dar es Salaam, jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma Mjini, akikabiliwa na makosa ya kuwachochea wafanyabiashara wasilipe kodi kwa serikali.

Kesi hiyo ambayo iko mbele ya Hakimu Mkazi, Rebecca Mbiu ilivuta hisia za watu hivyo kufanya idadi ya watu wengi, wakiwemo wafanyabiashara kufurika mahakamani hapo na hivyo kuifanya polisi kuimarisha ulinzi.
 

Maduka yakiwa yamefungwa katika moja ya mitaa ya jiji la Dar es Salaam

Umati mkubwa wa wafanyabiashara, walifika mahakamani hapo kumshuhudia Minja akisomewa mashtaka yake huku ulinzi ukiwa umeimarishwa mahakamani hapo, kutokana na kile kilichokuwa kikielezwa wafanyabiashara wa Dar es Salaam watafika Dodoma kumshuhudia mwenyekiti wao akisomewa mashtaka.

Akimsomea mashtaka yake Wakili wa Serikali, Godfrey Wambali alidai Kuwa Septemba 6, mwaka jana katika Chuo cha Mipango Dodoma, mshtakiwa akiwa kama Mwenyekiti wa Jumuia ya Wafanyabiashara Tanzania aliwashawishi Jumuia ya Wafanyabiashara wa Dodoma wasilipe kodi.

Katika shtaka la pili ilidaiwa kuwa Septemba 6, mwaka jana, katika Chuo cha Mipango mshtakiwa aliwapa maelekezo wafanyabiashara wa Dodoma wasitumie mashine za kodi za kielekroniki (EFD) za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambazo zilitengenewa kwa ajili ya kuwezesha kukusanywa kwa kodi.

Mshtakiwa huyo ambaye alikamatwa jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki na kusafirishwa hadi Dodoma kwenda kujibu tuhuma hizo, alikana mashaka hayo.

Wakili wa Serikali alisema upande wa mashitaka wa serikali, hauna pingamizi dhidi ya dhamana, ila anamuomba Hakimu kuzingatia umbali wa anakoishi mtuhumiwa wakati atakapokuwa akitoa masharti ya dhamana.

Kwa upande wake, Wakili wa utetezi, Godfrey Wasonga alimwomba hakimu kuzingatia haki ya mtuhumiwa, kutokana na kuwa ni mtu anayeaminiwa na wafanyabiashara kote nchini hivyo hataweza kutoroka na hivyo akaiomba mahakama hiyo isiweke masharti magumu ya dhamana.

Kutokana na hoja hizo mbili, Hakimu Mbiu alitoa masharti ya dhamana kwa kumtaka mshitakiwa huyo kuwa na wadhamini wawili na mmoja wapo akiwa mtumishi wa Serikali na wote wawili wawe na mali isiyohamishika, yenye thamani isiyopungua milioni nne. Kesi hiyo imepangwa kutajwa tena Februari 11, mwaka huu.

Tanga wapinga Minja kukamatwa

Huko Tanga wafanyabiashara wa jiji hilo, nao walifunga maduka kwa muda usiojulikana na wakadai wataendelea kufunga hadi hapo vyombo vya dola vitakapomwachia Minja.

Msimamo huo ulitangazwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara (JWT) Mkoa wa Tanga, Peter Kimaro. Alisema hayo alipohojiwa na gazeti hili jana kuhusu mgomo wa wafanyabisha hao, ulioanza jijini humo jana.

Alisema lengo la kufunga maduka yao ni kuitikia mwito wa wafanyabiashara wenzao walioko jijini Dar es Salaam, ambao walianza mgomo huo jana, ikiwa ni njia ya kuishinikiza Serikali imwachie Minja ambaye ameagizwa na JWT kuendelea kuhamasisha wafanyabiashara kupinga matumizi ya EFD.

“JWT inawahimiza wafanyabiashara wote kulipa kodi halali kwa sababu bila kodi nchi haiwezi kwenda …napenda ieleweke kwamba tukio la leo la kufunga maduka limefanywa na wafanyabishara wenyewe na kamwe halitokani na viongozi wetu wa kitaifa kama Serikali inavyodhani”, alisema.

Kimaro alisema kitendo alichofanyiwa mwenyekiti wao huyo, kimewashangaza na kuwatia hofu kubwa, wakiamini kwamba Serikali haikuwatendea haki, hasa ikizingatiwa kwamba tayari mazungumzo kuhusu malalamiko yao hayo ya EFD, yalikuwa yakiendelezwa baina yao na Waziri wa Viwanda, Naibu Waziri wa Fedha na Kamishna Mkuu wa TRA ili kupata suluhisho.

“Tunawaomba radhi wananchi kwa kuwanyima huduma, lakini pia tunaomba watuelewe kwamba tunafanya hivi ili kunusuru hatma ya kiongozi wetu ambaye wafanyabiashara tumemtuma... tutaendelea kuyafunga mpaka haki itendeke na kwa hili tuko tayari kufa njaa hadi hapo kitakapoeleweka”, alisema.

Katibu Mtendaji wa JWT mkoa wa Tanga, Yahya Chawalla alisema analaani kitendo cha kukamatwa Mwenyekiti wao huyo wa kitaifa na kuomba wahusika wamwachie, kwa kuwa alikuwa akitekeleza matakwa ya wanachama wake na sio maslahi yake binafsi kama inavyodhaniwa.

Iringa wasambaza vikaratasi

Huko Iringa wafanyabiashara mjini Iringa, wengi wao wakiwa ni wale wa biashara za madukani wameingia katika siku ya kwanza ya mgomo wao, wakipinga kukamatwa na Polisi kwa kiongozi wao wa Kitaifa, Johnson Minja.

Taarifa ya vikaratasi yenye maneno “Kwa Pamoja Tunaweza” ilisambazwa kwa wafanyabiashara hao juzi. Hata hivyo, taarifa hiyo haikusainiwa na mtu yoyote.

Kupitia vikaratasi hivyo, wafanyabiashara hao walihamasishana kwamba jana wasingefungua maduka nchi nzima kwa sababu ya kukamatwa kwa kiongozi wao.

Wakionekana kutekeleza kile kilichoandikwa katika vikaratasi hivyo, jana maduka mengi ya katikati ya mji wa Iringa, yalikuwa yamefungwa kutwa nzima na kusababisha usumbufu mkubwa kwa baadhi ya watu waliokuwa wakihitaji mahitaji.

Mgomo huo ulidaiwa kuwa uliathiri pia baadhi ya maeneo ya wilaya za Kilolo, Iringa Vijijini na Mufindi.

Akizungumzia usumbufu wanaopata wananchi wanaohitaji huduma katika maduka hayo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema, “Nimeshindwa kukutana na viongozi wa wafanyabiashara wa mkoa wa Iringa leo, lakini taratibu zinaendelea kufanywa ili nikutane nao kesho Alhamisi.”

Mwanza nao wafunga

Kwa jijini Mwanza wafanyabiashara wa maduka, walifungua biashara zao kama kawaida, lakini ilipotimu saa 4 asubuhi walifunga maduka hayo kwa kile walichodai kuwa wanaungana na wenzao wa Dar es Salaam kumsaka mwenyekiti wao wa taifa.

Kufungwa kwa maduka hayo, kulisababisha watu waliofika katikati ya jiji kwa ajili ya kununua bidhaa, kushindwa kukidhi mahitaji yao.

Maduka yalianza kufungwa katika maeneo ya Miti Mirefu na baadae maeneo ya Stendi na ilipofika majina ya saa 5 asubuhi vijana walionekana katika barabara ya Nyerere, wakihamasisha wafanyabiashara kufunga maduka yao.

Wafanyabiashara hao wa jijini hapa, waliahidi kufunga maduka kwa muda usiojulikana mpaka hapo mwenyekiti wao huyo, atakapoachiwa na Jeshi la Polisi.

Hali hiyo ilisababisha kusimama kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi kwani baadhi ya wafanyabiashara walifunga maduka na kurudi majumbani kwao.

Mmoja wa wafanyabishara hao, Said Mageye alidai Serikali inatakiwa kukaa pamoja na uongozi husika ili kutatua tatizo lililopo, badala ya kuendesha ‘kamatakamata’ ambayo ni adha kwa Watanzania na hata wafanyabishara wakubwa kutoka nje ya nchi.

“Serikali inatakuwa kufikiria shida wanazopata wananchi na wasiwe wanafikiria upande mmoja wakidhani kuwa wanatukomoa, wajue na wao pia wanajikomoa,kwani nchi yenye amani haiendeshwi kibabe,” alisema.

Devotha Edward ambaye ni mfanyabiashara mdogo, alisema baadhi yao wanafurahia maduka makubwa kufungwa. Lakini, alisema wapo watu walioathirika kwa sababu wanategemea kununua mali kwa wafanyabiashara wakubwa waliofunga maduka yao.

Edward alisisitiza kuwa jambo hilo ni janga kwa watu wote na wafanyabiashara wa sekta zote, kuanzia wale wenye biashara ndogo hadi kubwa.

Dar washikilia msimamo

Wafanyabiashara wa soko la Kariakoo wamesema hawatafungua maduka yao na kuendelea na biashara mpaka Jeshi la Polisi litakapomuachia Minja na kwamba kauli mbiu yao ni ‘Mwenyekiti kwanza, biashara baadaye’.

Jana ikiwa ni siku ya pili ya mgomo huo, maduka ya Kariakoo mengi yalikuwa yamefungwa huku wenye maduka wakiwa wamekaa nje ya maduka yao kwa madai kwamba hawawezi kufungua wanasubiri taarifa za Mwenyekiti wao Minja kuachiwa.

HabariLeo ilishuhudia pia mara kwa mara magari ya polisi yakiwa na askari yakipita katika mitaa ya Kariakoo, wakiimarisha ulinzi mara kwa mara.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Jumuia ya Wafanyabiashara Tanzania, Sulaiti Kayemba alisema wafanyabiashara wameendelea kufunga maduka yao na hawatayafungua kamwe kwasababu hawajui ni nini kitamkuta kiongozi wao huyo.

“Hatuwezi kufungua maduka yetu kamwe kwa sababu Minja hajaachiwa na pia hiyo ni kesi, hatujui nani na nani wataunganishwa katika kesi hiyo lakini kwa fununu tu tunasikia eti amehamasisha watu wasitumie mashine za mlipa kodi, hii sio kweli,” alisema Kayemba.

Alisema jambo la kushangaza ni kwamba kuhusu mfumo huo wa mashine za mlipa kodi, iliundwa kamati ya watu wa TRA na pia wafanyabiashara kwaajili ya kutafuta muafaka, lakini wakati kamati hiyo ikiendelea na kazi kiongozi wao amekamatwa.

Katika mahojiano na baadhi ya wafanyabiashara, ambao walikua nje ya maduka yao walisema kwamba wako tayari kufunga maduka yao hata kwa mwezi mzima ili mradi wamtetee kiongozi wao, ambaye wanaamini kwamba hana makosa na kwamba wakifungua itakuwa kama kumsaliti.

“Mgomo huu ni kuionesha Serikali kuonesha umoja na mshikamano wetu na waliofunga hawajalazimishwa ila ni kwa hiari yao wenyewe,” alisema Issa Azam.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi TRA, Richard Kayombo alisema TRA isihusishwe na kukamatwa kwa Minja na kwamba kama kuna maelezo yoyote, basi polisi ndio wanaohusika.

“Kamati iliundwa na inaendelea na kazi yake, TRA isihusishwe na kukamatwa kwa Minja, maelezo ya kwanini alikamatwa yanapatikana Polisi,” alisema Kayombo.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: