Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher ole Sendeka
MJI wa Mirerani uliopo wilayani Simanjiro mkoani Manyara unadaiwa kuvamiwa na raia wa nje wanaotuhumiwa kuendesha vitendo vya kihuni.
Vitendo hivyo ni pamoja na kuwafanyia fujo viongozi wa serikali na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaofanya ziara katika mji huo.
Hayo yalisemwa na Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher ole Sendeka alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa MAREMA tawi la Mirerani.
Sendeka alisema kuwapiga mawe ,chupa za maji na kumwagiwa vumbi baadhi ya viongozi , kwa asilimia kubwa kunafanywa na raia wa nje wanaoishi kwenye mji huo bila vibali.
Alisema inasikitisha kuona kuwa viongozi wa serikali na chama wakifanya ziara katika mji huo kukagua maendeleo wanafanyiwa vurugu na raia hao na dola inawaachia wakati wako hapa nchini kinyume na sheria.
Mbunge huyo alisema kuwa tabia ya Watanzania sio kufanyia vurugu viongozi wao lakini alipofanya uchunguzi aligundua wengi wao ni raia kutoka nje ya nchi. Alisema kamwe hawezi kuunga mkono vitendo hivyo.
Alisema hata kama atanyimwa kura katika mji huo wa Mirerani haimsumbui bali anataka kuona watu wakiwa na busara na ustaarabu.
‘’Sitaki kura katika mji wa Mirerani zenye tabia mbaya dhidi ya viongozi wake hilo siwezi kulivumilia kamwe na kama mnataka niwalinde kwa ujinga huo mimi sitaki kamwe na kura zenu msinipe kabisa.’’
‘’Naona na ninashuhudia viongozi wangu mnawapiga mawe na chupa za maji na ikitokea mtu akinipiga cha moto atakiona mimi sijali chochote,’’ alisema Sendeka.
Pia alitumia fursa hiyo kuwaasa wachimbaji wadogo wadogo kuheshimu wawekezaji kwani serikali iliyopo madarakani imewaweka kisheria hivyo hawapaswi kusumbuliwa kwa masuala binafsi.HABARILEO

0 comments:
Post a Comment