POLISI ACHENI MATUMIZI MAKUBWA YA NGUVU.
Juzi, Jeshi la Polisi lilirusha mabomu ya kutoa machozi, risasi za moto na maji ya kuwasha dhidi ya wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) jijini Dar es Salaam.
Polisi hao walifanya hivyo wakati wakizuia msafara wa Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, uliokuwa ukielekea eneo la Zakhem, Mbagala jijini Dar es Salaam ambako kuliandaliwa kufanyika mkutano wa hadhara.
Inaelezwa kuwa Profesa Lipumba alitarajiwa kwenda kutoa taarifa kwa wafuasi wa chama chake waliokuwa tayari wamekusanyika, kuwa mkutano na maandamano yao yamezuiliwa na Polisi.
Mkutano na maandamano hayo, vilipangwa kufanyika kwa lengo la kuwakumbuka wanachama wenzao zaidi ya 30 waliouawa Januari 27, mwaka 2001 wakati wakiandamana kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2000.
Katika kufanya hivyo, juzi Jeshi la Polisi lilimtia nguvuni Profesa Lipumba pamoja na wafuasi wengine wa chama hicho takriban 40.
Waliofuatilia tukio hilo kupitia kwenye runinga, waliwashuhudia polisi wengi waliovalia sare na kiraia wakiwa na bunduki na virungu, wakitembeza kipigo dhidi ya wafuasi wa CUF ambao hawakuonekana kuwa na silaha.
Mbali na kutembeza kipigo kwa wafuasi hao wa CUF, pia polisi walivurumisha ovyo mabomu ya kutoa machozi kiasi cha kuwadhuru hata wasiokuwamo.
Zipo taarifa kwamba, moshi wa mabomu hayo, pia uliwafikia wanafunzi wa shule moja ya chekechea ya Mango, Mtoni Mtongani iliyokuwa jirani na tukio na kuzua taharuki kubwa kwa watoto hao wasio na hatia.
Inasemekana baada ya mabomu hayo kurushwa, wanafunzi hao wengi wao wa umri mdogo, walitawanyika ovyo na kukimbia kujaribu kujiokoa, jambo ambalo ni la hatari kwa usalama wao.
Sisi tunaamini kwamba kitendo hiki kilichofanywa na Jeshi la Polisi, si cha kiungwana na kinastahili kukemewa na wapenda amani wote.
Tunasema hivyo kutokana na imani yetu kwamba polisi wangeweza kutumia namna nyingine ya kuepuka matumizi nguvu kama ilivyoshuhudiwa juzi.
Kimsingi, hatuoni kama Jeshi la Polisi lilikuwa na sababu za msingi kufanya yale yaliyoonekana na mwishowe kuibua sintofahamu iliyosababisha hata shughuli za Bunge kuahirishwa bungeni jana.
Hii ni kutokana na ukweli mwingine kwamba hakukuwa na taarifa zozote za kudai kwamba wafuasi wa CUF walikuwa na silaha au kuandamana kwa dhamira ya kufanya fujo. Hata taarifa za polisi hazijaeleza kuwapo kwa tuhuma zozote za aina hiyo.
Kinachoshangaza ni kwamba, wakati Polisi wakiendelea kutumia nguvu kubwa katika matukio ya kisiasa, kasi kama hiyo haioenekani kwa kiwango sawa katika kudhibiti uhalifu, hususan majambazi ambao wamefikia hatua ya kujitwalia silaha kutoka mikononi mwao.
Kwa mfano, ni wiki iliyopita tu, kituo cha Polisi cha Ikwiriri mkoani Pwani, kilivamiwa na majambazi, askari wawili wakauawa na silaha zikaporwa, zikiwamo bunduki aina ya SMG, SAR na risasi kadhaa.
Mbali ya tukio hilo, pia zipo taarifa za matukio ya majambazi yanayoendesha uhalifu wa kutumia silaha yatakavyo katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam ikiwamo Kimara jirani na kituo cha polisi, Mbezi Malambamawili, Tabata na maeneo mengine mengi nje ya Dar es Salaam, ikiwa ni pamoja na jijini Tanga ambako kuna taarifa kuwa askari wawili waliporwa bunduki zao na risasi takriban 60 baada ya majambazi wenye visu kuwavamia wakati wakiwa kwenye doria.
Majambazi wanazidi kuzua hofu kutokana na baadhi ya polisi wetu kuzidiwa, tena na wahalifu walio na silaha dhaifu kulinganisha na zile walizo nazo kama ilivyodhihirika katika baadhi ya matukio kama hilo la Tanga.
Sisi tunashauri kwamba nguvu hizi kubwa za polisi dhidi ya raia wasiokuwa na silaha za aina yoyote ziepukwe. Badala yake, wazielekeze katika kudhibiti wahalifu.
Kinyume chake, kuna hatari kwamba polisi watajiharibia taswira yao mbele ya jamii kwa kuonekana kuwa labda ni kweli hujiekeleza zaidi katika kudhibiti wanasiasa badala ya wahalifu wanaofikia hatua ya kuvamia vituo vyao.
Shime, polisi jiepusheni na mwenendo huu wa kutumia nguvu kubwa katika kuzima harakati za amani za kisiasa kwani kufanya hivyo ni kuviza misingi ya demokrasia.
Hivi kwa mfano, kama polisi wangeamua kuwaongoza wafuasi hao wa CUF hadi eneo lao la mkutano, kungetokea vurugu gani?
Tunalisihi Jeshi la Polisi litumie tukio hili na mengine mengi yaliyowahi kutokea hapo kabla kuhakikisha kwamba linatekeleza majukumu yake kwa weledi. CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment