BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

RAIS JAKAYA KIKWETE AWACHIMBA MKWARA MZITO WATAODHUBUTU KUFANYA VURUGU KATIKA UCHAGUZI MKUU.


Rais Jakaya Kikwete.

Dar es Salaam.
Rais Jakaya Kikwete ametuma ‘ujumbe mzito’ dhidi ya watakaofanya vurugu ama kuvuruga Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka huu, akisema watachukuliwa hatua kali.

Rais Kikwete, ambaye atakuwa akimaliza kipindi chake cha miaka kumi tangu akabidhiwe nchi mwaka 2005, ametoa kauli hiyo ikiwa ni wiki chache baada ya uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa kutawaliwa na vurugu na ukiukwaji wa sheria na taratibu na kusababisha wakurugenzi sita kutenguliwa ajira zao wakati wengine watano wakisimamishwa ili kupisha uchunguzi.


“Hatua za kinidhamu zilizochukuliwa na Serikali dhidi ya watu waliovuruga Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwishoni mwa mwaka jana ni ujumbe mzito kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba,” alisema Rais Kikwete juzi wakati akizungumza na mabalozi wa nchi mbalimbali Ikulu jijini Dar es Salaam.


“Tunatuma ujumbe mzito kwamba matukio hayo hayatavumiliwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2015,” alisema Rais Kikwete.


Katika uchaguzi huo uliofanyika Desemba 24, baadhi ya wafuasi wa vyama mbalimbali vya siasa, wamekamatwa na wengine kufikishwa mahakamani kutokana na kufanya vurugu wakati, kabla na baada ya uchaguzi huo.


Mbali na kukamatwa watu hao, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Hawa Ghasia Desemba 17, 2014, aliwasimamisha kazi wakurugenzi wa halmashauri mbalimbali kutokana na kuchelewa kuandaa na kupeleka vifaa vya kupigia kura.


Pia, walitimuliwa kazi kutokana na uzembe kutekeleza majukumu yao katika Uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba 14 na 20 mwaka jana.


Vyama vya siasa, CUFna Chadema vimeendelea kulalamikia matokea ya uchaguzi huo, ambao CCM ilipata ushindi mkubwa, lakini ikapoteza baadhi baadhi ya mitaa iliyokuwa ngome ya chama WRais Kikwete alisema licha ya vurugu katika baadhi ya maeneo nchini, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa umeonyesha kukua na kukomaa kwa demokrasia nchini.


Hata hivyo, tamko lake halikupokewa vizuri na viongozi wa vyama vya upinzani.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Bara, John Mnyika, alisema badala ya kuzungumzia vurugu, Rais alipaswa kuwaeleza mabalozi amemchukulia hatua gani Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa kutengeneza kanuni mbovu zilizosababisha uchaguzi uvurugike.


“Aidha, alipaswa aeleze amemchukulia hatua gani Pinda kwa kujibu bungeni kuwa maandalizi yote ya uchaguzi yalikuwa tayari, ikiwamo bajeti kumbe hali ni tofauti na hivyo kuathiri upatikanaji wa vifaa na ubora wa uchaguzi,” alisema Mnyika.


Pia, alisema inawezekana wakurugenzi waliosimamishwa walikataa kutii maelekezo ya kuhujuhumu upinzani.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Magdalena Sakaya alisema japokuwa Serikali iliwatimua kazi wakurugenzi ambao hawakuwajibika ipasavyo kwenye uchaguzi huo, bado matatizo yanaendelea.


“Wakurugenzi wamepewa adhabu na wengine wamefukuzwa, lakini tatizo limeendelea kubaki pale pale. Leo wakurugenzi wanawaapisha watu ambao hawakushinda, hizi nazo ni kasoro,” alisema.


Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally amesema alichofanya Rais ni kuwakumbusha wasimamizi wa uchaguzi kuwa makini wakati wa kusimamia mpango huo kwa kuwa zipo sheria zinazoliongoza na kutoa adhabu kwa anayekiuka.


“Sheria ya Uchaguzi Mkuu inataja adhabu, labda kisiasa anaweza kusema tu. Hata hao wakurugenzi waliofukuzwa kazi hawakuondolewa kwa sheria ya uchaguzi, waliondolewa kwa njia nyingine,” alisema.


Bashiru alieleza kuwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa haukusimamiwa na NEC, ndiyo maana Serikali imetangaza kuwa kuanzia mwakani utasimamiwa na tume hiyo.


Kimataifa
Rais Kikwete alisema mpaka sasa, Tanzania imetoa zaidi ya askari 3,000 kwenye Operesheni za Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kulinda amani katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Darfur nchini Sudan na Lebanon.


Alisema kutokana na idadi hiyo, Tanzania inakuwa nchi ya sita kwa kuchangia walinda amani wengi barani Afrika na ya 12 duniani.


“Siku zote tumekuwa msaada na tutaendelea hivyo ili kuhakikisha kuwa mashariki mwa DRC kunakuwa huru bila makundi ya watu wenye silaha yanayotishia amani ya Congo na majirani zake,” alisema Rais Kikwete.


“Uwakilishi wowote mbaya unafanywa na watu wanaojifanya kuijua Tanzania na kukifanya kile wanachokiamini kuwa kweli. Hili halikubaliki na ni jambo la aibu. Linafanywa na watu wenye nia mbaya na nchi yetu.”


Kuhusu elimu, Rais alisema Serikali ina mpango wa kutoa bure elimu ya sekondari kuanzia mwakani kwa lengo la kuwafanya Watanzania kupata elimu ya msingi na sekondari bure.MWANANCHI.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: