BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

TAKUKURU YAWAGWAYA MAWAZIRI WALIOKUMBWA NA KASHFA YA ESCROW.

http://www.ippmedia.com/media/picture/large/Hosea-june9-2014.jpg
Dar es Salaam. Wakati wananchi wakisubiri vigogo wa serikalini na mawaziri wanaotuhumiwa kuhusika kwenye kashfa ya uchotaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow kufikishwa mbele ya vyombo vya umma, ni watumishi watano tu wa umma waliofikishwa mahakamani, lakini Mkurugenzi wa Takukuru, Dk Edward Hoseah ana jibu la suala hilo; kazi yao ni kufikisha mahakamani ‘vidagaa’.


Katika kashfa hiyo ya Sh306 bilioni, mawaziri wa sasa na zamani pamoja na makatibu wakuu wa wizara, wanatuhumiwa kwa njia moja au nyingine kuhusika kwenye kufanikisha kwa makusudi au uzembe uchotwaji wa fedha hizo, kuikosesha mapato Serikali na kupokea mgawo wa fedha hizo, lakini hadi sasa ni watumishi wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Tanesco na Benki Kuu (BoT) pekee waliofikishwa mahakamani.


Wote watano, ambao ni vigogo kwenye taasisi zao, wameshtakiwa kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ili kufanikisha mkakati huo ulioibuliwa na gazeti la The Citizen na baadaye Bunge kulidaka na kufikia maazimio ya kutaka wahusika wote wawajibishwe na mamlaka zinazowahusu.


Juzi, mkurugenzi huyo wa Takukuru aliliambia gazeti hili kuwa taasisi yake itaendelea kuchunguza watu wote waliohusika katika kashfa ya escrow bila ya ubaguzi, lakini akabainisha kuwa kazi ya kuwapeleka mahakamani mawaziri na vigogo inatakiwa ifanywe na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).


Dk Hoseah, ambaye aliwahi kuingia kwenye mzozo wa DPP wa zamani kutokana na madai yake kuwa mafaili mengi ya kesi za rushwa hayafanyiwi kazi, alisema sheria haiwaruhusu kuwapeleka mahakamani mawaziri iwapo watabainika kuhusika kwenye vitendo vya rushwa.


Kwa mujibu wa kifungu cha 57 cha Sheria Namba 11 ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Mwaka 2007, endapo vigogo na mawaziri watabainika kuhusishwa na vitendo vya rushwa, jalada la uchunguzi wao litakabidhiwa kwa DPP ili achukue hatua ya kuwapeleka mahakamani.


Dk Hoseah alisema kwa sasa Takukuru inaendelea na uchunguzi wake mpaka itakapojihakikishia ushahidi wa kutosha dhidi ya vigogo hao.


“Bunge lilitoa maazimio yake na likaagiza kuchukuliwa hatua…Takukuru tulishaanza na tunaendelea na uchunguzi. Taratibu zote zikishakamilika kisha ushahidi ukapatikana kwa vielelezo vyote, basi watafikishwa mahakamani wala hakuna tatizo lolote,” alisema.


“Lakini watafikishwa mahakamani baada ya sisi kuwasilisha jalada letu la uchunguzi kwa DPP ambaye ndiye mamlaka ya kuwafikisha mahakamani kama sheria inavyotuagiza.”


Udhaifu huo wa sheria pia ulizungumziwa na Bunge wakati wa kujadili kashfa ya escrow na kuazimia kuwa sheria inayounda Takukuru ifanyiwe kazi ili iwe na mamlaka hayo ya kufikisha mahakamani vigogo wa rushwa kubwa.


Waliohusishwa na rushwa
Mawaziri waliotajwa kwenye sakata hilo ni Profesa Anna Tibaijuka, ambaye alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na ambaye aliingiziwa Sh1.6 bilioni na mwanahisa wa zamani wa Kampuni ya IPTL, James Rugemarila. Tibaijuka alivuliwa wadhifa huo kutokana na sakata hilo.


Wengine ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ambaye Rais Jakaya Kikwete alisema amemuweka kiporo baada ya Bunge kumuona kuwa hakushughulikia vizuri suala hilo na kuisababishia Serikali kukosa mapato.


Wengine ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti na ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu, Andrew Chenge, ambaye aliingiziwa pia Sh1.6 bilioni kwenye akaunti yake na Rugemarila; waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja, aliyeingiziwa Sh40.4 milioni; aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona (Sh40.4 milioni), mbunge wa zamani wa Sumbawanga (CCM), Paul Kimiti (Sh40.4 milioni) na aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Tanesco, Dk Enos Bukuku (Sh161.7 milioni).


Vigogo waliotajwa kwenye sakata hilo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliackim Maswi, ambaye amesimamishwa, Fredrick Werema, ambaye alijiuzulu kwa maelezo kuwa ushauri wake kuhusu suala la kodi kwenye fedha hizo haukueleweka na ulisababisha tafrani.


Awali, Dk Hoseah aliliambia gazeti dada la The Citizen kwamba katika uchunguzi wake, hakuna kiongozi wala kigogo yeyote ambaye atapona.


“Yeyote yule ambaye atabainika katika uchunguzi wetu, lazima afikishwe mbele ya sheria, hakuna kigogo wala kiongozi yeyote ataweza kukwepa endapo ushahidi utaonekana wazi,” alisema.


Alipoulizwa kama uchunguzi huo unamjumuisha Profesa Tibaijuka, mkurugenzi huyo alisema hawezi kutaja jina la mtu kwa kuwa ni kinyume cha sheria kutaja jina au taarifa ambazo ziko kwenye uchunguzi.”


Waliofikishwa mahakama ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu hadi sasa ni Mhandisi Mkuu wa Mradi wa Umeme Vijijini (Rea), Theophillo Bwakea na Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma, ambao kwa pamoja wanadaiwa kupokea rushwa ya Sh485.1 milioni.


Wengine ni Meneja Misamaha ya Kodi wa TRA, Kyabukoba Leonard Mutabingwa, Mwanasheria Mwandamizi wa Tanesco, Steven Roman Urassa na Mkurugenzi wa Fedha BoT, Julius Rutta Angello wanaokabiliwa na mashtaka ya kuomba na kupokea rushwa ya jumla ya Sh1.923 bilioni.


Maoni ya wasomi
Akizungumzia suala hilo, Profesa Gaudence Mpangalla kutoka Chuo Kikuu cha Ruaha alihoji sababu za Serikali kushindwa kuchukua hatua za haraka kuijengea uwezo Takukuru ili iweze kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa aina hiyo.


“Kama tunavyoona hivi sasa inawapandisha kizimbani watumishi wengine, sasa kuna tofauti gani na waziri atakayebainika kukutwa na kosa kama hilo? Sioni tofauti yoyote kwa wakosaji hao,” alisema.


“Udhaifu huo unaweza kujenga imani kwamba Serikali inawabeba mafisadi kwa mgongo wa ofisi ya DPP kwa sababu mashtaka mengi hayafanyiwi kazi katika ofisi hiyo.”


Mara kadhaa Dk Hoseah amekuwa akitoa kauli zinazoonyesha kuwa ameshawasilisha majalada mengi ofisi ya DPP, lakini amekuwa akiyakalia au kuyarudisha kutaka uchunguzi ukamilike.


Hata hivyo, Profesa Chris Maina wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anaona hilo halitafanyika kwa hivi sasa.


“Kwa jinsi sakata hilo lilivyoibuliwa na ushahidi kuwekwa wazi na Rais akaonyesha hisia zake, lazima DPP ajaribu kuwa makini sana na mawaziri au vigogo watakaofikishwa mbele yake,” alisema.


“Inamlazimu achukue hatua za haraka. Hili suala siyo sawa na mashtaka mengine… lakini tusubiri kwa sababu ni kiongozi mpya aliyeingia ofisi hiyo hatujui itakuwaje.”MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: