BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WASOMI WAMSIFU RAIS DK JAKAYA KIKWETE KUPANGUA SAFU YA MAWAZIRI.


Mhadhiri wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Ayoub Rioba.

MABADILIKO madogo ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete sanjari na kujiuzulu kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kumeelezwa kuwa kumenusuru Bunge na msuguano usio na tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Watu wa kada tofauti waliozungumza jana, walisema mabadiliko hayo na kuondoka kwa Muhongo, kumesaidia kufilisi hoja za baadhi ya wabunge, ambao wangeendelea kutumia sakata la ufisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow ya iliyokuwa Benki Kuu (BoT), kujijenga binafsi kisiasa.

Wasomi walisema hatua hiyo itaondoa msuguano wa muda mrefu, ulikuwapo ndani ya Bunge na hata kwenye jamii kwa ujumla.

Miongoni mwa waliozungumza na gazeti hili ni Mhadhiri wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Ayoub Rioba, aliyesema mabadiliko hayo yataondoa msuguano miongoni mwa wabunge, kwani wangeweza kukasirishwa kama kusingekuwa na mabadiliko.

Rioba alisema mabadiliko hayo madogo, ilikuwa lazima yatokee, kutokana na Serikali kuwa na wajibu wa kutekeleza mapendekezo ya Bunge juu ya sakata hilo la akaunti ya Escrow.

Mkuu wa Kitivo cha Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana, alisema kutokana na hatua hiyo ya kuwaondoa baadhi ya mawaziri waliohusishwa na sakata hilo, Rais Kikwete ametumia fursa nzuri katika utekelezaji wa maazimio ya Bunge.

Katika maazimio manane ya Bunge, mojawapo lilikuwa ni kuwawajibisha Waziri wa Nishati na Madini, Muhongo, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye alisema Watanzania wengi waliyategemea mabadiliko hayo, kutokana na sakata hilo lilivyotikisa Bunge.

Baadhi ya watu waliopiga simu kwenye chumba cha habari, ingawa walikosoa hatua ya Muhongo kuchelewa kujiuzulu, walisema kuondoka kwake kutafanya mkutano huo wa Bunge unaoanza kesho, kujadili mambo muhimu yanayogusa wananchi moja kwa moja.

“Napongeza hatua zilizochukuliwa, ingawa Muhongo alichelewa kujiuzulu, lakini sasa kuondoka kwake tunaamini tutapumua na suala hili la Escrow. Hata bungeni sasa wabunge wetu watajadili mambo muhimu yanayotugusa moja kwa moja badala ya wanasiasa kuchuana wenyewe kwa wenyewe kutafuta umaarufu,” alisema mkazi wa Mwanza, Joseph Kalisa.

Waliofilisiwa hoja.
Kile kilichoonekana kwamba suala la Escrow lingeendelea kuwasha moto katika mkutano wa Bunge unaoanza kesho, ni kauli zilizokuwa zimeanza kutolewa hivi karibuni na baadhi ya wabunge wa upinzani.

Kauli hizo zilionesha kwamba suala hilo lingeendelea kuwa mtaji wao wa kisiasa. Miongoni mwa wabunge hao ni Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema aliyedai angemtoa kwa mabavu bungeni Muhongo katika kikao kijacho cha Bunge, endapo angekuwa hajaondolewa kwenye nafasi hiyo.

Mkakati huo wa Lema uliungwa mkono na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) ambaye pia alikaririwa akisema amepanga kumtoa bungeni kwa nguvu, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge anayehusishwa pia na sakata hilo.

Muhongo kujiuzulu

Akizungumzia ya Muhongo kujiuzulu, Dk Rioba alisema ni hatua ya kiungwana ingawa alichelewa kuchukua uamuzi huo, hivyo kuruhusu mashambulizi dhidi yake yasiyo na sababu.

“Muhongo ni msomi na kwa hadhi yake ametoa mchango mkubwa kwa nchi kabla ya kuwa waziri na wakati akiwa waziri. Lakini tangu suala hili litokee alitakiwa kuchukua uamuzi huu mapema, kwani kuchelewa kwake kumekaribisha ‘mawe’ bila sababu na angewahi ingesaidia sana,” alisema Rioba.

Wakati watu mbalimbali wakiamini kwamba kujiuzulu kwake kutaleta tija kwenye Bunge linaloanza kesho, pia kwa upande wake, Muhongo, miongoni mwa sababu alizotoa wakati akijiuzulu ni kwamba yeye ni suluhisho la mjadala wa sakata hilo la Escrow.

Alisema aliona achukue uamuzi huo, serikali ipate nafasi ya kushughulika na matatizo ya Watanzania, badala ya kutumia muda mrefu katika mjadala huo.

Alisema uamuzi wake, utatoa nafasi kwa CCM kuendelea kutafuta suluhisho la kero za Watanzania, badala ya kutumia vikao kujadili suala hilo.

Meneja Mkuu wa Kampuni ya Madini ya Stamigold, Denis Sebugwao, alimshukuru Muhongo kwa kuunga mkono na kuwezesha uundaji wa kampuni hiyo ya kwanza ya serikali ya kumiliki madini.

Hata hivyo, alisema wanawakaribisha mawaziri wapya, akiamini watamsaidia Rais kukidhi matarajio yake ya kuhudumia umma.

Mwakyembe ashitua wengi.
Katika mabadiliko ya mawaziri aliyofanya Rais Kikwete, kuhamishwa kwa Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe kwenda Wizara ya Afrika Mashariki, kumeonesha kugusa wengi, kutokana na wengi kuhoji kupitia majukwaa mbalimbali, ikiwemo mitandao ya kijamii.

Mkuu wa Kitivo cha Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Bana alisema alitarajia Mwakyembe angeendelea kubaki katika wizara hiyo ya uchukuzi, kutokana na mipango na mikakati mingi aliyokuwa akiifanya katika kuendeleza sekta ya uchukuzi nchini.

“Katika hili, Rais angeangalia kwa jicho pana zaidi kwa sababu tayari Mwakyembe alionesha kufanya vizuri katika kutatua matatizo ya reli, kama vile Tazara na Bandari, ambayo hata hivyo pamoja na jitihada zake bado yana matatizo,” alisema Dk Bana.

Hata hivyo, alipongeza hatua ya Rais kuamua kumweka Samuel Sitta (aliyekuwa Wizara ya Afrika Mashariki) katika sekta hiyo ya uchukuzi na kusisitiza kwamba anaamini kutokana na uzoefu wa muda mrefu serikalini alionao, atafanya vizuri zaidi katika uchukuzi.

Dk Bana alisema kwa kuwa Mwakyembe ana uzoefu mzuri katika masuala ya kimataifa, anatarajia kufanya vizuri katika wizara hiyo ya Afrika Mashariki.

Lakini, alidai ana wasiwasi juu ya utendaji wenye tija wa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anne Kilango Malecela.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Simbeye alisema anasikitishwa na kitendo cha Mwakyembe kuhamishwa Wizara ya Uchukuzi kwa kile alichosema, tayari alikuwa anafanya vizuri katika kusimamia maboresho ya reli na bandari.

“Lakini napenda kusisitiza kuwa Sekta binafsi tunaahidi kutoa ushirikiano kwa mawazri wote wapya,” alisema.

Simbeye alisema taasisi hiyo imepokea kwa furaha uteuzi wa George Simbachawene kuwa Waziri wa Nishati na Madini, kwa kuwa ana uzoefu mkubwa katika masuala ya nishati na madini.

Aidha alisema taasisi hiyo inatarajia waziri huyo atasimamia kupitia Baraza la Mawaziri, kupitishwa kwa Sera ya gesi yenye kipengele cha nafasi ya wazawa kuweza kushiriki katika miradi ya gesi na mafuta nchini.

Walioteuliwa
Katika mabadiliko hayo yaliyotangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, Rais Kikwete aliteua naibu mawaziri wawili wapya na kupandisha cheo wawili huku mawaziri wengine sita walibadilishwa nafasi zao, hatua iliyochukuliwa pia kwa naibu mawaziri watatu.

Mawaziri Kamili:
George Simbachawene - Waziri wa Nishati na Madini

Mary Nagu - Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu)
Dk Harrison Mwakyembe - Waziri wa Afrika Mashariki
Wiliam Lukuvi - Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi
Steven Wassira - Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika
Samwel Sitta - Waziri wa Uchukuzi

Jenista Mhagama - Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu( Sera na Uratibu wa Bunge) Christopher Chiza - Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji)

Manaibu Waziri:
Steven Masele - Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano, Angellah Kairuki - Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi Ummy Mwalimu- Naibu Waziri wa Katiba na Sheria
Anna Kilango Malecela- Naibu waziri wa Elimu
Charles Mwijage - Naibu Waziri wa Nishati na Madini

Akaunti ya Tegeta Escrow ilifunguliwa BoT mwaka 2006 kwa ajili ya kuhifadhi fedha za malipo ya tozo ya uwekezaji (capacity charges) zilizokuwa zinalipwa na TANESCO kabla hazijakabidhiwa kwa anayelipwa, ambaye ni kampuni binafsi ya kufua umeme ya IPTL.

Kabla ya hapo TANESCO ilikuwa inalipa moja kwa moja kwa IPTL, lakini baadaye Tanesco ililalamikia kiwango chake.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: