BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

HII NDIYO ORODHA KAMILI YA MAJINA YA WAKUU WA WILAYA WAPYA, ZAMANI WALIOTOSWA KATIKA PANGA PANGUA YA RAIS DK KIKWETE 2015.

Paul Makonda.

Dodoma.
Rais Jakaya Kikwete ametengua uteuzi wa wakuu wa wilaya 12 na kuwateua wengine 27, akiwamo aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Zelothe Stephen na mjumbe wa Bunge la Katiba, Paul Makonda ambaye aliingia kwenye mzozo na mawaziri wakuu wawili wa zamani.



Katika uteuzi huo uliotangazwa jana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda mjini hapa, katibu mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka (TFF), Frederick Mwakalebela ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, huku wakuu wa wilaya 64 wakibadilishiwa vituo vyao vya kazi.


“Mabadiliko haya yamezingatia kuwapo nafasi 27 wazi zinazotokana na kufariki dunia kwa wakuu watatu wa wilaya, watano kupandishwa vyeo kuwa wakuu wa mikoa, saba kupangiwa majukumu mengine na 12 kutenguliwa uteuzi wao. Wakuu wa wilaya 42 wamebaki katika vituo vyao,” alisema Pinda wakati akitangaza uteuzi huo.


Pinda alitangaza uteuzi huo jana alasiri na baadhi ya wakuu wa wilaya ambao walibadilishiwa vituo walishangazwa na taarifa za uhamisho huo, ambao umeelezewa na viongozi wa vyama vya upinzani kuwa ni wa kufuja fedha za walipa kodi na unalenga kukiandaa chama hicho kwa Kura ya Maoni na Uchaguzi Mkuu ujao.


“Yaani unanipongeza kwa nini?... mimi nimehamishwa? Nimehamishiwa wapi?” alihoji mmoja wa wakuu wa wilaya baada ya kupigiwa simu na Mwananchi, lakini akaomba asitajwe gazetini.


Katika uteuzi huo yumo Zelotte, ambaye ni kati ya maofisa wachache wa Jeshi la Polisi kuteuliwa kushika nafasi za ukuu wa wilaya na hivyo atalazimika kuacha kibarua cha fani yake na kwenda Musoma. Zelotte anasifika kwa kufanikiwa kukamata vijana 11 waliokuwa wakihusishwa na mazoezi ya kigaidi mkoani Mtwra mwaka 2013.


Pia yumo Makonda, ambaye ameteuliwa kuwa mkuu mpya wa Wilaya ya Kinondoni. Kiongozi huyo wa Umoja wa Vijana wa CCM aliandikwa sana na vyombo vya habari wakati wa Bunge la Katiba kutokana na kutoa maneno ya kumshambulia mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba aliyewasilisha Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba.


Kiongozi huyo wa UVCCM aliandikwa zaidi na vyombo vya habari kutokana na kuhusishwa na vurugu zilizotokea Hoteli ya Blue Pearl jijini Dar es Salaam wakati wa mdahalo wa Katiba Inayopendekezwa akidaiwa kumshambulia mwilini Warioba, ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.


Mwishoni mwa wiki iliyopita, makada wawili wa CCM, John Guninita na Mgana Msindai walimwandikia kusudio la kumfungulia mashtaka wakidai kuwa Makonda aliwadhalilisha kwa kuwaita kuwa vibara wa Edward Lowassa, ambaye ni mbunge wa Monduli na aliwahi kuwa Waziri Mkuu.


Makonda aliwahi kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kumtuhumu Lowassa akidai kuwa anawatuma baadhi ya makada wa chama hicho wanaokivuruga chama. Alidai kuwa Lowassa hawezi kuwa Rais wa Tanzania na kwamba CCM haitafuti Rais pekee, bali mwenyekiti wake na mbunge huyo wa Monduli hawezi kuongoza chama hicho kikongwe.


Waliotenguliwa
Ma-DC waliotenguliwa ni pamoja na Martha Umbulla aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Kiteto, ambayo imekithiri kwa migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji. Mgogoro huo umesababisha watu zaidi ya 10 kuuawa na wengine kujeruhiwa.


Wengine ni Fatma Kimario (Kisarawe) ambaye alihamishiwa wilaya hiyo akitokea Igunga, baada ya kile kilichodaiwa kuwa ni kudhalilishwa na makada wa Chadema katika kampeni za uchaguzi mdogo.


Wengine ambao uteuzi wao umetenguliwa ni James Kisota Ole Millya aliyekuwa Wilaya ya Longido, Elias Wawa Lali (Ngorongoro), Alfred Ernest Msovella (Kongwa) na Danny Makanga (Kasulu).


Pinda aliwataja wengine kuwa ni Elibariki Kingu (Igunga), Dk Leticia Warioba (Iringa), Evarist Kalalu (Mufindi), Abihudi Saideya (Momba), Khalid Mandia (Babati) na Elias Goroi (Rorya).


Hata hivyo, Pinda alisema kutenguliwa uteuzi wa wakuu hao kunatokana na sababu za umri, kiafya na nyinginezo.


Wapya
Mbali na Makonda, Pinda aliwataja ma-DC wengine wapya kuwa ni


Mwakalebela, anayekwenda Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Iringa, akiwa amesogezwa karibu na Jimbo la Iringa Mjini alilogombea ubunge mwaka 2010, na ambaye anadaiwa kulinyemelea tena mwaka huu.


Akizungumzia uteuzi huo, Mwakalebela aliishukuru Serikali kwa kumuona kwamba bado ana mchango wa kuisaidia nchi yake na yuko tayari kuwatumikia wananchi.


Mwakalebela alisema anataka kwanza kufika wilaya hiyo na kujua changamoto kubwa zinazowakabili wananchi na baada ya hapo anataka kuanza kuzitatua moja baada ya ngingine.


“Naijua hii wilaya lakini kwanza nataka kufika huko kujua ni changamoto gani ambazo zinaikabili,” alisema Mwakalebela ambaye alieleza kuwa hatazipa nafasi harakati zake za ubunge kwa sasa.


“Nitaanza kuangalia tunawezaje kuzipatia ufumbuzi... kikubwa nawaomba wananchi wangu kunipa ushirikiano.”


Wengine wapya, kwa mujibu wa Pinda, ni mtangazaji wa TBC, Shaaban Kissu (Kondoa), makamu mwenyekiti wa UVCCM, Mboni Mhita (Mufindi), Mariam Mtima (Ruhangwa), Dk Jasmine Tiisike (Mpwapwa) na Pololeti Mgema (Nachingwea).


Wengine ni Fadhili Nkurlu (Misenyi), Felix Lyaniva (Rorya), Zainab Mbussi (Rungwe), Francis Mwonga (Bahi), Kanali Kimiang’ombe Nzoka, (Kiteto) na Husna Msangi (Handeni).


Wapya wengine ni Emmanuel Uhaula (Tandahimba), Hashim Mngandilwa (Ngorongoro), Mariam Juma (Lushoto), Thea Ntara (Kyela), Ahmed Nammohe (Mbozi), Pili Moshi (Kwimba) na Mahmoud Kambona (Simanjiro).


Pinda, pia, aliwataja wengine wapya kuwa ni Zainab Telack anayekwenda Sengerema, Bernard Nduta (Masasi), Zuhura Ally (Uyui), Mwajuma Nyiruka (Misungwi) na Muftah Mohamed (Sengerema).


Waliopangiwa majukumu mengine
Kwa mujibu wa Pinda, waliopangiwa majukumu mengine ambao ni Brigedia Jenerali Cosmas Kayombo, aliyekuwa Simanjiro, Kanali Ngemela Lubinga (Mlele), Juma Madaha (Ludewa) na Mercy Silla (Mkuranga).


Wengine ni Ahmed Kipozi (Bagamoyo), Mrisho Gambo (Korogwe) na Elinas Pallangyo (Rombo).


Waliobadilishwa vituo
Wakuu wa wilaya 64 waliobadilishwa vituo vya kazi ili kuboresha utendaji wa kazi ni Nyerembe Munasa, anayetoka Arumeru kwenda Mbeya), Jordan Rugimbana (Kinondoni-Morogoro) na Lephy Gembe (Dodoma Mjini-Kilombero).


Wengine ni Christopher Kangoye (Mpwapwa-Arusha), Omar Shaban Kwaang’ (Kondoa-Karatu), Fransic Mtinga (Chemba-Muleba), Elizabeth Mkwasa (Bahi-Dodoma), Agnes Hokororo (Ruangwa-Namtumbo), Regina Chonjo (Nachingwea-Pangani) na Husna Mwilima (Mbogwe-Arumeru).


Wengine ni Gerald Guninita (Kilolo-Kasulu), Zipporah Pangani (Bukoba-Igunga), Kanali Issa Njiku (Missenyi-Milele), Richard Mbeho (Boharamulo-Momba), Lembris Kipuyo (Muleba- Rombo) na Ramadhan Maneno (Kigoma-Chemba).


Venance Mwamoto (Kibondo-Kaliua), Gishuli Charles (Buhigwe-Ikungi), Novatus Makunga (Hai-Moshi), Anatory Choya (Mbulu-Ludewa), Christine Mndeme (Hanang’- Ulanga), Jacksone Msome (Musoma-Bukoba), John Henjewele (Tarime-Kilosa) na Dk Norman Sigalla (Mbeya-Songea).


Pia wamo Dk Michael Kadeghe (Mbozi-Mbulu), Crispin Meela (Rungwe-Babati), Magreth Malenga (Kyela-Nyasa), Said Amanzi (Morogoro-Singida), Antony Mataka (Mvomero-Hai), Elias Tarimo (Kilosa-Biharamulo) na Francis Miti (Ulanga-Hanang’).


Wengine ni Hassan Masala (Kilombero-Kibondo), Angelina Mabula (Butiama-Iringa), Farida Mgomi (Masasi-Chamwino), Wilman Ndile


(Mtwara-Kalambo), Ponsian Nyami (Tandahimba-Bariadi), Mariam Lugaila (Misungwi-Mbogwe) na Mary Tesha Onesmo (Ukerewe-Buhigwe).


Pia Karen Yunus anatoka Sengerema kwenda Magu), Josephine Matiro (Makete-Shinyanga), Joseph Mkirikiti (Songea-Ukerewe), Abdula Lutavi (Namtumbo-Tanga), Ernest Kahindi (Nyasa-Longido), Anna Nyamubi (Shinyanga-Butiama), Rosemary Kirigini (Meatu-Maswa) na Abdallah Kihato (Maswa-Mkuranga).


Erasto Sima (Bariadi-Meatu), Queen Mulozi (Singida-Urambo), Yahaya Nawanda (Iramba- Lindi), Manju Msambya (Ikungi-Ilemela), Saveli Maketta (Kaliua-Kigoma), Bituni Msangi (Nzega-Kongwa), Lucy Mayenga (Uyui-Iramba), Majid Mwanga (Lushoto-Bagamoyo) na Muhingo Rwehemamu (Handeni-Makete).


Pia Hafsa Mtasiwa anatoka Pangani kwenda Korogwe, Dk Nassoro Hamid (Lindi-Mafia), Festo Kiswaga (Nanyumbu-Mvomero), Sauda Mtondoo (Mafia Nanyumbu), Suleman Mzee (Kwimba-Kilolo), Esterina Kilasi (Wanging’ombe-Muheza), Subira Mgalu (Muheza-Kisarawe) na Jacqueline Liana, anayetoka Magu kwenda Nzega.


Wanasiasa wakosoa
Wakizungumzia uteuzi huo, wenyeviti wa Chadema na CUF, Freeman Mbowe na Profesa Ibrahim Lipumba walisema hawaoni umuhimu wa wakuu wa wilaya nchini na kuwa uteuzi huo unalenga kuandaa timu ya uchakachuaji wakati wa Uchaguzi Mkuu na Kura ya Maoni ili kupitisha Katiba Inayopendekezwa.


“Hayo ni maandalizi ya CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu. Chadema tulishaeleza kuwa wakuu wa wilaya hawana umuhimu wowote katika Taifa hili na wanaongeza gharama tu za Serikali,” alisema Mbowe.


Alieleza kuwa uteuzi wao hauzingatii uzoefu, sifa wala weledi na kwa kuthibitisha hilo, wanapoteuliwa hakuna sehemu inayoeleza wameteuliwa kwa kigezo kipi.


“Haya ndiyo matatizo ya rais wa nchi kuwa na mamlaka makubwa ya kikatiba ya kuteua kadri atakavyo. Nchi haiwezi kupata maendeleo kwa kuwa na mambo ya namna hii. Uteuzi huu ni kama kupeana zawadi tu,” alisema.


Naye Profesa Lipumba alisema: “Ukitazama utaona kuwa waliochaguliwa ni makada wa CCM walioandaliwa kuchakachua Kura ya Maoni na Uchaguzi Mkuu. Rais Kikwete anakwenda kumaliza muda wake. Sasa wakuu wapya wa wilaya au mabadiliko ya kazi gani.


“Watakwenda kufanya kazi gani mpya ambayo wengine wameishindwa, watasimamia jambo gani muhimu lililowekwa na Serikali?”


Alisema mamlaka ya rais katika uteuzi madhara yake ndiyo kama hayo kwa kuwa anaweka watu ambao watatekeleza matakwa yake.


“Kikubwa ninachokiona juu ya uteuzi huu ni wahusika kwenda kusimamia mchakato wa kupitisha wagombea wa CCM katika Uchaguzi Mkuu, zaidi ya hapo hakuna jipya lolote watakalolifanya,” alisema Lipumba.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: