BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WAKULIMA, WAFUGAJI NAMNA WANAVYOPIGA KWA KUTUMIA MAPANGA, MIKUKI, SIME KISA ARDHI VIJIJI VYA MBIGILI NA MABWEGERE WILAYA YA KILOSA.

Polisi wakishusha mwili wa marehemu mmoja na watu watatu waliofariki dunia katika mapigano ya wakulima na wafugaji wilayani Kilosa, Morogoro juzi. Picha na Juma Mtanda
Na Juma Mtanda, Mwananchi.


Mauaji yanayotokana na migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji mkoani Morogoro, yanazidi kutikisa baada ya watu wengine watatu kuuawa kwenye Kijiji cha Mbiligi, Kata ya Magole wilayani Kilosa.


Tukio hilo, ambalo limetokea mwezi mmoja tu baada ya mkulima mmoja kuuawa kwenye Bonde la Mgongola wilayani humo, ni kati ya matukio mengi ya mapigano baina ya jamii hizo mbili na ambayo yalijadiliwa kwa kina kwenye mkutano uliopita wa Bunge la Muungano.


Habari kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa, juzi saa 2.00 asubuhi wakulima wapatao 15 walikwenda eneo la Matembele na Ming’oni, jirani na Kijiji cha Mbigili ili kupanda mpunga, lakini saa nne baadaye vijana wawili wa Kimasai walifika na kuhoji sababu za kutumia eneo hilo kwa kilimo wakati ni mali ya Kijiji cha Mabwegela na kuwaamuru waondoke.


Lakini wakulima hao walikaidi na ndipo muda mfupi baadaye likaibuka kundi la wafugaji wapatao 50 na kurejea swali hilo.


Habari hizo zilisema kuwa, baada ya wakulima kuona wamevamiwa, walianza kuwarushia Wamasai mapande ya udongo na walipozidiwa ndipo waliporudi nyuma, lakini ghafla wakajikuta wamezingirwa.


Kwa mujibu wa habari hizo, wakulima waliamua kutoroka, ndipo baadhi yao waliposhambuliwa kwa mikuki, virungu, mishale na visu na kusababisha vifo vya watu hao watatu.


Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Elias Tarimo alisema watu wengine kadhaa walijeruhiwa na wamelazwa katika Kituo cha Afya cha St Joseph cha Dumila, Kilosa.


Alisema waliouawa ni Joseph Lawama, ambaye ni mkulima wa Mbigili (26), Rajabu Kigongo, mkulima wa Mbigili ambaye alichomwa mshale mgongoni na kuchanwa na shingoni na Kandura Kashu (30) mfugaji wa Mabwegere.


Alisema mtu mmoja alifariki dunia katika maeneo ya tukio na wengine wawili wakati wakitibiwa katika kituo cha afya. Pia aliwataja majeruhi kuwa ni Binzi Dotto (42), Juma Someke (35) na Mohamed Selemani (36).


“Mgogoro huu unatunyima usingizi viongozi katika jitihada zetu za kuutatua na kuepusha umwagaji damu. Tumekuwa tukijitahidi kuitisha vikao vya upatanishi kati ya vijiji vya Mbiligili na Mabwegere, lakini hakujawa na mafanikio,” alisema Tarimo.


Alisema tatizo hilo linatokana na baadhi ya viongozi wa Kijiji cha Mabwegere kukataa kuhudhuria vikao vya upatanishi.


Muuguzi wa zamu katika Kituo cha Afya cha St Joseph, Melania Shayo alisema walianza kuwapokea majeruhi saa 10.30 jioni na kwamba wakati wakiwahudumia, wawili walifariki dunia.


Shayo alisema watu hao ni Joseph Lawaza na Rajabu Kigongo ambaye alipoteza maisha saa 4.28 usiku wakati akifanyiwa mpango wa kusafirishwa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu zaidi.


“Awali tuliwapokea majeruhi saba na maiti moja, lakini baadaye vifo viliongezeka baada ya majeruhi wawili kufariki dunia hapahapa hospitalini wakati wakipatiwa huduma,” alisema Shayo.


Shayo alisema vurugu nusura zitokee kwenye kituo hicho baada ya wananchi kupata taarifa kuwa kulikuwa na mtu mmoja kutoka jamii ya Wamasai aliyefikishwa akiwa majeruhi na hivyo kutaka kuvamia ili wammalizie, lakini polisi walidhibiti hali hiyo.


Mmoja wa majeruhi, Mohammed Athuman alisema vurugu kati yao na wafugaji zilianza saa 6.00 mchana wakati wakipanda mpunga shambani.


Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Mussa Marambo alisema hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: