BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

HUZUNI, SIMANZI, VILIO NA MAJONZINi MAZISHI YA WANAFAMILIA SITA WALIOFARIKI KWA KUUNGUA MOTO DAR ES SALAAM.


Majeneza yaliyobeba miili ya watu sita wa familia moja waliofariki dunia baada ya nyumba yao kuungua moto eneo la Kipunguni A, jijini Dar es Salaam jumamosi usiku. Picha na Salim Shao.


Dar es Salaam.
Huzuni, simanzi na majonzi jana vilitawala maeneo ya Kipunguni A na baadaye kwenye Makaburi ya Airwing Ukonga, Ilala wakati miili ya watu sita waliofariki dunia kwa kuungua moto Jumamosi alfajiri ilipozikwa.


Shughuli zilisimama kwa muda katika maeneo hayo kati ya saa saba na nane mchana wakati msafara mkubwa wa waombolezaji ulipokuwa ukielekea makaburini.


Wananchi wengi waliokuwapo katika maeneo ambayo msafara huo ulipita, waliacha kwa muda shughuli zao na kujongea pembeni mwa barabara kushuhudia umati wa watu waliokuwa katika magari, pikipiki, baiskeli na wengine wakitembea kwa miguu wakielekea makaburini katika mazishi ya watu sita; Kapteni mstaafu, David Mpilla, mkewe Celina, mtoto wao Lucas, Shemeji wa Mpilla, Samwel Yegeya na wajukuu wa Mpilla Paulina na Celina Emmanuel.


Katika tukio hilo la Jumamosi, ni mtu mmoja pekee, Emmanuel Mpilla wa familia hiyo alinusurika kwani wakati moto huo ulipoteketeza nyumba yao hakuwapo.


Waombolezaji walianza kuwasili Kipunguni A kuanzia saa tatu asubuhi. Ilipotimu saa tano asubuhi, idadi yao iliongezeka kiasi cha wengine kukosa mahali pa kukaa na kuwafanya waratibu wa mazishi hayo kuwataka waanze kuelekea eneo la makaburi.


Miili ya marehemu iliondolewa nyumbani saa 7.20 mchana kwa gari la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Wakati inapakiwa kwenye gari hilo, vilio na simanzi vilitawala huku baadhi ya waombolezaji, wengi wao wakiwa kina mama, waligaragara na kulia kwa uchungu.


Hali ilivyokuwa
Kutokana na umati wa waombolezaji, ilipotimu saa 9.20 alasiri, askari wa JWTZ, walifunga barabara inayoelekea eneo la makaburi.


Baada ya miili hiyo kufikishwa makaburini, askari wa JWTZ waliipanga kwenye meza maalumu zilizokuwa zimepambwa kwa maua na picha za marehemu hao zikiwa mbele ya majeneza yao tayari kuanza kwa ibada ya mazishi iliyoongozwa na Askofu Msaidizi Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigirwa.


Askofu Nzigirwa, aliwaongoza waombolezaji akiwamo Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal kuaga miili hiyo ambayo, tofauti na ilivyo kawaida kwa waumini wa Dini ya Kikristo, majeneza yao hayakufunguliwa kutokana na miili ya marehemu kuharibika.


Katika tukio hilo la kuaga, baadhi ya waombolezaji walipoteza fahamu kutokana na uchungu hasa walipopita mbele ya majeneza yaliyokuwa na picha ya watoto Celina na Paulina wakiwa wamekumbatiana huku wakitabasamu enzi za uhali wao.


Miongoni mwa waliopoteza fahamu ni mama wa watoto hao, Mwajuma Issa.


Kiungo chapelekwa makaburini
Katika tukio lisilo la kawaida, moja ya kiungo kinachoaminika kuwa cha Kapteni Mpilla kilikutwa katika chumba chake, kiliwekwa kwenye jeneza lake ambalo tayari lilikuwa limeshaingizwa kaburini. Awali, kiungo hicho hakikuwa kimegundulika wakati miili ya marehemu hao ilipokuwa ikikusanywa.


Wakusanya viongozi
Mazishi ya marehemu hao ambao ni ndugu wa karibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya waliozikwa kuanzia saa 10.30 jioni yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa.


Mbali na Dk Bilal, viongozi wengine waliohudhuria ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe, Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani, Mkuu wa Wilaya Ilala, Raymond Mushi, Mbunge wa Ukonga, Eugene Mwaiposa, Mwenyekiti wa CCM Mkoa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida na Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema, Mabere Marando.


Akizungumza katika mazishi hayo, Dk Bilal alisema: “Tumesikitishwa na vifo vya watu hawa kwa wakati mmoja. Tunawapa pole wafiwa na tunawaomba wastahimili katika kipindi hiki kigumu,” aliongeza: “Wakati umefika sasa watu kubadili mfumo wa ujenzi wa madirisha ya nondo. Tunafahamu kuwa watu wanajilinda, lakini usalama wetu wengi uko shakani hasa inapotokea dharura.”


Simulizi za majirani
Majirani walileza jinsi walivyojitahidi bila mafanikio kuwaokoa na badala yake wakaishia kusikiliza sauti za vilio vya uchungu wa maumivu makali ya moto kisha vishindo vya kupasuka vichwa.


Mmoja wa majirani hao, Lusajo Mwaipopo alifika katika nyumba ya marehemu baada ya kusikia sauti ya vilio wakiomba msaada.


Alisema alipofika eneo hilo alikuta moto ukiwa tayari umetanda katika sebule ya nyumba hiyo. Anasema walianza kushauriana jinsi ya kutoa msaada hasa namna ya kuuzima moto huo.


“Nilipata wazo la kujaribu kuwashawishi wenzangu kutafuta sururu ili kuvunja. Tukapata mbili, nikachukua moja na kuanza kuvunja kwenye kona ya dirisha nilifanikiwa kutoboa lakini ghafla moto ulizuka kwenye tundu nikaogopa na kutimua mbio,” alisema Mwaipopo.


Alisema hilo ni tukio baya kulishuhudia katika maisha yake na inawaumiza karibu majirani wote walioshuhudia hasa kutokana na vishindo vya kupasuka kwa vichwa.


Wasifu wa baba, mama
Akizungumza katika mazishi hayo, Brigedia Jenerali Honoratus Lyamba alisema marehemu Mpilla alikuwa mtumishi mwaminifu wa JWTZ Kikosi cha Anga hadi alipostaafu 1994.


Mkurugenzi wa Swissport, Gaudence Temu alisema mke wa Kapteni Mpilla, marehemu Celina ambaye alikuwa mtumishi wa kampuni hiyo kabla ya kustaafu mwaka 2007, alikuwa mtumishi mwadilifu.


Vifo vya ghafla
Jirani mwingine, Christina Jabir alieleza kwamba mwaka 1989 familia hiyo ilipatwa na msiba mkubwa wa ghafla baada ya mtoto wao wa kwanza kufariki dunia kwa kugongwa na basi.


“Nakumbuka alikuwa anaitwa Kabuta, aligongwa na kufa papohapo alipokuwa akivuka barabara katika eneo la Banana, akitoka kanisani Ukonga,” alisema.


“Wakati wa msiba ule mama yake alituambia kwamba siku hiyo mwanaye alimlilia asubuhi akitaka waende wote kazini lakini alimbembeleza aende kanisani, huku akishangazwa na hali hiyo maana hakuwahi kumlilia (kutaka waende wote kazini),” alisema Jabir.


Mzazi atoa ya moyoni
Mama mzazi wa marehemu Kapteni Mpilla, Felister Lonjini Masanja alisema sasa amebakiwa na mtoto mmoja baada ya wengine wanne kufariki dunia. Mama huyo aliyekuwa na watoto wote wa kiume, alisema sasa amebakiwa na mtoto wake mkubwa.


Alisema kifo cha moto ni kibaya kwa sababu humkuta mtu huku akifahamu kuwa kifo chake kinakuja.


Alisema anamhurumia mjukuu wake, Emmanuel ambaye amebaki peke yake katika familia ya baba yake.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: