MWANDISHI WA RAIS JAKAYA KIKWETE HUKUTUTENDEA HAKI WANAHABARI.
RAIS JAKAYA KIKWETE.
Tafsiri ya jumla ya neno vyombo vya habari kwa mujibu wa kamusi mbalimbali, ni mfumo wa mawasiliano unaojumuisha utangazaji wa redio, televisheni, uandishi wa magazeti, majarida au vitabu.
Sekta ya habari ni chanzo muhimu cha upashaji na usambazaji wa habari katika jamii. Kwa maneno mengine, jamii haina cha kujivunia katika habari bila kuwapo kwa sekta hii.
Kutoa na kupokea habari ni haki ya msingi ndani ya jamii, ndiyo maana, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika wana matamko yanayoelekeza serikali kutoa uhuru wa kupokea na kutoa habari.
Vyombo hivi vina wajibu mkubwa kwa ustawi wa jamii na mahitaji yake muhimu, kama upashanaji na utoaji wa habari. Lakini ikumbukwe pia, vyombo hivi havifungwi na mambo hayo mawili tu, yaani kutoa na kusambaza habari.
Kila mwaka waandishi wa habari na wanaharakati mbalimbali tumekuwa tukiadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari ifikapo Mei 3, lakini uhuru huo umo hatarini katika sehemu kadhaa za dunia.
Ikumbukwe kuwa uhuru huo unaenda sambamba na uhuru anaopaswa kuwa nao mwandishi wa habari katika kupata habari au taarifa, kuulizwa au kuuliza maswali.
Moja kati ya vikwazo tunavyokumbana navyo, kimoja ni hiki kilichotupata Ikulu jijini Dar es Salaam Februari 3 mwaka huu, wakati Rais Jakaya Kikwete alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya mazungumzo ya faragha na mgeni wake, Rais wa Ujerumani, Joachim Gauck, aliyekuja nchini kwa ziara ya siku tano.
Jambo lililotusikitisha wanahabari takriban 20 tuliokuwapo katika mkutano huo, ni kitendo cha Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu kutuchagulia maswali ya kuwauliza marais hawa wawili.
Kabla ya marais hao kufika ukumbini, Rweyemamu aliwaita waandishi wa gazeti la Mwananchi, Daily News na Guardian na kuwataka kuuliza maswali aliyoyachagua yeye. Alisisitiza kuwa wasiulize maswali wanayoyajua wao kwani atawaumbua.
Mwandishi wa Mwananchi alitaka kumuuliza swali Rais Gauck juu ya uwekezaji wa China barani Afrika kupondwa, lakini nchi hiyo bila kuchoka imeendelea kuwekeza. Alitaka kujua kama Ujerumani iko tayari kuwekeza Afrika na Tanzania kama ilivyo kwa China.
Rweyemamu alilipinga swali hilo na kukata kabisa jina la mwandishi huyo kati ya watu waliotakiwa kuuliza maswali siku hiyo.
Tena alichukua hatua hiyo baada ya mwandishi huyo kukataa kuuliza swali la kupewa ambalo lilimtaka amuulize Rais Kikwete alijifunza nini katika mkutano aliohudhuria hivi karibuni nchini Ujerumani kuhusu chanjo.
Mwandishi wa Daily News alipewa nafasi ya kuuliza swali kuhusu uhusiano kati ya Tanzania na Ujerumani, bahati mbaya swali hilo lilikuwa limeshatolewa majibu na marais hao wawili.
Baada ya kupewa nafasi, mwandishi huyo aliuliza swali ambalo halikuwapo katika orodha ya maswali ya Rweyemamu na hapo ndipo hali ya hewa ilipoanza kuchafuka.
Swali hili lilihusu mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi, huku mwandishi huyo akitaka kusikia kauli ya rais huyo wa Ujerumani juu ya suala hilo ikikumbukwa kuwa historia ya mipaka ya nchi za Afrika iliwekwa miaka mingi na wakoloni, wakiwamo Wajerumani.
Uzito wa swali hilo ulimfanya Rais Gauck kutamka wazi kuwa hawezi kujibu lakini Rais Kikwete alilijibu kifupi.
Alichokifaya Rweyemamu, ambaye ni mwandishi wa habari aliyebobea, ni kinyume na taaluma ya uandishi wa habari. Sidhani kama Rais Kikwete anaweza kuwaita waandishi wa habari Ikulu na kuwapangia maswali ya kumuuliza.
Mpaka marais wanafikia hatua ya kuitisha mkutano na waandishi wa habari ni wazi kuwa wanakuwa wamejipanga kujibu maswali ya aina yoyote ile.
Jambo la kusikitisha zaidi waandishi wa habari walioambatana na rais huyo wa Ujerumani hawakupangiwa maswali ya kuuliza.
Nikiri wazi kuwa maswali waliyoyauliza ndiyo yaliyozaa habari nzuri zilizotawala katika vyombo vya habari (hasa magazeti) siku iliyofuata.
Mmoja wa waandishi hao kutoka Ujerumani, alitaka kauli ya Rais Kikwete na Rais Gauck, juu ya msingi wa uhuru wa vyombo vya habari na haki za binadamu nchini, akihusisha suala hilo na tukio la hivi karibuni la kufungiwa kwa gazeti la The East African na wanachama wa CUF kupigwa na polisi walipotaka kuandamana.
Maswali hayo pia yangeweza kuulizwa na waandishi wa Tanzania lakini walizuiwa.
Hata swali la mwisho lililokuwa liulizwe na mwanahabari kutoka gazeti la Guardian halikuulizwa, huku Rweyemamu akidai kuwa muda wa maswali ulikuwa umekwisha.
Fidelis Butahe ni mwandishi wa Mwananchi. 0714 787289.
0 comments:
Post a Comment