KLABU YA YANGA SC YAMSONONESHA MRISHO NGASSA.
Mchezaji wa Yanga Mrisho Ngassa (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano iliofanyika jana.
Winga wa Yanga, Mrisho Ngassa ni kama amemwaga mboga kwenye klabu hiyo baada ya jana kuiumbua akibainisha masaibu mbalimbali yaliyomfika tangu arejee klabuni hapo akitokea Azam na Simba.
Ngassa au ‘Uncle’ kama anavyofahamika kwa mashabiki wa klabu hiyo alieleza kuwa, hataki tena kucheza soka nchini baada ya mkataba wake na Yanga kumalizika msimu huu.
Alibainisha mbele ya waandishi wa habari kuwa anajutia kitendo chake cha kukataa kujiunga na El- Merreikh ya Sudan alipopata nafasi hiyo.
Winga huyo ambaye baada ya mazoezi ya jana asubuhi alipelekwa klabuni akishinikizwa azitolee ufafanuzi habari zilizotolewa juzi kuhusu hatma yake ndani ya klabu hiyo, alieleza bayana kuwa hana raha tena na soka kutokana na deni linalomkabili.
Katika mkutano uliofanyika makao makuu ya klabu hiyo, mtaa wa Twiga na Jangwani, Ngassa alieleza kuwa ameichezea Yanga kwa mapenzi, bila kulipwa chochote kufuatia mshahara wake mzima kukatwa kutokana na deni la Sh45 milioni alilokopa akiwa Simba msimu wa 2012/13.
Deni hilo, Ngassa alisema aliahidiwa na viongozi wa klabu hiyo kusaidiwa kulipa, jambo ambalo limekuwa kinyume.
Mchezaji huyo anayeichezea pia Taifa Stars aliwasili klabuni hapo saa 5.00 asubuhi, akifuatana na kocha mkuu, Hans Pluijm na meneja Hafidh Salehe, wakiwa kwenye gari dogo la klabu hiyo aina ya Hiace.
Baada ya kuwasili, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya klabu hiyo, Jerry Muro, mwanasheria Frank Chacha walimpokea na kisha kuingia naye kwenye chumba cha mkutano.
Muro alianza kuzungumza kwa jazba, akiwataka waandishi wa habari kutowahoji wachezaji hadi watakapopata vibali maalumu, huku akidai vyombo vya habari vimeripoti uongo kuhusu matukio ya mchezaji huyo ndani ya klabu.
Dakika kumi baadaye, Muro alimtaka Ngassa azungumze, ingawa mchezaji huyo alihoji aongelee kitu gani? Ndipo Muro alipomtaka aelezee safari yake ya Afrika Kusini na makato ya deni analodaiwa.
Tofauti na ilivyotarajiwa na Muro, Ngassa aliweka wazi namna uongozi wa klabu ulivyomgeuka, akijutia kitendo chake cha kukataa kujiunga na El- Merreikh ya Sudan ambako klabu za Simba na Azam zilipanga kumpeleka msimu uliopita wakati akiichezea Simba kwa mkopo kutoka Azam.
“Najutia uamuzi wangu wa kukataa kujiunga na El- Merreikh, timu iliyotaka kunipa ‘dau’ kubwa na kuamua kurudi Yanga kwa mapenzi yangu, hilo ni kosa langu siwezi, kumlaumu mtu.
“Niwaambie mashabiki wangu, mkataba wangu na Yanga utakapokwisha sitarajii kuendelea kucheza soka katika timu yoyote hapa nchini,” alisema Ngassa.
Hata hivyo, baada ya maelezo hayo, Muro alimzuia mchezaji huyo kujibu maswali ya waandishi wa habari kwa kile alichoeleza kila kitu kuhusu Ngassa atakijibu yeye.
“Ngassa hapaswi kujibu chochote, amechukuliwa mazoezini mara moja ili kutolea ufafanuzi suala hili, utaratibu wa Yanga baada ya mazoezi wachezaji wanapumzika, hivyo anatakiwa kuondoka,” alisema Muro na kumtaka Ngassa atoke nje ambako alipokelewa na kocha wake (Pluijm) aliyezungumza naye kwa muda kabla ya kwenda kuzungumza na mwanachama mmoja, Mzee Akilimali na kisha kuondoka.
Akizungumzia namna viongozi wa klabu hiyo walivyomgeuka, Ngassa alisema baada ya kukataa kujiunga na El- Merreikh uongozi wa klabu hiyo ulimuahidi kumsaidia kumlipia deni lake analodaiwa benki.
“Wakati wa mchakato wa deni hilo, viongozi walinifuata nikiwa mazoezini na kunichukua, sikujua kama tunakwenda benki, tulipofika huko walinitaka nisaini fomu za benki na wao kuahidi kunisaidia kulipa deni, mwanzoni niligoma, lakini waliposema watanisaidia kulipa, nikasaini. “Baada ya pale walinigeuka, deni nikawa nalipa mwenyewe, mwanzoni nilikuwa nakatwa Sh500, 000, kisha milioni moja na sasa nakatwa mshahara wangu wote, hali hiyo imeniathiri na kunifanya nikose raha ya kucheza soka.”
Niwaombe viongozi wangu kama watanisaidia kulipa, naamini itanisaidia pia kujituma zaidi na kuwa mfungaji bora, “ alisema.
Akizungumzia madai hayo, Muro alisema Ngassa amekuwa akikatwa fedha yote ya mshahara kutokana na kukaa mwaka mzima bila kufanya marejesho ya fedha alizokuwa akidaiwa.
“Makubaliano ya awali yalikuwa Ngassa akatwe Sh500,000 kila mwezi katika fedha yake ya mshahara ambao ulipitia benki, hata hivyo uongozi uliopita haukupitisha mshahara wake benki kwa kipindi cha mwaka mzima na kumlipa mkononi.
“Tulipoingia sisi tulihitaji kuweka mambo sawa, hivyo tulikaa na kuzungumza, tukaanza kupitishia mshahara wake benki, kitendo cha benki kuukata wote ni kufidia fedha deni ambalo kwa mwaka mzima halikuwa limekatwa kama makubaliano yalivyokuwa,” alisema.
Alisema analipeleka suala lake kwa uongozi ili kuona watamsaidia vipi mchezaji huyo sanjari na kuanza naye mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya.
Alibainisha kuwa Ngassa anajielewa, ana uhuru wa kuamua mambo yake kama mchezaji.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment