MIZENGO PINDA APIGA MARUGUKU UKARABATI WA MAABARA ZA ZAMANI NA KUMCHIMBIA MKWARA NZITO MKUU WA MKOA IRINGA.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akitazama mafunzo kwa vitendo ya kumfanyia upasuaji panya yaliyokuwa yakifanywa na wanafunzi wa kidato cha tatu, Rosemary Kapugi (kushoto) na Faudhia Ndunguru (wa pili kushoto) wakati alipotembelea maabara ya Bayolojia ya shule ya sekondari ya Kiwere, jimbo la Kalenga akiwa katika ziara ya mkoa wa Iringa juzi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amepiga marufuku ukarabati wa maabara za zamani za shule za sekondari na kusisitiza kwamba ni lazima zijengwe mpya kama ambavyo Serikali ilielekeza.
Alitoa agizo hilo jana mchana, wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa Kata ya Ilula, baada ya kukagua ukarabati wa maabara za sayansi kwenye Shule ya Sekondari Ilula, wilayani Kilolo, mkoani Iringa.
“Mmefanya ukarabati kwenye jengo lililojengwa zaidi ya miaka 20 iliyopita. Kuna chumba nimekuta ni kidogo mno sababu hakiendani na maelekezo ya sasa... chumba kimoja kimepasuka ukuta, hapana! Mkuu wa Mkoa kama kuna nyingine ya aina hii kazi isiendelee.
“Huu ukarabati mliofanya ni kinyume na maelekezo ya Serikali ya kutaka zijengwe maabara mpya. Tulisema zijengwe maabara mpya, ili zidumu kwa miaka mingi kidogo. Kuna chumba dari iko chini kwa sababu ujenzi ni wa zamani.
Ujenzi wa sasa mapaa yako juu zaidi ili kuruhusu hewa ya kutosha. “Ningeweza kusema vunjavunja, lakini haitakuwa haki kwa sababu kuna fedha za watu zimetumika... kwa sasa yatatuhifadhi kwa muda kidogo, lakini haya majengo hayatadumu hata kidogo,” alisema.
Waziri Mkuu pia alikataa kuahidi mchango alioombwa achangie na kuwaeleza kwamba atakuwa tayari kuchangia ujenzi wa jengo jipya na siyo ukarabati, kwani huo utakuwa ni upotevu wa fedha.
Majengo aliyooneshwa Waziri Mkuu Pinda, yalijengwa mwaka 1995 na yalikuwa yakitumika kama maabara kwenye sekondari hiyo. Alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza asimamie watu wake ili ujenzi wa maabara ukamilike kwa muda uliopangwa.
Mkoa huo unahitaji maabara 72 na zilizokamilika ni maabara tano tu huku nyingine 53 zikiwa kwenye hatua mbalimbali za ujenzi na 13 bado ziko kwenye msingi na moja iko kwenye lenta.
Awali akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mtendaji wa Kata ya Ilula, Titus Katemo alisema Shule ya Sekondari Ilula ilijenga maabara zake mwaka 1995 kwa nguvu za wananchi na zilikuwa zikitumika kipindi chote hicho.
Alisema ili kuendana na matakwa ya Wilaya, ukarabati wa vyumba vitatu ulianza Novemba 15, mwaka jana kutokana na vyumba hivyo kutumiwa na watahiniwa wa kidato cha nne wa mwaka 2014 kwenye mitihani ya vitendo.
“Makisio ya gharama za ukarabati wa vyumba vitatu yalikuwa Sh milioni 38.29 na tunatarajia ukarabati utakamilika ifikapo Machi 30, 2015,” alisema na kumuomba Waziri Mkuu awaunge mkono kwa mchango kwani kasi ya wananchi kuchangia imekuwa ndogo.
Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake wilayani Kilolo jana alitarajiwa kukagua mradi wa umwagiliaji wa Nyanzwa na kuzungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment