MSICHANA AWABWAGA WAVULANA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE MWAKA 2014 TANZANIA.
Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde
MATOKEO ya Mtihani wa Taifa wa Kumaliza Elimu ya Sekondari uliofanyika mwaka jana, yametangazwa huku msichana wa shule ya Baobao iliyoko mkoani Pwani akiongoza kwa ufaulu.
Kwa mujibu wa matokeo hayo yaliyotangazwa jana na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde, mwanafunzi aliyeibuka kidedea ni Nyakaho Marungu ambaye ndiye mwanafunzi bora wa mtihani wa kidato cha nne 2014.
Dk Msonde alisema mbali na Nyakaho, mwanafunzi wa pili (wapo tano) kwa ubora na shule zao ni, Elton Jacob (Feza Boys), Samwel Adam (Marian Boys), Fairness Mwakisimba (St Francis Girls) na Mugisha Lukambuzi (Bendel Memorial).
Katika nafasi ya sita kitaifa ni Paul Jijimya (Marian Boys), akifuatiwa na Angel Lundgreen Mcharo (St Francis Girls), Atuganile Jimmy (Canossa), Jenifa Lundgreen Mcharo (St Francis Girls) na Mahmoud Bakili (Feza Boys).
Kwa upande wa wasichana bora wameongozwa na kinara wa kitaifa, Nyakaho (Baobao) na kufuatiwa na Fairness Mwakisimba (St Francis Girls), Angel Mcharo (St Francis Girls), Atuganile Jimmy (Canossa), Jenifa Mcharo (St Francis Girls).
Wengine ni Levina Ndamugoba (Msalato), aliyeshika nafasi ya sita akifuatiwa na Veronica Wambura (Canossa), Sifaely Mtaita (St Marys Mazinde Juu), Catherine Ritte (St Francis Girls) na Anastazia Kabelinde (Kaizirege).
*Wavulana bora
Kwa upande wa wanaume ni Elton Jacob (Feza Boys), Samwel Adam (Marian Boys), Mugisha Lukambuzi (Bendel Memorial), Paul Jijimya (Marian Boys) na Mahmoud Bakili (Feza Boys).
Wengine ni Amani Andrea (Moshi Technical), Mahmoud Msangi, Elias Kalembo, Haji Gonga na Kelvin Sessan kutoka Feza Boys.
*Shule 10 bora
Dk Msonde alitaja shule 10 bora kwa shule zenye idadi ya watahiniwa zaidi ya 40 kuwa ni Kaizirege (Kagera), Mwanza Alliance (Mwanza), Marian Boys (Pwani), St. Francis Girls (Mbeya), Abbey (Mtwara), Feza Girls na Canossa (Dar), Bethel SABS Girls (Iringa), Marian Girls (Pwani) na Feza Boys (Dar).
*Zilizoshika mkia
Shule 10 za mwisho ni Manolo (Tanga), Chokocho (Pemba), Kwaluguru (Tanga), Relini (Dar), Mashindei (Tanga), Njelekela Islamic Seminary (Kigoma), Vudee (Kilimanjaro), Ruhembe (Morogoro) na Magoma (Tanga)
*Hesabu pasua kichwa
“Katika masomo ufaulu wa juu ni wa somo la Kiswahili, ambapo asilimia 69.66 ya watahiniwa wote waliofanya somo hilo, wamefaulu huku ufaulu wa chini kabisa ukiwa katika somo la Hisabati ambao ni asilimia 19.58.”Pamoja na ufaulu wa masomo ya sayansi kuendelea kuimarika kidogo ukilinganisha na mwaka 2013, lakini wastani wa ufaulu kwa masomo mengi uko chini ya asilimia 50, hivyo juhudi zinahitajika katika kuinua kiwango cha ufaulu wa masomo yote,” alisema Dk Msonde.
Masomo ambayo ufaulu wake uko zaidi ya asilimia 50, ni Kiswahili (69.66), Kiingereza (55.10) na Kemia (56.73).
*Matokeo yaliyofutwa
Baraza limefuta matokeo ya watahiniwa 184 waliobainika kufanya udanganyifu, watahiniwa 128 wakiwa ni wa kujitegemea na 56 ni watahiniwa wa shule.
Dk Msonde alisema wanafunzi hao 128 walifanya mitihani yao katika vituo vya watahiniwa wa kujitegemea vya Kisesa na Ubago.
“Baraza limezitaka mamlaka husika kuchukua hatua za kinidhamu kwa wasimamizi waliosimamia mitihani kwa mujibu wa sheria za utumishi, kwani hiwezekani karatasi moja ya majibu ya maswali yakajibiwa na watu tofauti wakati msimamizi yupo,” alisema.
Aidha Dk Msonde alisema watahiniwa wa shule 42 ambao walishindwa kufanya baadhi ya masomo na 47 ambao hawakufanya mtihani yao yote, wamepewa fursa ya kufanya mtihani kwa mwaka 2015.
Ikilinganishwa na watahiniwa wa shule waliofaulu katika mtihani kwa matokeo haya ni 167,643, wakati mwaka 2013 waliofaulu walikuwa watahiniwa 201,152.
Hata kwa wanafunzi wa kujitegemea, matokeo yanaonesha waliofaulu ni wachache ikilinganishwa na waliofaulu mwaka 2013. Matokeo hayo yameonesha kuwa watahiniwa 29,162 wamefaulu mtihani wa mwaka 2014, wakati mwaka 2013 watahiniwa 34,075 wa kujitegemea walifaulu.
Katika ubora wa ufaulu, waliopata distinction ni watahiniwa 7,375 (3.07%), merit watahiniwa 25,131 (10.46%), credit ni watahiniwa 41,326, pass ni watahiniwa 93,822 na waliofeli ni 72,667 ambayo ni asilimia 30.24.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment