RAIS JAKAYA KIKWETE: MGOMBEA URASI BADO HAJAJITOKEZA, WALIOJITOKEZA KUWANIA NAFASI HIYO IMEKULA KWAO ?.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete amedokeza kuwa atakayekuwa mgombea wake wa urais baadaye mwaka huu ni yule ambaye hajajitokeza mpaka sasa.
Akihutubia jana katika sherehe za miaka 38 ya kuzaliwa kwa chama hicho mjini Songea, mkoani Ruvuma, Rais Kikwete alisema: “Wapo watu wenye sifa zote za urais lakini hawajitokezi na hata wakiambiwa kuwa wanaweza husema hawajajiandaa. Hawa ndiyo tunaowahitaji kwa kuwa wanahitaji kukumbushwa tu.”
Kauli hiyo ya Rais Kikwete inaweza kuwa mwiba mchungu kwa baadhi ya makada wa CCM ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakipita huku na kule kutafuta uungwaji mkono, huku baadhi yao wakiwa wamepewa onyo kali kutokana na kushiriki kampeni kabla ya muda na kushiriki vitendo ambavyo ni kinyume na maadili.
Katika hotuba yake iliyorushwa moja kwa moja na vituo vitatu vya televisheni, Rais Kikwete alisema chama hicho kitakuwa na mgombea bora wa urais kwa kuwa upo utaratibu mzuri wa kumpata kwa kutumia kanuni walizojiwekea. Pia alieleza kwa msisitizo kwamba kinachokatazwa ni ‘kukiuka kanuni na taratibu.’
“Oktoba tunachagua rais, mimi nataka rais huyo atoke CCM. Chama kina mfumo wa kumpata mgombea mzuri wa urais na nawahakikishia kuwa tutakuwa na mgombea bora wa urais na wananchi hawatanung’unika,” alisema na kuongeza:
“Ushindi ni lazima na nayasema haya kwa bariiidiii na uhakika. Najua kuwa wapinzani wetu hawana chao.”
Rais alieleza kuwa ni lazima CCM ishinde katika uchaguzi mkuu ujao hasa kwa kuzingatia kuwa imekuwa ikifanya hivyo tangu mfumo wa vyama vingi uanzishwe, zaidi ya miaka 20 iliyopita.
Alisema ushindi huo haupingiki kwa chama hicho kutokana na idadi kubwa ya wanachama waliopo na wale wanaotarajiwa kuandikishwa mwaka huu.
“Tunao wanachama milioni sita mpaka sasa na katibu mkuu anapanga kutoa kadi nyingine milioni mbili kwa wanachama wapya. Hiyo itatufanya tuwe na wanachama milioni nane watakaokipigia kura chama chetu. Hiyo ni idadi kubwa kuliko chama chochote cha siasa kilichopo hapa nchini. Huo ni mtaji wa kutosha tulionao kabla ya uchaguzi wenyewe,” alisema.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo aliwatahadharisha wanachama wake kuwa ni lazima wajiandae kukabiliana na upinzani uliopo na ili kufanikisha hilo, aliwataka wale wote wenye nia kuanza kuwa karibu na wananchi ili kusikiliza kero walizonazo.
Alisema mwaka huu ni lazima kila kiongozi ahakikishe anajiweka katika maandalizi kamili; ndani na nje ya chama ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza wakati wowote wa kuelekea katika kinyang’anyiro hicho. “Pamoja na uhalisi wa ushindi katika uchaguzi ujao, upinzani unaanzia ndani ya chama. Tushindane kwa nia njema na baada ya hapo tuimarishe umoja miongoni mwetu ili kuwakabili wapinzani,” aliongeza.
Mfuko wa uchaguzi
Rais Kikwete alitumia fursa hiyo kuwakumbusha viongozi wa chama hicho kuanzisha mifuko ya uchaguzi kila mkoa ili kuwa na uhakika wa kuendesha kampeni kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, alitahadharisha umakini katika upokeaji wa fedha kutoka kwa watu, taasisi au shirika lolote litakalokuwa tayari kuchangia kwa hofu ya kuwapo kashfa zozote za rushwa na ufisadi ambao unaweza kukichafua chama.
“Tulikubaliana kila mkoa uwe na mfuko wa uchaguzi utakaoendesha shughuli za ngazi zote. Natoa tahadhari hapo kuwa makini na fedha zinazotolewa na wachangiaji. Msichukue fedha zenye matatizo… msichukue fedha za moto kwani mtaungua mikono,” alisema Rais Kikwete.
“Kila ofisi ya mkoa na wilaya inayo gari zuri kabisa. Land Cruiser, mkonga. Yatumieni magari hayo kuwafikia wananchi, ila msiendee shambani kwenu. Wasikilizeni wanataka nini na muwaambie wakuu wa mikoa na wilaya washughulikie matatizo waliyonayo. Bila kufanya hivyo hatuwezi kushinda,” alisema.
Kutengua ahadi walizoshindwa
Mwenyekiti aliwakumbusha viongozi wa chama chake kutengua ahadi walizoshindwa kuzitekeleza na kuandaa majibu ya kwa nini wameshindwa ili kuepusha hamaki ambazo zinaweza zikawaangusha.
Aliwakumbusha kuwa walitoa ahadi nyingi ambazo wanaweza kuwa wamezisahau lakini wananchi walioahidiwa bado wanazikumbuka, hivyo watakaporudi ni lazima wataulizwa wameshindwaje kuzitekeleza.
“Wakati wa kampeni zilizopita tulitoa ahadi nyingi. Tulifanya hivyo kila tulipobanwa katika kinyang’anyiro kile ili tufanikiwe. Tunapokwenda tena kwa wananchi lazima tuwe na maneno mazuri ya kuwaeleza, la sivyo tutahamaki kwa maswali watakayotuuliza na kuwaambia walioliza kuwa wametumwa,” alisema.
Alitumia hadhira hiyo kueleza namna alivyotekeleza ahadi kadhaa alizozitoa kwa wananchi wa Ruvuma katika ziara aliyoifanya miezi minne iliyopita.
“Nilitoa ahadi ya ujenzi wa hospitali ya rufaa, niulize uongozi wa mkoa, mmetenga eneo hilo? Mkifanya hivyo kazi yangu inakuwa ni kuikumbusha Wizara ya Afya ianze utekelezaji wa zoezi hilo mara moja. Tayari Sh8 bilioni zimeletwa kwa ajili ya malipo. Niliambiwa kuwa wanataka kuanza kuwalipa lakini nikasema isiwe hivyo badala yake waanze wakulima, maana Serikali haiwezi kudaiwa na maskini,” alisema Rais Kikwete.
Vilevile, alieleza utekelezaji wa ujenzi wa njia ya umeme kutoka Njombe mpaka Songea na kuelekea Wilaya za Mbinga na Namtumbo ili kuvifikia vijiji 300 vya mkoa huo kuwa utekelezaji wake umeanza na utakapokamilika mkoa huo utakuwa miongoni mwa iliyonufaika zaidi.
Ukawa na kura ya maoni
Akizungumzia msomamo wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaoundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD kuhusu kura ya maoni, Rais Kikwete alisema sababu ya kutangaza kususia kura ya maoni ni kutowapo kwa Serikali tatu katika Katiba Inayopendekezwa na si vinginevyo.
Januari 24, mwaka huu, Ukawa walitangaza kutoshiriki kura ya maoni inayotarajiwa kufanyika Aprili 30 kutokana na maandalizi duni yanayofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Pamoja na hayo Rais Kikwete alisema hakushangazwa aliposikia Ukawa wamesusia kura ya maoni kwa kuwa hata bungeni walisusa; “Ninawashauri wasisuse, washiriki kwenye kura ya maoni, lakini kama wataendelea na msimamo wao, wananchi wasiwasikilize wajitokeze kupiga kura ya maoni.
“Nawashangaa hawa jamaa, kwa sababu kushiriki katika kupiga kura ya maoni ndiyo wataweza kuikataa kidemokrasia Katiba Inayopendekezwa lakini wakisusa itapita kwa sababu watakaoipigia ni wale tunaoikubali,” alisema.
“Naona kama wangekuwa watu makini wangeshiriki katika zoezi hilo ili wapige kura ya hapana kuikataa,” alisema Kikwete.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema iwapo Katiba Inayopendekezwa itakataliwa, Katiba ya sasa itaendelea kutumika na haijulikani kama rais ajaye atalipa kipaumbele suala la Katiba.
“Tunaweza kumpata rais ambaye Katiba kwake siyo kipaumbele na kuendelea kuitumia hii ya sasa,” alisema.
Akizungumzia maandalizi ya kura ya maoni, Rais Kikwete alisema uandikishaji wa daftari utaanza katikati ya mwezi huu na kwamba kila mwananchi ahakikishe anajiandikisha la sivyo hatakuwa na sifa ya kupiga kura kwenye kura ya maoni na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Rais Kikwete aliwataka wanachama wa CCM kuwakumbuka waasisi wake kuhakikisha wanaondokana na utegemezi wa fedha kutoka kwa wafadhili, wafanyabiashara na wahisani.
Sherehe hizo zilihudhuriwa pia na Makamu mwenyekiti wa Chama tawala cha Uganda; National Resistance Movement (NRM), Kapteni Michael Mukura, Katibu Mkuu, Jestine Lumumba, Mweka Hazina, Rose Namayanja na ofisa wake wa uchaguzi, John Kiangi.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment