BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

RIPOTI YA MABILIONI YA FEDHA ZA USWISI IPO TAYARI.


Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju akizungumza kwenye mkutano na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, Dar es Salaam jana. Picha na Abuu Kimario.


Dar es Salaam. Kamati iliyoundwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kuchunguza mabilioni ya fedha yaliyofichwa na baadhi ya Watanzania katika benki mbalimbali nchini Uswisi, imekamilisha uchunguzi na inasubiri kukabidhi ripoti ya kazi hiyo kwa Spika wa Bunge.


Hayo yalisemwa jana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alipokuwa akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, Dar es Salaam.


Masaju alisema kamati hiyo ilikamilisha kazi yake baada ya kuwahoji watu mbalimbali na kukamilisha kazi hiyo kama walivyoagizwa na Bunge na kinachosubiriwa ni kuikabidhi kwa chombo hicho cha kutunga sheria.


“Ofisi yangu kupitia kamati iliyoundwa tulikwishamaliza kazi hii, lakini hatuwezi kutoa taarifa kupitia sehemu nyingine zaidi ya ofisi iliyotupatia kazi kama utaratibu unavyoelekeza.


“Sasa wananchi na nyie waandishi wa habari msubiri taarifa hiyo itolewe kule bungeni ambako tuhuma hizi zilianzia,” alisema Masaju.


Watuhumiwa


Vigogo 10 wametajwa kuhusika katika kashfa hiyo. Inadaiwa kuwa katika orodha hiyo, yupo kiongozi mmoja mwandamizi mstaafu, maofisa watatu wastaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), mawaziri wastaafu ambao baadhi yao bado ni wabunge na aliyewahi kuwa kiongozi mwandamizi wa Benki Kuu Tanzania (BoT).


Kamati ilivyoundwa


Kamati hiyo maalumu iliundwa kwa Azimio la Bunge baada ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kuibua tena tuhuma hizo bungeni mapema mwaka jana, akidai kuna vigogo walioficha Sh323.4 bilioni katika benki mbalimbali za Uswisi.


Kiasi hicho cha fedha kinaweza kujenga barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 300 ambao ni sawa na kutoka Morogoro hadi Iringa.


Kwa mara ya kwanza, tuhuma hizo zilitolewa bungeni na Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), mwaka 2012.


Katika kikao cha Tisa cha Bunge, Zitto aliwasilisha hoja binafsi kulitaka Bunge kuchunguza na kuielekeza Serikali kuchukua hatua dhidi ya Watanzania aliowaita vigogo walioficha fedha na mali haramu nje ya nchi.


Kutokana na hoja hiyo, Bunge chini ya Spika Anne Makinda, liliipa Serikali muda wa mwaka mmoja ambao ulimalizika Oktoba mwaka jana iwe imekamilisha uchunguzi na kuwasilisha ripoti yake bungeni.


Wakati sakata hilo lilipokuwa limepamba moto, Serikali ya Uswisi kupitia kwa Balozi wake nchini, Olivier Chave iliwahi kusema Serikali ya Tanzania haijaonyesha nia ya dhati kutaka kuchunguza na kurejesha mabilioni ya fedha hizo.


Balozi Chave alikaririwa wakati huo akisema hawajaona jitihada zozote zilizofanywa na Serikali ya Tanzania kutaka kuzipatia ufumbuzi tuhuma hizo.


Chave alisema nchi yake iko tayari kushirikiana na Tanzania kujua uhalali wa fedha hizo na endapo zitagundulika ni chafu watakuwa tayari kuzirejesha nchini.


Taarifa kutoka Benki Kuu ya Uswisi inaonyesha kuwa baadhi ya fedha hizo zimewekwa katika akaunti za vigogo hao na kampuni za mafuta na gesi zilizopo nchini.


Hata hivyo, Machi mwaka jana ilielezwa kuwa mabilioni ya shilingi yaliyowekwa na Watanzania katika benki za Uswisi yalikuwa yameanza kuhamishwa kimyakimya.


Ripoti ya Benki za Uswisi ya 2012 ilionyesha kuwa fedha zinazotoka Tanzania zilipungua kwa karibu Sh36.4 bilioni ikilinganishwa na zilizokuwapo 2011 nchini humo, lakini haielezi sababu ya kupungua kwake.


Watanzania 99


Hivi karibuni, Timu ya Wanahabari wa Kimataifa wanaoandika Habari za Uchunguzi (ICIJ) ilitoa ripoti ikisema Watanzania 99 wanamiliki Dola za Marekani 114 milioni (Sh193bilioni) kwenye akaunti za benki nchini Uswisi.


Ripoti hiyo inayoitwa SwissLeaks iliyotolewa Marekani, imesheheni taarifa za Benki ya HSBC ya Uswisi na namna watu maarufu wakiwamo wanasiasa, wachezaji, viongozi wa dini na wafanyabiashara walivyoficha mamilioni ya fedha na kufanikiwa kuzikwepa mamlaka za mapato katika nchi zao.


Katika orodha hiyo, Tanzania inashika nafasi ya 100 duniani na nafasi ya pili Afrika Mashariki ikiwa nyuma ya Kenya inayoshika nafasi ya 58 duniani kwa kuweka zaidi ya Sh950 bilioni nchini Uswisi.


Ingawa taarifa hiyo haikutaja majina ya watu wote walioweka fedha Uswisi, imemtaja mfanyabiashara Shailesh Vithlani ambaye anadaiwa kuwa dalali wakati Tanzania iliponunua rada kutoka kwa kampuni ya BAE system kuwa ni miongoni mwao.


Hivi karibuni, Waziri wa Fedha Saada Mkuya alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akitahadharisha kwamba si kila aliyeweka fedha Uswisi amezipata kwa njia haramu.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: