BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

UKUU WA WILAYA SASA UNAVYOGAIWA KAMA PELEMENDE (PIPI) SERIKALI YA TANZANIA.


Hawra Shamte.
Ilinibidi nikae chini na kufanya fikra jadidi, hivi ni sifa gani mtu anapaswa awe nazo ili angalau achaguliwe kuwa Mkuu wa Wilaya ?.

Niliwaangalia watu ninaowafahamu ambao wamepata nafasi hiyo ya kuwa wawakilishi wa rais katika wilaya, nikaangalia sifa walizonazo, kielimu, kiutendaji na kimsimamo au kiitikadi.


Nikagundua kuwa mtu anapaswa awe hodari wa kujipendekeza, ili aonekane. Anapaswa afanye mambo ambayo ataonekana wazi kuwa ni mfuasi wa mtu fulani, au chama fulani, ikibidi hata kusema uongo.


Nikagundua kuwa kumbe si lazima uwe na sifa za kusifika ili uwe mkuu wa wilaya. Mara nyingine kwa sisi waandishi ukitumia kalamu yako kuandika yanayowapendeza au kauli zako kuonyesha kujipendekeza na kujiainisha kwamba unasaidia mrengo fulani, unaweza kupewa ukuu wa wilaya kama ahsante.


Wananchi wa kawaida tu wanafahamu kuwa ukuu wa wilaya hauna tija kwa Taifa, kwani hayo waliyasema wakati wa kukusanya maoni ya Katiba Mpya.


Walisema kuwa wilayani wapo Wakurugenzi wa wilaya, wako wabunge, wako madiwani na mlolongo mzima wa watendaji ambao kwa hakika wanafanya kazi sawa na za mkuu wa wilaya.


Wakurugenzi wa wilaya ndiyo wenye fungu la fedha za kuendesha shughuli za maendeleo ya wilaya husika, kumweka mkuu wa wilaya juu ya mkurugenzi wa wilaya ni kuongeza urasimu tu wilayani na sehemu nyingine kusababisha migogoro.


Nchi yetu ni masikini lakini matumizi ya Serikali ni makubwa tofauti na kipato kinachokusanywa. Wakuu wa wilaya ni marais wa wilaya husika, kwa sababu ni wawakilishi wa rais, hawa huwa na hadhi kubwa wilayani na gharama zao pia ni kubwa. Wanapewa nyumba, gari, gharama za ziara na masurufu mengine muhimu.


Wakati huohuo yupo mwakilishi mwengine wa Serikali ambaye ni Mkurugenzi wa Wilaya. Huyu angetosha kabisa kufanya kazi za mkuu wa wilaya, tofauti yake ni kuwa huyu si mwanasiasa, hivyo pengine huyu si rahisi kuburuzwa.


Huyu hufanya kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za kazi za Serikali wakati yule anayefanya kazi za kisiasa husubiri kupokea maagizo, mara nyingine hata utekelezaji wa maagizo hayo ni kitendawili.


Mathalan mkuu wa wilaya huambiwa kuwa ahakikishe kuwa katika wilaya yake kila shule ina maabara, wakati hajapewa fungu la kusimamia uanzishwaji wa maabara. Anatarajia fungu la wilaya lililopo kwa mkurungenzi wa wilaya, fungu ambalo ni la bajeti mahsusi ambayo ilipitishwa wakati wa bajeti kuu ya Serikali, hivyo hakuna kasma ya kujenga maabara.


Hapo ndipo kizungumkuti kinapoanza, mkuu wa wilaya anasisitiza agizo la rais litekelezwe bila kujali kuwa hakuna fungu la kufanya hivyo, matokeo yake tunayaona, majengo ya maabara hayana vifaa.


Hii maana yake nini? Ni kuwa miradi ya maendeleo imebinywa na sasa haitekelezeki kwa sababu fedha zimepelekwa kwenye ujenzi wa maabara.


Kupanga ni kuchagua, tunaposhindwa kupanga vyema, tunapanga kushindwa kutekeleza shughuli za maendeleo ya Taifa.


Nchi hii ina wilaya 133 ndiyo kusema kuwa tuna wakuu wa wilaya 133, kuna majimbo 239, maana yake kuna wabunge 239 wa kuchaguliwa, 102 viti maalumu wote hawa wanapaswa wasaidie katika utendaji wa wilaya ama majimbo wanayotoka.


Bado kuna wakurugenzi, madiwani, wenyeviti wa chama na wengine kwa mzo katika nafasi mbalimbali za utendaji wa wilaya, je, kwa mlolongo wote huo wa watendaji kulikuwa na haja ya kuwa na wakuu wa wilaya?


Muundo wa Serikali yetu ni mkubwa sana, hivyo kufanya ugumu katika uwajibikaji. Ilidhaniwa kuwa kuwa na watu wengi ndiyo kunarahisisha utekelezaji wa mambo na ufikishaji wa maagizo muhimu, lakini uzoefu hauonyeshi hivyo, bali ni kuongeza gharama za uendeshaji wa Serikali ambazo mzigo wote huo anaubeba mlipakodi.


Baraza la Mawaziri pekee lina mawaziri 56, wakati Baraza la Mawaziri la Marekani lina watu 16 tu, Canada wana wajumbe 39, India wako 45. Unaweza ukadadavua mwenyewe kuona kama kuna uhusiano baina ya ukubwa wa Serikali na utendaji wa kimaendeleo wa serikali husika.


Katika mambo ambayo yalikuwamo katika rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Jaji Warioba ni kupunguza madaraka ya rais ya uteuzi na kwamba ziundwe taasisi za kikatiba za kumshauri rais kabla hajafanya teuzi. Katiba inayopendekezwa imeyafuta mapendekezo hayo ya wananchi na kumuongezea rais madaraka.


Pengine kungekuwapo taasisi za kumshauri rais kabla ya kufanya uteuzi, vyeo vingi visingegaiwa kama peremende. Zingewekwa sifa za mtu kuwa mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya na kadhalika.


Kama yuko mwenyekiti wa chama kinachotawala katika wilaya, kwa nini tuwe na kiongozi mwingine wa rais ambaye ndiye mwenyekiti wa chama chenye serikali iliyopo madarakani?


Kugawana vyeo kwa urafiki au kulipa fadhila si mtindo mzuri wa uendeshaji wa Serikali, pamoja na kwamba ni muhimu rais kuzungukwa na watu anaowaamini, lakini vilevile ni muhimu kwa kiongozi kuzungukwa na watu wenye uwezo wa kiutendaji, wenye uwezo wa kimawazo na wenye maadili ya kutukuka.


Ndio maana tunawaona watu waliowapiga na hata kuwatusi waliowahi kuwa viongozi wa juu wakipewa kazi hiyo. Watu wanajiuliza kwa sifa zipi walizonazo?


Huko ni kupeana vyeo kwa varange varange, kila anayevuruga kwa maslahi ya chama ndiye anayefaa kuongoza wilaya au mkoa, hapa ndipo tunapouharibu mfumo wa uongozi wa nchi yetu.


Ingekuwa ukuu wa wilaya una tija, basi ile mikoa saba ambayo haikuwa na wakuu wa wilaya kwa muda mrefu ingekuwa iko taabani kwa migogoro na hata kwa maendeleo.


Tunapozungumzia suala la maendeleo tuangalie pia maendeleo yaliyoko wilayani, je, yanakidhi uwepo wa mlolongo wa viongozi serikalini ?.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: