WENYE ULEMAVU WAPONGEZA KATIBA INAYOPENDEKEZWA.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Amon Mpanju.
WATU wenye ulemavu nchini wamepongeza Katiba pendekezwa na kuelezea kuwa ni mwanga wa walemavu wote nchini kupata haki zao za msingi huku wakitaka ikiwa mchakato wa Katiba utahairishwa masuala yote ya walemavu yaliyomo yaingizwe kwenye mabadiliko yatakayofanywa kwa Katiba ya sasa.
Wamepeana hamasa ya kuhakikisha wanajitokeza kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura tayari kwa ajili ya kupiga kura ya maoni kwa Katiba hiyo huku wakitaka masuala yao kuhamishiwa katika Ofisi ya Rais au Makamu wa Rais ili kuwe na utekelezaji.
Wakizungumza katika warsha ya watu wenye ulemavu kujadili Katiba Inayopendekezwa, aliyekuwa mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba Amon Mpanju ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Amon Mpanju. Alisema Katiba pendekezwa imegusa masuala mengi ya walemavu.
Alitaja baadhi ya masuala hayo kuwa ni pamoja na haki zao kwenye michakato mbalimbali ya uchaguzi katika siasa kwani Katiba pendekezwa imeeleza kutokuwepo na ubaguzi wa aina yoyote, vitisho na unyanyapaa na kutaka vyama vya siasa katika michakato ya kuteua wagombea kutobagua walemavu.
Alisema pia kuna haki ya mawasiliano na kupata habari hivyo mlemavu atakayekosa haki hizo ana haki ya kudai mahakamani katika Ibara ya 55 ya Katiba hiyo huku aya ya sita inakataza ubaguzi wa aina yoyote kwa wenye ulemavu.
Mpanju aliungwa mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi isiyo ya Kiserikali inayoshughulikia masuala ya Haki za Kisheria, Maendeleo ya Jamii na Kiuchumi (DOLASED), Gidion Mandesi aliyesema katika Katiba Pendekezwa kati ya masuala 25 walemavu waliyoomba, 18 yameingizwa.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment