
Geita. Jeshi la Polisi mkoani Geita linawashikilia waganga wa kienyeji 32 kwa tuhuma za kupiga ramli ‘chonganishi’ zinazosababisha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, akiwamo mtoto Yohana Bahati (1) mkazi wa Kijiji cha Ilelema, Wilaya ya Chato mkoani hapa na mauaji ya vikongwe.
Waganga hao ambao walikamatwa kwa nyakati tofauti ni wale wanaojihusisha na kazi za kuwatakasa wanaokata mapanga na kupiga ramli ‘chonganishi’ zinazoenda sambamba na mauaji ya albino.
Akizungumza jana na waandishi wa habari, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa Joseph Konyo, alisema kuwa baada ya kutokea mauaji ya mtoto Yohana Bahati mwenye ulemavu wa ngozi aliyetekwa kisha kuuawa kwa kukatwa mikono na miguu yake, jeshi hilo lilianzisha kampeni ya kuwasaka waganga na wanaofanya kazi ya kukata mapanga.
“Suala la mauaji ya albino ni suala ambalo lina mtandao mkubwa, kuna wakataji, kuna watakasaji, kuna wapiga ramli ambao ni waganga, hivyo tulianzisha kampeni ya kuwasaka na tumefanikiwa kukamata hao 32 katika wilaya zote za mkoa wa Geita,” alisema.
Alisema katika kuwakamata walitumia njia za kiintelijensia na kuna baadhi ya askari walijifanya kwenda kutibiwa kwa waganga hao, kwa kupigiwa ramli na kuelezwa kuwa wamerogwa na wanamikosi hivyo wanatakiwa kusafishiwa nyota hizo kwa kupeleka viungo vya albino.
“Tumewakamata waganga wakiwa na vitu vyao vya uganga kama vile ngozi za wanyama kama chui, simba, ng’ombe, kondoo, mafuta ambayo hayajajulikana ni ya binadamu au ya nini, mapembe ya wanyama ambayo huyatumia kusafiria angani, ungo, vioo vinavyotumika kuonyesha mtu ambaye anatuhumiwa kumroga mteja na vitu mblimbali vinavyotumika kupiga ramli,” alisema Konyo.
Aidha, alisema katika oparesheni hiyo pia walikamata mnyama aina ya kakakuona na ndege wa aina mbalimbali na kwamba waganga hao wanatarajiwa kufikisha mahakamani muda wowote baada ya upelelezi kukamilika.
“Bukombe tumekatama waganga watano, Geita waganga 12, Mbogwe waganga sita Wilaya ya Chato sita, Nyang’hwale watatu na Wilaya ya Nyang’hwale walikamata kobe aliye hai anayetumika kutoa utabiri kwa wanaoenda kuoshwa nyota zao.
“Niseme kwamba wananchi wanadanganywa katika hii operesheni tuliyoifanya tumegundua watu wanadanganywa kisaikolijia kwa kutumia vitu ambavyo siyo vya kawaida vinavyomfanya mtu aamini,” alisema Konyo. Pia, aliwataka wananchi waache kuendekeza imani za kwenda kwa waganga kwa kusema kuwa wanawapotosha kwani hakuna ukweli wowote.
Katika hatua nyingine Konyo alikili kuwepo kwa upungufu wa ushahidi katika kesi ya mauaji ya Albino ya Zawadi Magindu iliyotolewa hukumu jana na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Joacquine De-Mello kwa baadhi ya mashahidi kutokuwapo mahakamani.MWANANCHI

0 comments:
Post a Comment