BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

Dk MOHAMED SHEIN KIOO KIPYA KWA UADILIFU ZANZIBAR.


Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein (Kushoto) akimwapisha Katibu Mkuu wa Cuf, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, wakati wa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa kitaifa (SUK), Novemba mwaka 2010

Watu wengi hawakuamini kama Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, angehimili mikikimikiki na dhoruba ya kuoengoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) hatimaye ifikishe miaka mitano madarakani na kuifikisha ngwe ya uchaguzi wa mwaka 2015 bila Serikali hiyo kuyumba au kugawanyika.


Pamoja na kumudu jambo hilo; Rais wa Zanzibar anabaki Kuwa ndiye kiongozi mwenye sifa pekee ya kuongoza nchi kwa kufuata misingi ya uadilifu, uwazi, uwajibikaji na ushirikishaji hasa anapoitisha vikao vya kiutendaji na tathmini ya mipango kazi ya Serikali kila baada ya miezi mitatu, maarufu bango kitita.


Dk Shein ni kiongozi aliyebahatika kufanya kazi za kiserikali akiwa Naibu Waziri wa Afya chini ya Serikali ya Dk Salimin Amour Jumaa na kuwa Waziri wa Utawala Bora katika Serikali ya Dk Amani Abeid Karume baadaye Makamu wa Rais chini ya Rais Benjamini Mkapa pia akifanya kazi na Rais Dk Jakaya Kikwete kabla ya kuwa Rais wa Zanzibar mwaka 2010.


Kukabidhiwa kwake jahazi la kuongoza SUK inayovishirikisha vyama hasimu vya CCM na CUF na kufikisha miaka mitano; ni ukweli usiopingika Rais huyo ameonyesha ushujaa, umahiri, ujuzi wa kuendesha mambo huku akiwa hakabiliwi na tuhuma za ufisadi, rushwa, uporaji ardhi, matumizi mabaya ya rasilimali za nchi pia hatamani kujitajirisha.


Mara zaote katika uongozi wake akiwa Rais amekuwa akiheshimu misingi ya utawala wa sheria, kuenzi haki za binadamu, kutambua mipaka ya demokrasia na kufuata siasa za wastani katika kuwatumikia wananchi wake.


Katika maeneo yote ambayo amekuwa mtumishi wa umma kwenye Wizara, Dk Shein hatajwi wala hajakumbwa na kashfa za odokozi, ufisadi, ubadhirifu wa mali za umma, upendeleo, ubinafsi na kila wakati amesimama na kuonyesha kuheshimu taratibu, kanuni na utii wa Katiba ya nchi.


Wakati huu nchi na Taifa zikielekea uchaguzi mkuu wa dola, ipo haja na umuhimu wa kupata viongozi wa aina yake kuanzia urais, ubunge, uwakilishi na udiwani kwani kutoka uchaguzi mmoja hadi mwingine kuna kipindi cha miaka mitano ambacho wananchi wakitegemea wapate unafuu katika ujenzi wa uchumi, kwa maendeleo ya jamii na ya kisekta.


Viongozi wetu katika maeneo ya uwalilishi kwenye vyombo vya kutunga sheria kama Bunge na Baraza la Wawakilishi (BLW) yakiwemo na mabaraza ya madiwani, kunahitaji wapatikane aina ya viongozi wasioongozwa na tamaa, uchu wa kupora maliasili na rasilimali, ufisadi au tabia ya kutumia madaraka ili kujitajirisha na kuwaacha waliowachagua wakiishi kwa shida na dhiki.


Ukiacha tabia yake hiyo, Rais huyo wa Zanzibar amebaki si kiongozi anayeongoza kwa vitisho, ubabe, maneno makali au anayeongoza Serikali chini ya kivuli cha uvunjaji wa sheria au ukiukaji wa Katiba zote mbili ikiwamo ile ya Zanzibar ya mwaka 1984 na ya Jamhumri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.


Mara zote amesimama kwa miguu yake na kuonyesha kutii uzalendo, kutobabaishwa, hatikisiki wala kuongozwa na matamshi ya vitisho ambayo wakati mwingine hutoka upande wa hasimu zake kisiasa huku akiwa mgumu wa kupoteza mwelekeo hata pale watu na viongozi wa upande wake wanapomshauri mambo ambayo yako kinyume na misingi iliyowekwa.


Kwa mfano mwanzoni mwa mwaka huu, akifanya ziara ya kuimarisha chama chake na kukutana na mabalozi wa nyumba kumi wa CCM, aliambiwa ipo haja ya kuivunja Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa madai kuwa chini ya mfumo huo Zanzibar imekumbwa na matatizo mengi ikiwamo watu kumwagiwa tindikali na kupigwa risasi kuliko ilivyokuwa katika mfumo wa anayeshinda achukue vyote.


Dk Shein aliwaeleza kinagaubaga wanachama wenziwe kuwa kuundwa kwa SUK ni mchakato ambao kuoondosha kwake lazima kufuate taratibu zile zile na si jambo la kukurupuka au kufumba macho na kufumbua. Akasema ili aongezewe nguvu za kiutawala na kuudhofisha upinzani mambo mawili yanahitajika.


Bila kutafuna maneno akasema lazima wana CCM waipigie kura nyingi nafasi ya urais, pili chama tawala kishinde viti vingi Pemba na Unguja na tatu kikombea majimbo yaliopotea Unguja hapo ndipo kudhoofu kwa upinzani katika uendeshaji Serikali na kupata nguvu za maamuzi, utakapopatikana na si kuamka na mtu kufikiri anaweza kuifuta Serikali iliowekwa na wananchi kwa mujibu wa katiba na sheria.


Si hivyo ila mara zote Dk Shein amekuwa akisema anapata ushauri wa moja kwa moja toka kwa Makamu wa Kwanza na wa Pili wa Rais yaani Maalim Seif Sharif Hamad na Balozi Seif Ali Idd katika masuala ya uendeshaji Serikali, mawaziri chini ya SUK hufanya kazi kwa pamoja na ushirikiano hadi ikishindakana kuwabagua ni yupi CCM na yupi CUF.


Wakati SUK chini ya Dk Shein ikipasua anga na kuchana na mawimbi, nchi kadhaa Barani Afrika zikiwamo Zimbabwe, Sudan Kusini na Kenya zimeshindwa kuhimili suluba ya uendeshaji wa Serikali zenye mifumo hiyo, sasa baadhi ya nchi hizo ziko kwenye mapigano, kuvunjika na nyingine kushirikiana bila ya kuwepo umoja na kutofahamiana.


Katika kipindi hiki wakati aliyekuwa Rais wa Namibia Hifikepunye Pohamba akitwaa Tuzo ya Mo Ibrahim na kujichukulia kitita cha Dola milioni tano, najaribu kumtazama Dk Shein katika jicho jingine huku nikimuona ni kiongozi anayestahili kupigiwa mfano bora katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na Kati kwa utumishi wa uadilifu Visiwani hapa. 


Licha ya Dk Shein kuonyesha unguli katika uendeshaji wa SUK tokea kuundwa kwake, ameonyesha ni madhubuti katika kutetea Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, mpambanaji na mlinzi wa misingi ya Mapinduzi ya Zanzibar pia alipoguswa na waliojaribu kuvuruga haiba ya amani na umoja, Serikali yake ilichukua hatua za kuwakabili waliotaka kumchezea paka sharubu.

Kwa upande mwingine tunapoitazama Zanzibar katika historia ya siasa na chaguzi zake kuu tokea mwaka 1957 hadi mwaka 2009, tunaiona ilivyokumbwa na misukosuko mikubwa ya kisiasa hali iliopekekea viongozi na wafuasi wa vyama vya kisiasa kukosa maelewano na azma ya kufanya kazi pamoja.


Chini ya Serikali ya awamu ya saba Zanzibar hasa baada ya kufanyika maridhiano ya kisiasa vyama vikuu vimefanikiwa kuzika uhasama na sasa chini ya uongozi wa Rais huyo mambo yanakwenda kwa murua huku kiongozi mkuu wa Serikali akionekana kuongoza bila kutikisika.


Kuundwa kwa SUK mwaka 2010 mara baada ya uchaguzi mkuu na kupatikana utulivu, maelewano na vyama vya kisiasa vikuu kushirikiana katika uendeshaji wa Seikali kwa takriban miaka mitano sasa, hapo ndipo ninapolazimika kumuona na kumtafsiri Rais Dk Shein ni kioo kipya cha uadilifu na mhimili imara wa maridhiano yaliopatikana visiwani humu.


Hata hivyo Dk Shein mara zote amekataa katakata kugeuka nyuma huku akikwepa siasa za makundi ambapo historia ikimuonyesha ndiye Rais pekee ambaye ameingia madarakani akiwa hana kundi toka ndani ya chama chake na hata alipokabidhiwa dhamana ya kuongoza nchi amejiweka kando na miruzi ya ushabiki huo.


Si yeye wala watoto wake ambao wameingia hamkani ya kulitumia jina la baba yao kwa ajili ya kuhodhi viwanja na majumba ya Serikali kwa njia isiyo halali, kujiingiza kwenye kazi za biashara huku wakiwa hawana mitaji na rasilimali-fedha vilevile mke wake Mwanamwema mara zote ni mwanamama wa kawaida asiyeongozwa na mbwembwe wala mikogo ya kulitumia jina la nafasi ya mumewe kujinufaisha.


Nafikiri hii si zama tena za kiongozi kusimama hadharani kutoa matamshi yanayotonesha vidonda vilivyoanza kupona, kupotosha umma kwa uzushi wa kitoto ili kusaka ridhaa ya kupata madaraka kwa njia za hila au kufanya uchochezi wa maneno ya kuwagawa wananchi kama baadhi ya wanasiasa wengine Zanzibar wafanyavyo majukwaani.


Mwaka huu ni mwaka ambao kila mtu atavuna kile alichopanda; kama yuko aliyepanda maboga asitegemee kuvuna mpunga, aliyetoa jeuri atakula jeuri yake, bingwa wa hadaa, tapeli wa kisiasa na asiyewatumikia wananchi kwa kuchapakazi, mbabaishaji, mwenye majibu mkato au kujibadili sauti na namba ya simu, asitarajia kama atafaa tena na kupata mtaji wa kura.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: