IGP WA ZAMANI WA JESHI LA POLISI ALIKOSOA JESHI LA POLISI LA TANZANIA, AELEZA ASKARI WA SASA HAWAOGOPWI NA WAHALIFU.
“Askari lazima atishe. Popote anapokuwapo wahalifu wajue kuwa kuna mtu hatari dhidi yao. Kama mhalifu atatiwa woga na uwepo wa polisi, uhalifu utapungua tu na hivyo kubakiwa na kazi ndogo ya kuwakamata wachache wanaoendelea na vitendo hivyo.” Omari Mahita.
Dar es Salaam. Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) mstaafu, Omary Mahita amesema askari polisi kwa sasa wamepoteza hadhi, hawaogopwi na wahalifu na ndiyo sababu kubwa ya kuongezeka kwa vitendo vya kihalifu kila kukicha.
Mahita aliyestaafu mwaka 2006, alisema mbali na kuongezeka kwa uhalifu, inafikia hatua wahalifu wanawaingilia polisi kwa kuvamia vituo vya polisi na kupora silaha ilhali zamani hakukuwa na matukio hayo.
Hata hivyo, IGP, Ernest Mangu amejibu kauli hiyo akisema: “Siwezi kutumia mbinu za Mahita kwa sababu alichokuwa anakabiliana nacho, kwa sasa hakipo.”
Kauli ya Mahita
Kauli ya Mahita imekuja miezi minane baada ya askari 10 kuuawa na bunduki zaidi ya 20 kuporwa katika matukio mbalimbali ya uvamizi wa polisi na vituo vya polisi.
Akizungumza na mwandishi wetu baada ya kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Mkurugenzi wa zamani wa Mamlaka ya Hali ya Hewa, Dk Mohamed Mhita, Oysterbay Dar es Salaam juzi, Mahita alisema: “Ili kupunguza vitendo vya kihalifu vinavyozidi kuongezeka kila kukicha, ni lazima askari warudishe hadhi yao ya kuogopwa na wahalifu popote walipo.
“Askari lazima atishe. Popote anapokuwapo wahalifu wajue kuwa kuna mtu hatari dhidi yao. Kama mhalifu atatiwa woga na uwepo wa polisi, uhalifu utapungua tu na hivyo kubakiwa na kazi ndogo ya kuwakamata wachache wanaoendelea na vitendo hivyo.”
Mahita alikosoa kitendo cha askari polisi kuwa wapole na kueleza kuwa hilo ni suala lisilotakiwa kabisa kufanywa ndani ya jeshi hilo na polisi... “Unambembelezaje mhalifu? Hawa ni watu wanaostahili kubanwa kwa kila namna ili kukomesha vitendo vyao katika jamii. Mhalifu yeyote akiachiwa, madhara yake ni makubwa katika jamii.”
Licha ya suala hilo, IGP huyo mstaafu alieleza umuhimu wa doria katika kudhibiti uhalifu wa kila siku ambao hupunguza amani miongoni mwa jamii na kuwafanya wananchi washindwe kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na ratiba waliyojiwekea.
Alitolea mfano wa vikundi vya uhalifu vilivyojitokea hivi karibuni kama ‘Panya Road’, ‘Mbwamwitu’ na ‘Libya’ kwamba vimekuwapo kutokana na kupungua kwa doria inayotakiwa ifanywe na jeshi hilo nchi nzima na hasa maeneo ya mijini.
“Enzi zangu doria ilipewa kipaumbele. Magari na pikipiki yalikuwa yanazunguka kote katika jiji hili na kwingineko mikoani karibu kila siku na walikuwa wanaogopeka… kwa sasa yapo lakini sidhani kama wanafanya kazi kama ilivyokuwa enzi zile,” alisema Mahita.
“Wahalifu walikuwa wanajua kuwa polisi wapo kazini muda wote. Lakini sasa hivi mambo hayo hayapewi uzito unaotakiwa ndiyo maana unaona kikundi kama Panya Road kinatingisha mji mkubwa kama huu (Dar es Salaam).
“Inawezekana vipi kikundi kama hicho kikatingisha amani ya jiji hili lenye viongozi wote wa jeshi?” alihoji Mahita.
Mahita alikuwa maarufu kwa jina la ‘Ngunguri’ kutokana na kauli yake alipokuwa akikabiliana na maandamano ya wafuasi wa CUF kwamba kama viongozi wake wako ngangari basi polisi iko ngunguri kukabiliana nao.
Akizungumzia uhalifu katika vituo vya polisi, Mahita alisema polisi imekosa kuungwa mkono hivyo kupunguza ufanisi wake katika kutekeleza majukumu yake.
“Hata jamii ipo mbali pia… Raia ndiyo wanavamia na kuua askari. Watu hawa wanaishi katika jamii hiihii. Hivyo ni vyema ikajirudi na kuona kuwa hii ni taasisi muhimu kwa maisha na mali ya kila mwananchi.”
Akizungumzia vifo vya askari hao, Mahita alisema kuwa jamii imewasahau na kuwatenga kwani hakuna anayeshtuka pindi wanapoteza maisha hata kama mauti hayo huwakuta wakiwa kazini.
IGP Mangu
Akizungumzia hoja hizo, Mangu alisema mabadiliko ya jamii na maendeleo ya kiuchumi yamebadili mbinu za uhalifu.
“Mbinu za kiuhalifu zimebadilika kiasi cha kulilazimu jeshi pia kubadilika ili kuendana na mbinu hizo mpya. Haiwezekani jeshi likabaki kama ilivyokuwa miaka 20 iliyopita.
“Jamii ya wakati wa Mahita ni tofauti na ya sasa. Hata askari hawawezi kuendelea kuwa wale waliokuwapo. Mazingira na kila kitu vimebadilika. Enzi hizo kulikuwa na uhalifu wa ulipuaji wa mabomu na utakumbuka ilishatokea huko Arusha na Zanzibar matukio ambayo hayapo kwa sasa,” alisema Mangu. Alisema ni vigumu kulinganisha vipindi tofauti vya viongozi na kwamba kufanya hivyo ni sawa na kutowatendea haki kwani wanakuwa wanaongoza katika mazingira tofauti kwa kila kitu.
“Kubadilika kwa mbinu na aina za uhalifu kunamlazimu kiongozi husika kuitikia mabadiliko hayo pia. Mimi siwezi kutumia mbinu za Mahita kwa sababu alichokuwa anakabiliana nacho hakipo sasa hivi.
Hapakuwa na mauaji ya albino wakati wake, hili peke yake linaonyesha jamii iliyopo ni tofauti na iliyokuwapo,” alisema.
“Hata mimi nikistaafu baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba atakayekuja atapata changamoto tofauti na hizi ninazokutana nazo au walizokutana nazo watangulizi wangu,” alisema.“Rais Kikwete alikemea mauaji ya polisi kila yanapofanywa... hivi ndivyo tunavyotakiwa kufanya,” alisema Mangu.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment