JESHI LA POLISI TANZANIA LAMNG'ANG'ANIA ASKOFU WA KANISA LA UFUFUO NA UZIMA JOSEPHAT GWAJIMA, HAKUNA PA KUTOKEA !.
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima (kushoto) na Mchungaji Ngwandu Mwangasa wakitoka katika Kituo Kikuu cha Polisi, jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Wakili wa Askofu Gwajima, John Mallya. Picha na Venance Nestory.
Dar es Salaam. Sasa ni dhahiri kwamba polisi wamemshika pabaya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima baada ya kumhoji na kisha kumtaka arejee katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam Aprili 16, mwaka huu akiwa na vitu 10 vinavyohusu usajili, umiliki, uongozi na mali za kanisa analoliongoza.
Hatua hiyo imekuja kinyume na matarajio yake na ya wengi kuwa kiongozi huyo angekuwa anahojiwa tu kuhusu matamshi yake ya kashfa dhidi ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Kutokana na matamshi hayo yaliyosambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii kwa njia ya video na sauti, Gwajima alitakiwa kuripoti polisi kuhojiwa Machi 27, mwaka huu lakini kabla ya mahojiano yao kukamilika aliishiwa nguvu na kupelekwa hospitalini alikolazwa kwa siku nne, huku taarifa zikieleza kuwa alishtushwa na kuhojiwa taarifa binafsi badala ya tuhuma alizoitiwa polisi.
Hata baada ya kutoka hospitalini, Gwajima aliendelea kutembea akiwa kwenye kiti chenye magurudumu, alichotumia hadi Aprili 6 alipohubiri katika Ibada ya Pasaka.
Siku iliyofuata askofu huyo alitupa kiti hicho akidai kuwa amepona baada ya maombi ya wachungaji wageni waliofika kanisani hapo kutoka Japan.
Baada ya mahojiano ya jana, wakili wake, John Mallya alilalamikia hatua ya polisi akisema mahojiano kuchukua mkondo wa mambo binafsi badala ya kile alichoitiwa na kusema watakwenda kulalamikia hatua hiyo mahakamani.
Mambo 10
Wakili huyo alitaja mambo yanayotakiwa kuwasilishwa polisi kuwa ni hati ya usajili wa kanisa, namba ya usajili, majina ya Baraza la Wadhamini (Baraza la Kiroho), idadi ya makanisa (matawi) anayohudumia, nyaraka za helikopta ya kanisa, muundo wa uongozi wa kanisa, waraka wa maaskofu uliosomwa makanisa yote, nyaraka za nyumba na mali za kanisa, nyaraka kuonyesha taarifa za hesabu kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Hiari na kuambatana na mtu anayepiga picha za video kanisani hapo.
Mallya alisema watalalamika suala hilo litakapofika mahakamani kutokana na mteja wake kuhojiwa masuala tofauti na kile kinachodaiwa kutoa lugha ya matusi.
Alisema mteja wake amehojiwa muda mrefu kwa sababu alikuwa akihojiwa masuala binafsi yakiwamo ya familia yake, watoto wake, ndugu zake hadi waliokufa.
“Mahojiano yamekuwa ya muda mrefu, cha kushangaza kaulizwa maswali binafsi badala ya kile anachodaiwa kukifanya, mahakamani tutahoji hilo,” alisema Mallya.
Alisema licha ya kuambiwa walete vitu hivyo ambavyo kimsingi vipo, hawajaambiwa watafanywa nini kama wasipoviwasilisha.
Ilivyokuwa
Saa 1.15 asubuhi akiwa ameongozana na watu wawili akiwamo msaidizi wake ambaye alikuwa amemshikilia kutokana na kutembea kwa kupepesuka na wakili wake Malya, Gwajima alionekana akikunja uso kila alipopandisha ngazi moja kwenda nyingine kuelekea ndani ya Kituo Kikuu cha Polisi.
Baada ya kukaa ndani hadi saa 6.45 mchana, Gwajima alitoka akiwa ameshikiliwa kama alivyoingia na kuzungumza na waandishi wa habari na kusema mahojiano yalikwenda vizuri kuliko walivyotarajia, huku akimtaka wakili wake kufafanua zaidi, ndipo wakili huyo alipotaja mambo hayo.
Katika eneo la polisi, wafuasi wa Gwajima walikuwa katika makundi na ilipofika saa 1.40 asubuhi, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Simon Sirro aliwaita wapatao 20 miongoni mwao na kuwaliza wanachotaka, nao wakamjibu bila hofu kuwa wamemfuata baba yao.
Sirro aliwataka waumini hao waondoke akiwaeleza kuwa baba yao yupo katika mikono salama na wao waende wakafanye kazi za kutafuta mkate wa siku.
Hata hivyo, waumini hao walimjibu kuwa hawaondoki hadi baba yao atakapotoka na wao ndipo watakapoondoka.” Majibu yaliyomuacha hoi na kumfanya kucheza na kisha kuondoka kurejea ofisini kwake huku akisema... “Makubwa.”
Waumini hao walikuwa wakiongezeka kadri muda ulivyokwenda na hadi saa tano walikuwa wengi katika makundi wakiwamo walinzi shirikishi ambao walipata mafunzo kwa ufadhili wa Gwajima, ambao walikuwa wamejipanga langoni mwa kituo hicho wakiwa watulivu.
Waumini wazungumza
Wakizungumza kituoni hapo, waumini hao walisema wamepita mapito mengi na kiongozi huyo hivyo ni vigumu kumuacha peke yake katika eneo ambalo alipata matatizo mara ya kwanza.
Mmoja wao, Eugen Mkwasa alisema hajakwenda katika biashara zake kwa sababu ya kulinda usalama wa baba yao, kwa kuwa hana imani na eneo alilokuwapo kwani ndilo lililokuwa chanzo cha mateso yake ya sasa.
“Askofu wetu mpendwa anaumwa, hali hiyo ilimuanza akiwa hapa kituoni, nitakuwa na raha gani kubaki nyumbani au kwenda kibaruani bila kufahamu kama baba ametoka salama?” alisema Mkwasa.
Muumini mwingine, Elizabeth Peter alisema hajali jua na hata ikinyesha mvua kwa sababu analipa kile anachotendewa na Askofu Gwajima... “Askofu tumepita naye katika mapito mengi, siwezi kukaa mbali na suala lake kwa sababu ana mchango mkubwa maishani mwangu, siwezi kumtupa wakati huu mgumu wa kusumbuliwa na Jeshi la Polisi.”MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment