BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KUNDI LA KIGAIDI LA AL SHABAAB YAFANYA SHAMBULIZI NA KUUA WATU 147.


Wanajeshi wa Kenya wakilinda lango la kuingilia hospitali jana ambako wanatibiwa majeruhi wa shambulio la Al Shabaab juzi kwenye kampasi ya Chuo Kikuu cha Garissa.

Idadi ya vifo kutokana na shambulizi la wanamgambo wa Kisomali kwenye kampasi ya Chuo Kikuu cha Garissa, nchini Kenya, kilomita takriban 200 (maili 120) kutoka mpaka na Somalia imefikia 147.

Hata hivyo, imeelezwa kuwa upo uwezekano mkubwa kwa idadi hiyo kuwa kubwa zaidi, kwa mujibu wa chanzo kimoja serikalini na vyombo vya habari jana, huku wananchi wakiwa na hasira juu ya serikali kushindwa kuzuia umwagikaji wa damu.

Taarifa zinaeleza kuwa wakati wakivamia kampasi ya chuo hicho, walikuwa wamejifunga milipuko kwenye miili yao na silaha huku wakiwa wameficha nyuso zao.

Huku wakirusha maguruneti na kumimina risasi dhidi ya wanafunzi waliokuwa wamejawa na hofu, washambuliaji hao mwanzoni waliua bila kuchagua.
Lakini baadaye waliwaachia baadhi ya Waislamu na badala yake kuwalenga wanafunzi Wakristo wakati wa sakata hilo ambalo lilidumu kwa saa takriban 15.

ONYO LA SHAMBULIO
Hasira dhidi ya mauaji hayo ziliongezeka kutokana na ukweli kwamba lilitolewa onyo wiki iliyopita kwamba ulikuwepo uwezekano mkubwa wa kutokea shambulizi kwenye chuo kikuu kimoja nchini humo.

Wananchi wanashutumu mamlaka kwa kupuuzia kuboresha usalama kwenye eneo hilo lenye maendeleo kidogo sana.

"Ni kwa sababu ya serikali kupuuzia ndiyo maana mambo haya yanatokea. Kwa kitu kama hiki kutokea wakati ulikuwepo na uvumi ni kitu kisichokubalika," alisema Mohamed Salat, (47), mfanyabiashara wa Kenya mwenye asili ya Kisomali.

Maofisa walisema watu takriban 150 walikufa, huku kwa uchache 79 wakiwa wamejeruhiwa, wengi wao vibaya sana. Lakini bado kuna wanafunzi na wafanyakazi ambao hawajulikani walipo, na hivyo idadi ya waliokufa inaweza kuongezeka.

"Ndiyo, kuna uwezekano mkubwa wa idadi kuongezeka," kilisema chanzo kimoja cha serikali kinachoshughulikia shambulizi hilo la Garissa.
Gazeti linaloongoza kwa mauzo nchini Kenya, Daily Nation, likinukuu vyanzo, lilisema idadi ya vifo inaweza kufikia kuwa ya juu sana.

BADO WALIO HAI?
Nje ya milango ya chuo kikuu hicho, kundi la wanawake waliojifunga vitambaa walikuwa bado na matumaini kwamba watu ambao hawajulikani walipo wanaweza kuibuka wakiwa hai.

"Tunasubiri habari kama tunaweza kuwapata, wakiwa hai au wamekufa," alisema Barey Bare, 36, akimaanisha binamu yake aliyekuwa akifanyakazi kama karani kwenye chuo kikuu hicho na amekuwa hajulikani alipo tangu juzi.

Mauaji hayo yatamuongezea shinikizo Rais Uhuru Kenyatta, ambaye amekuwa akihaha kuzuia mashambulizi ya mara kwa mara ya risasi na maguruneti ambayo yamechafua taswira ya Kenya nchi za nje na kuiyumbisha kabisa sekta yake muhimu ya utalii.

WATU ZAIDI YA 400 WAMESHAUAWA
Watu zaidi ya 400 wameshauliwa na kundi hilo linalofungamana na al Qaeda la Al Shabaab kwenye taifa hilo la Mashariki mwa Afrika, tangu Kenyatta alipoingia madarakani Aprili 2013, wakiwamo watu 67 waliouawa Septemba mwaka huo huo kwenye shambulizi jengo moja la maduka mjini Nairobi.

Kundi la al Qaeda lenyewe liliua watu taktiban 207 wakati lilipolipua ubalozi wa Marekani mjini Nairobi mwaka 1998.

Kundi la Al Shabaab linasema wimbi lake la hivi karibuni la mashambulizi, ni kulipiza kisasi kwa Kenya kupeleka wanajeshi wake nchini Somalia kupambana na kundi hilo.

Saa chache baada ya shambulizi hilo, Kenya iliweka dau la shilingi milioni 20 (dola za Kimarekani 215,000) kwa kukamatwa kwa Mohamed Mohamud, mwalimu wa zamani wa Garissa anayeelezewa kuwa "Mtu anayetafutwa zaidi" kwenye tangazo moja la serikali na kuhusishwa na vyombo vya habari vya Kenya kwenye mashambulizi mawili tofauti ya al Shabaab eneo la jirani la Mandera mwaka jana.

Serikali pia ilitangaza amri ya watu kutotoka nje kuanzia jioni hadi asubuhi huko Garissa, Mandera na maeneo mengine mawili ambayo yamekuwa yakikumbwa sana na matukio ya kihalifu kwenye mpaka wa Somalia.

Wachambuzi na wanadiplomasia wanasema vyombo vya usalama vya Kenya bado havifanyi kazi kwa pamoja. Maswali yamekuwa yakiibuliwa na vyombo vya habari juu ya ni vipi watu wanne wenye silaha waliweza kupambana kwa saa kadhaa na mamia ya watu wa usalama, wakiwamo wanajeshi na polisi wa vikosi maalumu.

Mwanadiplomasia mmoja wa Magharibi alisema Kenya, mshirika mkubwa wa magharibi katika mapambano dhidi ya Uislamu wa itikadi kali, inaendelea kupokea msaada zikiwamo habari kutoka mashirika ya intelijinsia ya Magharibi lakini inahaha kuzifanyia kazi. CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: