BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MWANAFUNZI WA KIDATO CHA PILI AUAWA BAADA YA KUFUMWA NA BARUA YA MAPENZI ILIYOANDIKWA NA RAFIKI WAKE WA KIKE MKOANI RUKWA.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa , Jacob Mwaruanda
MWANAFUNZI wa Kidato cha Pili, Jofrey Robert Mwakatenya (15) anatuhumiwa kuuawa kikatili na baba yake mzazi, Robert Mwakatenya (35) baada ya kumkuta akiwa na barua ya mapenzi, inayodaiwa aliandikiwa na rafiki wake wa kike.


Mzazi huyo ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa eneo la Majengo ‘D’ Manispaa ya Sumbawanga, anadaiwa kumwadhibu mwanafunzi huyo, ambaye ni mtoto wake wa kwanza kwa kupiga ngumi na mateke mfululizo kwa zaidi ya saa tatu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa , Jacob Mwaruanda alithibitisha tukio hilo, lilitokea usiku wa kuamkia Jumapili iliyopita. Alisema bado wanamtafuta mtuhumiwa huyo kwani baada ya kufanya kitendo hicho alitokomea.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mwenyekiti wa Serikali Majengo D, Antony Nyambo alidai kuwa mzazi huyo alikuwa na tabia ya kumwadhibu mwanawe huyo, akimtuhumu kuwa ni mtoro wa shule .

“Nilitaarifiwa juu ya kisa hiki Jumapili saa mbili asubuhi baada ya kutoka katika ibada na raia mwema, ndipo niliamua kufika nyumbani kwa marehemu, nilimkuta akiwa amelazwa chumbani, nilipomfunua niliona akiwa ametapakaa vumbi mwili mzima huku akiwa amevaa nguo ya ndani tu,” alidai mwenyekiti huyo wa mtaa.

Inadaiwa kuwa usiku huo wa tukio, mtuhumiwa alianza kumwadhibu kumpiga ngumi na mateke kuanzia saa mbili usiku hadi usiku wa manane.

Mtoto huyo baada ya kupata kipigo hicho, alizimia ambapo baba yake alimwagia maji mwilini hadi akazinduka, kisha akamwamuru alale chumbani humo pamoja na mdogo wake.

Mzazi wa mtoto huyo alidamka alfajiri na kwenda kwenye chumba walicholala watoto hao na kugundua kuwa Jofrey alikuwa mfu.

“Ndipo baba huyo alipoaga nyumbani hapo, akidai kuwa anaenda kutafuta gari ili Jofrey aweze kupelekwa hospitalini kwa matibabu. Mzazi huyo hakurudi tena nyumbani kwake hadi sasa,” alibainisha.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: