BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SERIKALI YATANGAZA BAJETI YA MWAKA 2015/2016 LAKINI FEDHA NYINGI ZIMETENGWA KWA AJILI YA POSHO ZA VIONGOZI NA MATUMIZI MENGINE.

http://www.ippmedia.com/media/picture/large/Saada%20Mkuya(2).jpg

Serikali imetangaza sura ya bajeti ya mwaka 2015/16, ikiwa imejielekeza zaidi katika matumizi ya kawaida ya safari, posho za viongozi na matumizi mengine kuliko miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya Watanzani moja kwa moja.


Bajeti ya mwaka ujao inatarajiwa kuwa Sh. Trilioni 22.480, kwa matumizi ya kawaida na maendeleo.

Makadirio hayo ni ongezeko la asilimia 13.2 ya bajeti ya mwaka 2014/15 ambayo ilikuwa ni Sh. Trilioni 19.853.

Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya, alisema jana jijini Dar es Salaam kwamba katika makisio hayo, miradi ya maendeleo imetengewa Sh. Trilioni tano. Fungu hilo ni pungufu kwa Sh. Trilioni moja ikilinganishwa na Sh. Trilioni sita za mwaka wa fedha unaomalizika.

Alifafanua kuwa Sh. trilioni 16.711 sawa na asilimia 74.3 ya bajeti yote ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida huku fedha za miradi ya maendeleo zikipungua kwa asilimia 10.49.

VIPAUMBELE
Mkuya akiwasilisha mapendekezo ya mfumo wa mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka 2015/16, alisema Bajeti hiyo itaweka vipaumbele katika kugharimia uchaguzi mkuu na kukamilisha miradi inayoendelea na kuweka msukumo maalum kwenye miradi ya umeme vijijini, maji vijijini na kuimarisha rasilimali watu.

Kati ya fedha hizo, Sh. trilioni 6.612 sawa na asilimia 39.6 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa serikali na taasisi na Sh. trilioni 2.600 sawa na asilimia 15.6 kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za serikali zitakazoiva.

Katika bajeti ya mwaka 2014/15 fungu la matumizi ya kawaida lilikuwa ni Sh. trilioni 13.402 wakati kwa mwaka ujao wa fedha imeongezeka kwa asilimia 24.7.

Pia, bajeti hiyo imeelekeza fedha kidunchu kwenye miradi ya maendeleo ambazo ni Sh. trilioni 5.769 sawa na asilimia 25.9 ya bajeti kuu, ikiwa inaonyesha kupungua kutoka Sh. trilioni 6.445 ya mwaka 2014/15.

KUPUNGUZA UTEGEMEZI
Aidha, sura hiyo imeonyesha utegemezi kwa washirika wa maendeleo ambao kwa mwaka huu watachangia bajeti kwa Sh. Trilioni 1.888 sawa na asilimia 8.4 ya bajeti, ikilinganishwa na mwaka 2014/15 ambayo ilikuwa ni asilimia 14.8 ya bajeti ambazo ni mikopo ya masharti nafuu.

Waziri Mkuya alisema mapato ya ndani kwa bajeti hiyo ni Sh. trilioni 14.824 sawa na asilimia 57.8 ya bajeti yote na kwamba serikali imelenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya Sh. trilioni 13.353 sawa na asilimia 90.1 ya mapato ya ndani.

Alisema mapato yasiyo ya kodi na mapato kutoka vyanzo vya halmashauri ni Sh. bilioni 949.2 na Sh. bilioni 521.9 kwa mtiririko huo na kwamba serikali imetenga kukopa kiasi cha Sh. trilioni 5.767 kutoka vyanzo vyenye masharti kibiashara.

“Bajeti ya mwaka 2015/16 ni ya kipekee. Ni mwaka wa uchaguzi mkuu, mwaka ambao serikali ya awamu ya nne inamaliza muda wake na serikali mpya inaingia madarakani. Ni mwaka ambao MKUKUTA na mpango wa kwanza wa maendeleo ya miaka mitano inafika tamati, mwaka ambao malengo ya millennia ya mwaka 2015 na vile vile utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 unakamilika,” alisema.

SHABAHA YA MISINGI YA BAJETI
Mkuya alisema shabaha ya uchumi ni kuongeza kasi ya ukuaji wa pato halisi la Taifa kufikia asilimia 7.2 mwaka 2015, kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja.

Pia, kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya halmashauri kufikia asilimia 15.7 ya pato la Taifa, kuongeza mapato yatokanayo na kodi kufikia asilimia 14.2 ya pato la Taifa na matumizi ya serikali yanatarajiwa kuwa asilimia 20.7 ya pato hilo.

Alisema mengine ni kupunguza nakisi ya bajeti hadi kufikia asilimia 3.6, kasi ya ukuaji wa ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi kuwa asilimia 16 mwezi Juni mwaka 2016, mikopo kwa sekta binafsi itakuwa kwa asilimia 19.5 ya pato la Taifa, kupunguza nakisi katika urari wa malipo ya nje ya kawaida unaojumuisha urari wa biashara ya bidhaa, huduma, mapato ya vitega uchumi na uhamisho mali wa kawaida kufikia asilimia 10.7. CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: