BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

VIONGOZI WASIFU STAILI YA UONGOZI WA SHEKHE ABEID AMAAN KARUME.

  

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein (wa pili kulia) na viongozi wengine wakiitikia dua iliyoombwa na Mufti wa Zanzibar, Shehe Saleh Omar Kabi (kulia) baada ya kisomo cha hitma, iliyosomwa jana katika ukumbi wa Ofisi ya CCM Kisiwandui mjini Unguja. (Picha na Ikulu).

VIONGOZI wa Serikali na kidini, wamesifu staili ya uongozi wa Shekhe Abeid Amaan Karume kwa uzalendo na kuweka mbele maslahi ya Taifa na kuwatumikia wananchi.


Walisema hayo jana mjini hapa katika Kisomo cha Hitima ya kumwombea dua Hayati Karume, kiongozi shupavu na Rais wa Kwanza wa Zanzibar aliyeuawa mwaka 1972 kwa kupigwa risasi, miaka minane tangu aanze kuiongoza Zanzibar.

Katika shughuli hiyo iliyofanyika katika kaburi la Hayati Karume, pembezoni mwa jengo la Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui alikofikwa na mauti Aprili 7 mwaka 1972, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein ndiye aliyewaongoza viongozi na wageni wengine, kwa kuweka shada la maua na kufuatiwa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Mohammed Gharib Bilal na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis Mwamunyange.

Familia ya Karume iliongozwa na mtoto wa pili wa marehemu, Balozi Ali Karume kuweka shada la maua na kufuatiwa na viongozi mbalimbali wa dini, akiwemo kiongozi wa dini ya Kihindu, Banguaji Siruanji.

Waasisi wa Mapinduzi waliofanya kazi bega kwa bega na Karume hadi Mapinduzi ya mwaka 1964, waliwakilishwa na Hamid Ameir katika kuweka shada la maua.

Na mara baada ya kisomo kilichoongozwa na Mufti, Shekhe Mkuu Saleh, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alizungumza na kuwataka viongozi wa sasa, kuiga mfano wa Karume wa kuwatumikia wananchi kwa kuweka mbele uzalendo na kuacha tabia ya kujilimbikizia mali na utajiri wa kutisha.

Alisema leo hii taifa linamkumbuka Mzee Karume, kutokana na mchango wake mkubwa katika kuwatumikia wananchi na kuweka mbele maslahi ya taifa na wananchi wake.

Alitoa mfano kuwa licha ya kuongoza kwa miaka minane, aliyoyafanya ni kielelezo kikubwa kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla huku wakiwa na kila sababu ya kumuenzi kwa vitendo.

“Viongozi wa sasa wa Tanzania tunatakiwa kumuiga Karume katika kufanya kazi na kuwatumikia wananchi kwa uzalendo wa hali ya juu na sio kujilimbikizia mali na kutafuta umaarufu wa kuchuma mali kupindukia,” alisema.

Alisema uzalendo wa Karume ni mfano katika Bara la Afrika, ambalo limewahi kutoa viongozi wa aina hiyo waliokuwa wakitaka kuona umoja wa Afrika unadumishwa kwa nguvu zote.

Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum akitoa mawaidha yake alimwelezea Karume kama kielelezo cha kiongozi shujaa, aliyefanya kazi zake kwa muda wote wa maisha yake kuwatumia wananchi kwa maslahi ya taifa.

“Tunapaswa kumkumbuka kiongozi shujaa wa taifa hili Mzee Abeid Amaan Karume kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa maslahi ya wananchi wa Zanzibar na kuona wanapiga hatua kubwa ya maendeleo,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu wa Mufti, Shekhe Fadhil Soraga alisema uaminifu katika uongozi ni hekima kubwa, ambayo viongozi wanatakiwa kuzingatia katika kipindi chote cha kuongoza wananchi.

“Uongozi ni dhamana ya kuwatumikia wananchi kwa hivyo uaminifu na utii ni mambo muhimu yanayofanikisha utumishi wa umma kwa taifa,” alisema Soraga.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi na Utumishi wa Umma), Haroun Ali Suleiman alisema Karume alipata sifa na umaarufu, kutokana na uwezo wake wa kufanya kazi na kuweka mbele uadilifu wa hali ya juu katika kuwatumikia wananchi.

“Nyumba zote unaziona leo, zile za Michenzani pamoja na vijijini za ghorofa ikiwemo katika jimbo langu la Makunduchi, zimejengwa na yeye bila ya fedha za wafadhili,” alisema.

Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni, Masauni Yussuf Masauni aliwataka vijana kusoma historia ambayo watapata faida mbali mbali kuhusu mambo yaliyofanywa na hayati Karume kwa wananchi wa Zanzibar.

Mtoto wa marehemu, Balozi Ali Karume alisema siku ya Karume inawakumbusha Wazanzibari kwa kupoteza kiongozi hodari shujaa, ambaye alikuwa na uchungu wa Zanzibar.

Juzi, katika mahojiano na gazeti hili yaliyochapishwa toleo la jana ikiwa ni moja ya habari maalumu za Kumbukumbu ya Siku ya Karume, Ameir alisema miongoni mwa siri za mafanikio ya Karume ni nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, jambo alilohimiza viongozi walio madarakani kumuiga kwa kufanya kazi kwa bidii na kuweka mbele maslahi ya taifa na wananchi kwa ujumla.

Alisema Karume aliacha somo kubwa kwa viongozi kufanya kazi kwa kujituma, kuweka mbele uaminifu wa hali ya juu na kupambana na ubadhirifu wa mali ya umma.

Kuhusu utajiri wa Karume, Ameir alisema hadi anauawa mwaka 1972, baada ya kuongoza Zanzibar kwa miaka minane, alikuwa na nyumba mbili alizojenga mwenyewe bila ya kujilimbikizia maeneo ya ardhi.

“Sisi wajumbe wa timu ya watu 14, Karume alikuwa sawa na rafiki yetu. Tulikuwa tukimfahamu vizuri, hakupenda kujilimbikizia mali wala tamaa ya kujenga nyumba na kukusanya viwanja...kama alitaka kufanya hivyo, nafasi alikuwa nayo kubwa,” alisema.

Alisema katika kipindi cha miaka minane, hakuna matukio ya ubadhirifu wa mali aliyopata kuyasikia kutoka kwa viongozi waliokuwa madarakani. Pia alisema, suala la rushwa lilidhibitiwa kwa kiwango kikubwa.

Alitoa mfano wa nyumba za ghorofa Michenzani mjini Unguja na zilizoko vijijini, kwamba zilijengwa kwa kutumia fedha za ndani zinazotokana na mauzo ya karafuu.

“Siri kubwa ya Karume inatokana na uwezo wake mkubwa wa kudhibiti na kutunza hazina ya fedha kwa ajili ya matumizi yaliyotengwa ambayo yanatokana na makubaliano,” alisema.

Kutokana na heshima kubwa ya mwasisi huyo wa taifa la Zanzibar, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema iko katika mchakato wa kumtangaza hayati Karume kuwa Baba wa Taifa la Zanzibar, kutokana na mchango wake mkubwa wa maendeleo na kuimarisha huduma za kijamii.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalumu za Serikali (SMZ), Haji Omar Kheir alisema hivi karibuni katika kikao cha Baraza la Wawakilishi wakati wajumbe wakijadili kamati za Baraza ikiwemo ya viongozi wakuu wa Serikali.

Kheir alisema mchango wa Karume ni mkubwa zaidi katika kuimarisha hali za wananchi za kuwapatia makazi bora ya kisasa.

Askofu akemea ufisadi
Wakati wengi wakielezea kuguswa na uadilifu wa Karume na kulaani tabia ya viongozi kujilimbikizia mali, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Nchini, Dk Jacob Chimeledya pia ameonya dhidi ya tabia ya kujilimbikizia mali, inayofanywa na viongozi na kusema hali hiyo inahatarisha amani ya taifa.

Askofu huyo alisema hayo kwenye mahubiri ya Pasaka katika ibada iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Watakatifu Wote, Ving’hawe mjini Mpwapwa.

Alisema vitendo vya kujilimbikizia mali vinasababisha ubinafsi, kupungua kwa uadilifu, taifa kuzingirwa na vitendo vya rushwa na kutengeneza kundi kubwa la walionacho na wasionacho.

Alisema vitendo vya ufisadi, vinavyofanywa na baadhi ya viongozi vinasababisha watanzania wanyonge, kuteseka kwa kukosa dawa hospitalini, akina mama kufa kwa kukosa vifaa vya kujifungulia, na watoto shuleni kukosa vifaa vya kutosha huku mtanzania mmoja anamiliki pesa ambazo zinaweza kupunguza matatizo hayo.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: