BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

CHADEMA YAUNGA MKONO MGOMO WA MADEREVA, MGOMBEA URAIS KUPATIKA AGOSTI 4, ATAYEINGIA CHUNGU CHA UKAWA..


Viongozi wa Chadema wakiomba dua kabla ya kuanza kwa kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kilichofanyika Dar es Salaam jana. Kuanzia kulia ni Makamu Mwenyekiti, Profesa Abdallah Safari, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu Dk Willibrod Slaa na Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu. Picha na Venance Nestory


Dar es Salaam.
Kamati Kuu ya Chadema imepanga Agosti 4 kuwa siku ya kumpata mgombea wake wa urais ambaye ataingia kwenye kinyang’anyiro cha kumtafuta mgombea wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).


Vyama vinne vilivyounda Ukawa, Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, vimekubaliana kusimamisha mgombea mmoja wa kuanzia ngazi ya urais, lakini kila chama kitateua mgombea wake kabla ya kukubaliana mtu atakayeungwa mkono na vyama vyote.


Ratiba iliyotolewa jana na Chadema inaonyesha kuwa chama hicho kitatumia siku 76, kuanzia Mei 18, kumaliza mchakato wa kuwapata wagombea wake wa nafasi za udiwani, ubunge na urais kwa kuhitimisha na Mkutano Mkuu. Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Chadema itampata mgombea wake wa urais takriban siku 14 zaidi kulinganisha na mwaka 2010 wakati Dk Willibrod Slaa alipoteuliwa.


Kwa mujibu wa Ibara ya 7.710 (C) ya katiba ya Chadema, Mkutano Mkuu ndiyo chombo chenye mamlaka ya kumpitisha mgombea wa urais kwa tiketi ya chama hicho.


Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwaambia wanahabari jana kuwa kamati hiyo imeridhia mchakato wa uchukuaji na urejeshaji fomu uanze ili watia nia katika maeneo mbalimbali waanze kuchukua fomu za udiwani, uwakilishi na ubunge.


Katika ratiba hiyo , chama hicho kimeyapa kipaumbele maeneo yanayoonekana kutokuwa na madiwani na wabunge, kuanza kuchukua fomu siku ya kwanza ya kazi hiyo na kuzirudisha Juni 25.


Aidha ratiba hiyo inaonyesha kuwa makada waliopo kwenye maeneo yenye madiwani watachukua na kurejesha fomu ndani ya siku 10 kuanzia Julai Mosi.


Wakati huo, maeneo yenye wabunge kwa sasa yakipatiwa siku tano za kukamilisha uchukuaji na urejeshaji wa fomu hizo kuanzia Julai 6 hadi 10 huku vigogo wanaounyemelea urais wakipigiwa kipenga Julai 20 hadi 25.


Mara baada ya wagombea urais kukamilisha taratibu za kinyang’anyiro, Chadema imepanga kufanya uteuzi wa mwisho wa wagombea ubunge Agosti 1 na 2 huku Baraza Kuu likipangwa kukutana siku inayofuata kabla ya Mkutano Mkuu kukutana Agosti, 4.


Chadema imeungana na CUF kutangaza ratiba ya kuwapata wanachama watakaowania uongozi katika Uchaguzi Mkuu ambao kikatiba unatakiwa ufanyike wiki ya mwisho ya Oktoba na kubakiza mchakato wa kumpata mgombea mmoja kila nafasi ya uongozi.


Akielezea zaidi yaliyojiri katika vikao vya kawaida vilivyofanyika Mei 3 na 4 mwaka huu, Mbowe alisema Kamati Kuu ilipokea na kujadili makubaliano yaliyofikiwa ndani ya Ukawa.


Mbowe, ambaye pia ni mbunge wa Hai, alisema kuwa kamati hiyo iliwapongeza viongozi hao kwa hatua walizofikia na kuwataka wamalize masuala machache yaliyosalia ili wawajulishe Watanzania wanaounga mkono umoja huo wajue kinachoendelea.


Ukawa wameshakubaliana kwa asilimia 95 masuala mbalimbali, hususan kuachiana majimbo kwa kuzingatia nguvu ya chama katika eneo husika, huku wakibakiza majimbo 12 yenye utata.


Dk Slaa, ambaye ni katibu mkuu wa Chadema, alisema watafanikiwa kumaliza mgogoro wa kuachiana maeneo yenye utata salama huku akiwananga wanaowaombea mabaya.


Alisema kuna manabii wa uongo wanaotabiri kuwa Ukawa itaparaganyika kwa kushindwa kuafikiana katika kuachiana maeneo tata, watashindwa kwa kuwa “ngoma ya Ukawa, CCM haitaiweza”.


“Kama tumeweza kumaliza asilimia 95 tutashindwaje kumaliza asilimia tano? Kuna maeneo ambayo hatutaweza kuafikiana hadi siku mbili tukamilishe mchakato, lakini tutamalizana na safari hii lazima CCM itang’oka,” alisema Dk Slaa.


Dk Slaa alisema watu wameng’ang’ania tu kuachiana majimbo huku wakisahau kuna madiwani zaidi ya 4,800 ambao nao wanatakiwa kuafikiana na kubainisha kuwa masuala yote hayo wanaendelea kuyajadili.


Kamati Kuu ya Chadema ilijadili pia mwenendo wa uandikishaji wa wapigakura kwa kutumia teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR) na kujiridhisha kuwa hadi sasa hakuna dhamira ya dhati ya kisiasa wala maandalizi ya kutosha yakiwemo matakwa ya kisheria, kitaalamu na kibajeti kuwezesha zoezi hilo kwa mujibu wa Katiba.


Kuhusu Uchaguzi Mkuu, Mbowe alisema kamati imeazimia lazima ufanyike mwezi Oktoba kwa mujibu wa Katiba na Serikali ya CCM isijiandae kutumia kisingizio chochote kuahirisha kwa sababu uchaguzi si jambo la dharura kwa kuwa lilishajulikana miaka mitano iliyopita.


“Aidha Kamati imeitaka Serikali ya CCM chini ya Rais Jakaya Kikwete kuacha hila zozote za kutaka kujiongezea muda wa kukaa madarakani, ikiwamo kutaka kupeleka ‘Muswada wa Marekebisho ya Katiba’ bungeni ili kujihalalishia kuongeza uhai wa Serikali,” alisema Mbowe.


Akielezea zaidi wasiwasi kuahirishwa Uchaguzi Mkuu, Dk Slaa alisema mpaka sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haijatangaza zabuni yoyote ya kununua vifaa mbalimbali vya uchaguzi, zaidi ya kutangaza manunuzi ya vifaa vya Kura ya Maoni ambavyo siyo kipaumbele kwa sasa.


Alisema utaratibu wa zabuni za ndani unaonyesha kuwa huchukua miezi tisa kukamilika wakati zile za nje huchukua hadi miezi 18 kukamilika, hivyo kuwapo kwa viashiria vya wazi kuwa bila kukimbizana na muda, uchaguzi utaahirishwa kwa sababu imesalia miezi mitatu tu.


Hata hivyo, mkuu wa Idara ya Elimu ya Mpiga Kura na Habari wa NEC, Ruth Masham alisema kwa sasa wamejikita zaidi kuandikisha wapigakura huku akibainisha kuwa ratiba ya uchaguzi itatolewa baadaye.


“Kwa sasa tunashughulikia uboreshaji Daftari la Wapigakura kwa sababu pia kuna Kura ya Maoni hivyo kwa sasa hatuwezi kuzungumzia ratiba. Mtuvumilie tutatangaza aidha baada ya kukamilisha daftari au kabla na taarifa tutawapatia,” alisema Masham.


Chadema yaunga mkono mgomo wa madereva.
Mbowe alisema kuwa kamati hiyo ilipokea na kujadili sekta ya uchukuzi na kubaini kuwa kuna udhaifu mkubwa wa uongozi na kusababisha kukosa mwelekeo.


Alisema kamati hiyo pia imebaini athari mbalimbali za mgomo wa madereva kwa wagonjwa, wanafunzi wa kidato cha sita kuathirika kiuchumi na kisaikolojia.


“Baada ya tafakuri ya kina, Kamati Kuu imeazimia kuunga mkono madai ya madereva kwani ni halali na hivyo ni lazima serikali iyatekeleze kwa sababu kuendelea kuyapuuza madai hayo ni kuuendelea kuhatarisha maisha ya abiria wanaosafiri mara kwa mara,” alisema.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: