Mabasi yakianza kuondoka katika Kituo Kikuu Ubungo, Dar es Salaam jana kuelekea mikoani baada ya madereva kusitisha mgomo wao.
HUDUMA za usafiri wa mabasi ya mikoani na daladala, zilizokuwa zimekwama kwa saa 31 kuanzia alfajiri ya juzi, zilirejea jana mchana.
Zilirejea baada ya madereva kusitisha mgomo wao, kutokana na ushawishi wa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda aliyezungumza nao.
Makonda pia alijitwisha mzigo wa kufuatilia madai ya madereva hao katika kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ili kuona hadidu za rejea za kamati hiyo na muda wa kamati hiyo kufanya kazi.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kwa kuwa kamati husika iliyoundwa, ina hadidu za rejea hivyo ni vyema kuzihakiki kuona kama suala la mkataba, malipo, matibabu na suala la kusoma, limo ndani ya hoja husika na kuhakiki muda husika wa Kamati kufanya kazi.
Maafikiano hayo yalitokana na kuwepo kwa mazungumzo ya muda mrefu baina ya viongozi wa madereva na wamiliki, huku Makonda na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohammed Mpinga wakisimamia mazungumzo hayo.
Hata hivyo, madereva hao na mkuu huyo wa wilaya walikubaliana kuwa kazi hiyo isipokamilika kuanzia leo saa 4:00 asubuhi, wataendeleza mgomo huo, ambao umesababisha athari kubwa kiuchumi kwa taifa.
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe alikuwa sehemu ya mazungumzo hayo, aliyokuta yameshaanza na baadaye viongozi wa madereva kuingia makubaliano na kusaini na viongozi wa serikali.
Katika muda wote wa mazungumzo hayo, kadhia mbalimbali zilijitokeza ikiwa ni kupigwa kwa mawe kwa viongozi hao na polisi baada ya askari kuwatawanya maelfu ya raia kwa mbwa wa polisi, baada ya maelfu ya raia kuwazunguka viongozi hao.
Hata hivyo mapema asubuhi jana, mabasi sita ya mikoani yaliondoka kwa kusindikizwa na polisi huku baadhi ya abiria wakilalamika kukesha Ubungo na wengine kushushwa, kutokana na kuumwa wakipelekwa hospitalini kwa matibabu.
Kusitishwa mgomo
Mazungumzo ya kufikia tamati, yalianza saa 3:35 asubuhi kwa Makonda kuwafuata viongozi wa madereva, waliokuwa ndani ya Kituo Kikuu cha Mabasi ya mikoani Ubungo, kinachotumiwa na zaidi ya mabasi 600 kwa siku na kuanza kuzungumza nao nje na baadaye kuhamia ndani, zilipo ofisi za madereva hao.
Baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa takriban saa tatu kukumbwa na kelele nyingi kutoka kwa wananchi waliokuwa eneo hilo, hatimaye wahusika hao kwa pamoja walikubaliana kutoka nje na kufuata kilipo kipaza sauti ili kutangaza hadharani kuhusu makubaliano hayo.
Akizungumza na madereva hao, Makonda alisema wamekubaliana na kuweka saini na viongozi hao kuwa ifikapo leo saa 4 kama hadidu za rejea, majina na muda wa kufanya kazi kwa kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu hazitakuwa wazi, utekelezaji wa madai ya madereva hao, yeye peke yake (Makonda) atasimama kuendeleza mgomo.
“Tumekubaliana na kuweka saini na viongozi wa madereva hawa ili kwa pamoja tuende tukafuatilie majina ya wanakamati hiyo maana yawezekana wahusika hawamo, kuona hadidu za rejea na pia kujua kamati hiyo itafanya kazi kwa muda gani,” alisema Makonda katika umati huo uliokuwa na kila aina ya kelele za maelfu ya wananchi.
Alisema kama hakutakuwa na majibu katika kamati iliyoundwa juu ya madai ya madereva hao, hata wananchi wasikate tiketi na kuanzia sasa wanakwenda kupitia na kuhakiki na viongozi hao wa madereva waweze kutoa taarifa kwa wenzao.
Alisema wakati mwingine mgomo ni dawa na hoja za madereva hao ni za msingi na kwa vile kamati ya kushughulikia madai hayo imeundwa, wanahitaji kujua majina ya waliomo, kujua kama ni wahusika ambao wanaweza kutetea maslahi ya madereva na kama sio wengine waweze kuongezwa.
Waliokamatwa na Polisi
Makonda alitumia fursa hiyo kuitaka polisi kuwaachia huru wananchi 36 waliokamatwa katika maeneo mbalimbali nchini, kutokana na kuwepo kwa matukio kadha wa kadha kufuatia mgomo huo.
Aidha, baada ya Makonda kuzungumza aliondoka eneo la tukio na alisimama Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva nchini, Clement Masanja ambaye aliwataka madereva kuanza safari kwa kufuata sheria za barabarani kwa kuwa mwisho wa haki zao unafuatiliwa.
“Madereva twende kwa sheria za barabarani...twende kwa tahadhari, wale ambao kesho hawatokuwepo Dar es Salaam wenzao watawapa taarifa kuanzia kesho (leo),” alisema Masanja na kuongeza kuwa aliyoyasema Mkuu wa Wilaya asipoyatekeleza wataratibu mgomo mwingine kama huo.
Mabasi yasindikizwa na polisi
Jana asubuhi mapema kabla ya kumalizika kwa mgomo, yaliondoka mabasi ya mikoani sita yakitoa huduma za usafiri kwa abiria wao yakianza na mabasi mawili ya Kampuni ya Shabiby, matatu ya Dar Express na moja la Mohammed Trans.
Wananchi walishangilia baada ya kuanza kurejea kwa huduma za usafiri kwa kuwa mara baada ya kutia saini kwa madereva na Makonda, wengi walirejea katika vyombo vyao vya usafiri na kuanza kuwasha magari tayari kwa safari huku madereva wa daladala nao wakitoka kufuata vyombo vyao.
Magari hayo yaliondoka kwa kuongozana huku nje ya kituo cha Ubungo, wananchi wakiwashangilia kuonesha matumaini ya kuanza kwa huduma za usafiri.
Hii ni mara ya pili kwa mgomo wa madereva kutokea nchi nzima ndani ya mwaka huu, mara ya kwanza ikiwa Aprili 10 ambapo madereva waligoma kwa saa tisa na ulikoma baada ya serikali kuingilia kati na kuwasihi warejee kazini wakati madai yao yakishughulikiwa.HABARILEO
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment