JK KUSHUGHULIKIA KERO NA CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI SHEMEJI ZAKE KABLA YA KUNG'ATUKA KITI CHA URAIS.
AHADI ya Rais Jakaya Kikwete ya kushughulikia changamoto za walimu kabla ya kumaliza muda wa uongozi wake mwishoni mwa mwaka huu, inatarajiwa kuanza kutekelezwa mwezi ujao.
Tayari Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, limeelezwa kuwa zaidi ya walimu 80,000 watanufaika na malipo ya malimbikizo ya madeni mbalimbali yatakayofanyika mwisho mwa mwezi ujao.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Kassim Majaliwa alisema hayo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Karatu, Mchungaji Israel Natse (Chadema).
Alisema Serikali imeshalipa zaidi ya Sh bilioni 25 ya fedha katika madeni ya walimu yaliyohakikiwa na Sh bilioni tatu nyingine zitalipwa hadi kufikia Juni 30, mwaka huu, ambapo walimu 80,000 wanatarajiwa kulipwa stahiki zao katika malipo hayo.
Katika swali lake, Mchungaji Natse alitaka kufahamu idadi ya walimu walioguswa na mabadiliko ya madaraja katika jimbo analoongoza, wanadai kiasi gani na watalipwa lini.
Nyongeza Majaliwa alisema Serikali pia imeridhia na kutoa muundo mpya wa kada za walimu kuanzia Julai 2014, ambao umewezesha walimu waliokuwa wamefikia ukomo katika muundo wa zamani, kunufaika kwa kupata nyongeza ya ngazi ya muundo mpya kupitia bajeti ya mwaka 2015/2016.
Kuhusu madai ya walimu katika Jimbo la Karatu, Majaliwa alisema, “katika Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, mabadiliko haya yamewagusa walimu 295.
Alisema uchambuzi wa taarifa za walimu walioguswa na mabadiliko hayo, umebaini katika Halmashauri ya Wilaya ya Karatu walimu 295 wanadai Sh bilioni 1.09 ambazo walimu wataanza kulipwa mwaka 2015/2016.
“Pamoja na mabadiliko hayo, Serikali imeondoa utaratibu wa kuwataka watumishi kukubali vyeo kabla ya kuwarekebishia mishahara, hali ambayo imerahisisha kazi ya urekebishaji wa mishahara ya watumishi kwa pamoja. “Awali, mwalimu alikuwa anaandikiwa barua ya kupandishwa daraja na kutakiwa kukubali ndipo taratibu nyingine zianze.
Kwa sasa, mwalimu atapata barua na taratibu zikiwa zinaendelea,” alifafanua Naibu Waziri. Aidha alisema kwa sasa halmashauri zimeagizwa kutohamisha watumishi kama hawana fedha, labla kama ni kwa kuwianisha ikama.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM) aliomba Mwongozo wa Spika akihoji kuwa wapo walimu wapya wilayani Kwimba hawajapewa posho zao tangu waripoti mwanzoni mwa mwezi huu, na kutaka kusikia kauli ya Serikali juu ya hilo.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema hilo linashughulikiwa na Tamisemi, na maagizo yalikuwa ni walimu wote hao zaidi ya 31,000 nchini kulipwa wanapofika vituoni mwao bila upungufu wowote.
Hivi karibuni Rais Kikwete alisema atahakikisha anamaliza matatizo yote yanayowakabili walimu kote nchini katika kipindi kilichobaki cha utawala wake. Alitoa ahadi hiyo wakati alipozungumza na walimu wapatao 1,500 kutoka wilaya 153 na mikoa yote ya Tanzania Bara, pamoja na wawakilishi kutoka Visiwani.
Akizungumza kwa hisia katika mkutano huo wilayani Arumeru mkoani Arusha, Rais Kikwete alisisitiza kuwa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) anachokiongoza, kinaendelea kujali maslahi ya walimu kama watumishi muhimu zaidi katika Taifa. Alisema kwamba kilio chao ni cha umma na ni wajibu wa viongozi wote kutilia maanani.
“Nimeyasikia matatizo yenu kupitia risala maalumu, na mengi tulikwishaanza kuyafanyia kazi “Nawaahidi kutatua matatizo yenu kabla sijaondoka rasmi mwishoni mwa mwaka huu, na hata kama nitastaafu hapo baadaye, mengine yaliyosalia yataendelea kutatuliwa na viongozi wa serikali ijayo nami binafsi nitaacha maagizo hayo,” alisema Kikwete.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment