KOCHA MKUU WA KLABU YA SIMBA SC KOPUNOVIC ARIDHISHWA NA TIMU YAKE KUSHIKA NAFASI YA TATU LIGI KUU TANZANIA BARA.
Kocha mkuu wa Simba Mserbia, Goran Kopunovic amesema ameridhishwa na timu yake kushinda nafasi ya tatu katika ligi kuu ya Tanzania Bara iliyomalizika hivi karibuni.
Kopunovic amesema Simba pia ilikuwa na ndoto ya ubingwa, lakini ndoto hiyo ilifutika kutokana na kutofanya vizuri katika mechi za nyuma.
Simba ilianza vibaya ligi hiyo kwa kukumbwa na droo saba mfululizo katika mechi zake saba za mwanzo ikiwa chini ya kocha aliyeondolewa, Mzambia Patrick Phiri.
Kocha huyo amesema anajivunia kuwa na kikosi imara na ana imani timu hiyo itafanya vizuri sana katika msimu ujao.
“Ubingwa tumeukosa, lakini huu sio mwisho wa safari, ni mwanzo wa safari ya msimu ujao” amesema kocha huyo, Simba ilikuwa katika vita ya kugombania nafasi ya pili na Azam, lakini pia ilishindikana.
Yanga, watani wa jadi wa Simba, ndio mabingwa wa ligi hiyo katika msimu wa 2014/2015 wakifuatiwa na waliokuwa mabingwa watetezi, Azam FC na Simba wakiikwaa nafasi ya tatu, hivyo kuwa nje ya michuano ya kimataifa hapo mwakani.
Yanga wataiwakilisha Tanzania katika michuano ya kombe la Washindi barani Afrika wakati Azam watabeba bendera ya nchi katika michuano ya kombe la Shirikisho.
Timu zilizoshuka daraja katika ligi hiyo ni za Ruvu Shooting na Polisi Morogoro ambazo msimu ujao zitacheza Ligi Daraja la Kwanza.
0 comments:
Post a Comment