MAKAMPUNI YA TTPL NA TLTC YAONGEZA AJIRA 3,000 KILA MWAKA MOROGORO.
Kampuni za Tumbaku za Tanzania Tobacco Procesing (TTPL) na Tanzania Lifes Tobacco (TLTC) zimeongeza soko la ajira hususani kwa vijana na wanawake mkoani Morogoro baada ya kutoa ajira za msimu wastani wa ajira 3000 kila mwaka.
Ajira hizo za msimu pia zimeweza kukuza uchumi na kupunguza matatizo ya uhalifu katika mkoa huo yaliyokuwa yakifanywa na vijana wasiokuwa na shughuli maalumu ambao walikuwa wakizagaa mitaani.
Mkurugenzi mkuu wa Makampuni hayo, David Crowhorst alisema hayo wakati wa sherehe za kumaliza msimu uliopita na kukaribisha msimu mwingine pamoja na kutoa zawadi kwa wafanyakazi waliotumikia kampuni hizo kwa muda mrefu pamoja na wafanyakazi bora zilizofanyika Kiwandani hapo.
Crowhorst alisema kuwa Kampuni hizo mbili kwa pamoja zinajivunia kuwa za kwanza katika Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na Serikali iliyopo madarakani kutatua tatizo la ajira kutokana na kuajiri idadi kubwa ya wafanyakazi kuliko zingine zilizopo mjini hapa.
Alizitaja sababu za kutoa ajira nyingi kwa kampuni hizo za tumbaku ni kutumia wafanyakazi wengi kuliko mashine hatua ambayo inasaidia kutoa mwanya mkubwa wa ajira kwa wananchi wa mkoa wa Morogoro.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Utumishi cha makapuni hayo, Gabriel Thobias alisema kuwa kuwepo kwa wafanyakazi hao wa msimu kumechangia kufikiwa kwa malengo ya uzalishaji wa asilimia mia moja kila baada ya kumalizika kwa msimu.
Hata hivyo alisema kuwa pamoja na kufikia kwa malengo hayo lakini kumekuwepo na changamoto mbalimbali za usafirishaji wa tumbaku kutoka katika maeneo ya vijijini ambyo yanazalishwa tumbaku hiyo kutokana na ubovu wa barabara na kuitaka Serikali kuongeza jitihada za kutengeneza barabara katika maeneo hayo.
Thobias aliongeza kuwa Kampuni hizo zimekuwa na sera mbalimbali ikiwemo ya kuhakikisha inatoa elimu ya mara kwa mara juu ya usalama wa wafanyakazi wake pamoja na masuala ya afya kwakuwa maisha yao ni muhimu kwa ustawi wa taifa hili.
Kwa upande wake mmoja wa wafanyakazi wa siku nyingi katika Kampuni hizo, Francis Mizambwa alisema kuwa katika kipindi cha miaka 15 aliyofanya kazi ameweza kunufaika kwa kiasi kikubwa ikiwa pamoja kujenga nyumba yake na kumudu gharama za masomo kwa watoto wake hadi ngazi ya vyuo vikuu.
0 comments:
Post a Comment