BAJETI YA 2015/2015 NI BAJETI PEKEE ILIYOSHINDWA KUONGEZA KODI KATIKA SIGARA NA POMBE NA KUMINYA NISHATI YA MAFUTA..
Dar es Salaam. Kwa mara kwanza Bajeti ya 2015/16, ambayo ni ya mwisho ya Serikali ya Awamu ya Nne, haijaongeza kodi katika bidhaa za pombe na sigara, badala yake imeendelea kupandisha kodi katika mafuta huku ikiminya uingizaji wa bidhaa nchini kwa ajili ya kulinda viwanda na wazalishaji wa ndani na kuongeza ajira.
Pia, bajeti hiyo ya mwisho kwa utawala wa Rais Jakaya Kikwete imeweka kipaumbele katika kugharamia Uchaguzi Mkuu, kuweka msukumo maalum kwenye miradi ya umeme vijijini, maji vijijini, kukamilisha miradi ya kimkakati inayoendelea pamoja na kuwekeza kwenye rasilimali watu.
Bajeti hiyo imeeleza mikakati mbalimbali ya ukusanyaji mapato kwa kufanya mageuzi kwenye mfumo wa kodi, kudhibiti mianya ya matumizi ya fedha za Serikali, kupunguza misamaha ya kodi, kupunguza kero za wastaafu kwa kuwaongezea mafao ya mwezi kutoka Sh50,000 hadi Sh85,000, kupunguza Kodi ya Malipo ya Kadri ya Mapato (Paye) kwa asilimia moja na kuanzisha mafao ya kila mwezi kwa wazee.
Akiwasilisha bajeti hiyo ya mwaka wa fedha wa 2015/16, Waziri Mkuya alipendekeza mabadiliko ya sheria mbalimbali zitakazosaidia kupunguza na kuongeza kodi zitazoisadia Serikali kuongeza mapato ili iweze kufanikisha utekeleji wa bajeti ya Sh22.5 trilioni.
Waziri Mkuya aliliomba bunge liridhie mabadiliko katika Sheria ya Sheria ya Mafuta ya Petroli Sura namba 392 ili kuongeza tozo ya mafuta ya petroli na dizeli kutoka Sh50 hadi Sh100.
Pia, tozo ya mafuta ya taa imependekezwa kuongezwa kutoka Sh50 hadi Sh150 ikiwa ni moja ya njia ya kupunguza uwezekano wa uchakachuaji.
“Hatua ya kuongeza Tozo ya Mafuta ya Petroli inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh139.78 bilioni na fedha zote zitaelekezwa katika mfuko wa Rea kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa usambazaji umeme vijijini,” alisema Mkuya huku baadhi ya wabunge wakionyesha kupinga.
Pia, Mkuya alipendekeza mabadiliko katika Sheria Tozo za Mafuta na Barabara namba 220 ili kuongeza tozo katika mafuta ya Dizeli, Petroli na kwa Sh50 hadi kufikia Sh313.
Alisema hatua hiyo ya kuongeza tozo hiyo pia itaongeza mapato kwa takribani Sh136.4 bilioni ambayo alisema yataelekezwa katika mradi wa kusambaza umeme vijijini wa Rea.
Pamoja na maumivu hayo, Mkuya alipendekeza Waziri wa Fedha apatiwe mamlaka ya kusamehe Tozo ya Mafuta ya Petroli kwenye miradi inayotekelezwa kwa misaada ya wafadhili na yenye mikataba isiyohusisha utozaji wa tozo hiyo ili kuondoa usumbufu na ucheleweshaji katika utekelezaji wake.
Katika jitihada za kulinda viwanda vya ndani na kuongeza ajira, Serikali inapendeleza mabadiliko ya Sheria za Kodi ya Mapato namba 332, Sheria ya mauzo ya nje namba 196, Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004 na Sheria ya Uwekezaji Tanzania Sura 196.
Waziri Mkuya alibainisha kuwa ili kumpunguzia mzigo mfanyakazi wamependekeza kupunguza kiwango cha chini cha kutoza kodi ya mapato ya ajira kutoka asilimia 12 hadi asilimia 11 akibainisha ni dhamira ya Serikali tangu mwaka mwaka 2006/07 kodi hiyo ilipokuwa asilimia 18.5.
Pia, mabadiliko ya Sheria ya Mapato yatashuhudia wafanyabiashara wadogo wakipunguziwa kiwango cha kutozwa kodi kwenye mapato ghafi kwa asilimia 25 ikiwa ni njia ya kuwahamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari. Mbali na kutoa nafuu hizo, Serikali inatarajia kufanya marekebishao ya Sheria hiyo kwa kuondoa msamaha wa kodi kwenye miradi ya Serikali inayotekelezwa kutokana na mikataba baina ya Serikali na taasisi mbalimbali inayohusisha mikopo ya kibiashara kuanzia Julai Mosi, 2015.
“Hatua hizi za Kodi ya Mapato zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 47.2 bilioni,” alisema Mkuya.
Serikali pia, imependekeza kurejesha msamaha wa tozo ya ufundi stadi kwa sekta ya kilimo ili kutoa unafuu wa kodi kwenye shughuli za kilimo mashambani ambazo hutegemea nguvukazi kwa kiasi kikubwa kabla ya kuanza kupata manufaa kutokana na uwekezaji kwenye kilimo.
Hata hivyo, hali si shwari kwa wafanyabiashara wa bidhaa za ngozi nje ya nchi kutokana na bajeti hiyo kuongeza kiwango cha tozo kinachotozwa kwenye kwenye ngozi ghafi.
Bidhaa zinazosafirishwa kwenda nje ya nchi zitatozwa asilimia 80 ya thamani ya ngozi inapokuwa bandarini (FOB) au dola ya Marekani 0.52 kwa kilo moja kutegemea kiwango kipi ni kikubwa kutoka asilimia 60 ya awali au shilingi 600 kwa kilo moja.
Hatua hiyo, kwa mujibu wa Mkuya inazingatia makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kuwianisha viwango vya kodi kwenye ngozi ghafi na pia kuzuia biashara ya magendo na kuhamasisha usindikaji wa ngozi ndani ya ukanda wa Jumuiya ili kuongeza thamani, mapato na ajira.
Hata hivyo, bidhaa za ngozi zilizosindikwa kwa kiwango cha kati zitatozwa asilimia 10 ya kodi ya mauzo ya nje ili kuhamasisha uongezaji thamani wa bidhaa hizo na uwekezaji katika viwanda vya kutengeneza bidhaa za ngozi nchini.
Alisema hatua hizo mbili kwa pamoja zinatarajia kuongeza mfuko wa Serikali kwa Sh920 milioni.
Kampuni zinazozalisha bidhaa za mabomba ya PVC na HDPE zinatarajiwa kupata ahueni baada ya Serikali kuziondoa katika orodha ya bidhaa zinazotambuliwa kuwa ni za mtaji (Deemed Capital Goods) ambazo kwa sasa zinapata msamaha wa kodi kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
“Mapendekezo haya yanazingatia kwamba bidhaa hizi hivi sasa zinazalishwa hapa nchini kwa kiasi cha kutosheleza mahitaji. Hatua hii itasaidia kulinda viwanda vinavyotengeneza mabomba ya aina hiyo na hivyo kuchochea ongezeko la ajira na mapato ya Serikali,” alisema.
Ahueni hiyo itawafikia pia watengenezaji wa matela ya kusafirishia mizigo nchini baada ya bajeti hiyo kufuta msamaha unaotolewa kupitia Kituo cha Uwekezaji kwenye matela hayo, hatua itakayowezesha ushindani katika soko, kuhamasisha uwekezaji mkubwa wa kutengeneza matela nchini, kuongeza ajira na kuongeza mapato ya Serikali.
Wawekezaji wenye nia ya kuwekeza nchini ili watambuliwe kuwa ni mahsusi kwa watatakiwa kutimiza masharti kadhaa ili kupata ahueni ya kikodi, likiwemo la kuwa mtaji wa jumla usiopungua dola za Marekani 300 milioni (630 bilioni) na mtaji huo upitie taasisi za ndani za kifedha.
“Pia anatakiwa kuwa na uwezo wa kutengeneza ajira za moja kwa moja kwa Watanzania zisizopungua 1,500; ikiwa ni pamoja na idadi inayoridhisha katika ngazi za juu za uongozi wa kampuni. Kuwa na uwezo wa kuzalisha fedha za kigeni au kuzalisha bidhaa mbadala wa zile zinazoagizwa nje,” alieleza Mkuya.
Pia, bajeti hiyo inabana uingizaji wa mchele, sukari na vyuma kwa kuongeza ushuru huku bidhaa za nyuzi za kutengezea nyavu, malighafi za kutengenezea pasta na tambi zikiondolewa kodi.
Yaiokoa Sukari
Katika kudhibiti uingizaji wa sukari kiholela na kulinda viwanda vya ndani, Serikali imeongeza kiwango cha ushuru wa forodha kutoka Dola 200 za Marekani kwa tani au asilimia 100 ya thamani ya bidhaa hiyo inapokuwa imefika bandarini, hadi Dola 460 za Marekani kwa tani au asilimia 100 ya thamani ya bidhaa hiyo inapofika bandarini, kutegemea kiwango cha mzigo.
“Sukari inayotumika viwandani hivi sasa hulipiwa ushuru wa forodha wa asilimia 10 badala ya kiwango cha ushuru kilichoainishwa kisheria cha asilimia 100.
Katika utaratibu maalumu unaopendekezwa, waagizaji watatakiwa kulipia ushuru wa asilimia 50 na mara baada ya kuzalisha bidhaa viwandani na kuthibitishwa na Mamlaka ya Mapato kwamba sukari hiyo imetumika ipasavyo watarejeshewa asilimia 40,” alisema Mkuya.
Serikali imepunguza ushuru wa mabasi yenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 25 kwa kutoza asilimia 10 badala ya 25 kwa ajili ya mradi wa mabasi wa jiji la Dar es Salaam (DART) kwa mwaka mmoja.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment