MFANYABIASHARA AKIONA CHA MOTO BAADA YA KUVUTA SIGARA NA KUSABABISHA JAJI, MAWAKILI NA KARANI KUKOHOA MOSHI MAHAKAMANI.
Moshi. Mfanyabiashara wa Moshi Mjini, Lenana Marealle amejikuta matatani baada ya kuwekwa mahabusi kwa saa tatu kwa amri ya jaji baada ya kuvuta sigara eneo la Mahakama Kuu Kanda ya Moshi.
Moshi wa sigara unadaiwa kuingia kwenye vyumba vya mahakama na kusababisha Jaji Mfawidhi, Aishiel Sumari, mawakili na karani wa mahakama kuanza kukohoa mfululizo.
Hili linaweza kuwa tukio la kwanza kwa mhimili wa Dola kutumia mamlaka yake kuzuia uvutaji wa sigara kwenye maeneo ya wazi ya umma licha ya Sheria inayosimamizi bidhaa za tumbaku ya mwaka 2003 kuharamisha.
Tukio hilo limekuja miezi minne tangu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid kutoa agizo la kuzuia uvutaji wa sigara hadharani ikiwamo katika ofisi za umma.
Kwa mujibu wa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Benard Mpepo, Marealle aliwekwa mahabusu iliyopo mahakamani hapo kuanzia saa tano asubuhi hadi saa nane mchana.
Mpepo alisema Marealle aliwekwa mahabusi kwa kosa la kuidharau mahakama chini ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu kifungu 114 kama ilivyofanyiwa marekebisho na Bunge mwaka 2002.
Naibu Msajili alisema kifungu cha 114(b) cha kanuni ya adhabu kama kilivyofanyiwa marejeo na Bunge mwaka 2002 kinakataza mtu kufanya matendo yatakayoharibu usikilizaji wa kesi.
Mpepo alisema adhabu ya kosa hilo ni kifungo cha miezi sita jela au kulipa faini ya Sh500, lakini ilionekana adhabu ya kukaa mahabusi kwa muda huo inatosha kuwa fundisho kwake.
Machi 12, mwaka huu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iliamua kuchukua hatua mahususi katika kuzuia matumizi ya bidhaa za tumbaku katika maeneo ya umma nchini kote.
Dk Rashid alisema madhumuni ya agizo hilo ni kuilinda jamii kutokana na madhara yatokanayo na moshi wa sigara ambao wataalamu wanasema unaweza kusababisha ugonjwa wa saratani.
Agizo hilo la Waziri wa Afya lilihusu maeneo yote ya umma ambayo yanajumuisha ofisi zote za Serikali na taasisi zake, watu binafsi, vyuo na kwenye mikutano na shughuli za umma.
Maeneo mengine ni vituo vya huduma za afya ikiwamo hospitali, vituo vya afya na zahanati, vituo vyote vya usafiri, sehemu za mikutano, bustanini na kwenye fukwe.
0 comments:
Post a Comment