HATIMA YA NCCR-MAGEUZI NDANI YA UKAWA KUJULIKANA BAADA YA MASAA 72.
viongozi wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi ( Ukawa), kutoka kushoto ni James Mbatia,Freeman Mbowe na kulia ni Profesa Ibrahim Lipumba.
Dar es Salaam. Hatma ya chama cha NCCR-Mageuzi kuwa ndani ya Ukawa itajulikana Jumamosi kwenye kikao cha Halmashauri Kuu Taifa, ambacho pamoja na mambo mengine, kitajadili taarifa za kutoridhishwa na mgawanyo wa majimbo ya uchaguzi.
Kikao hicho cha Jumamosi kitakutanisha viongozi wa NCCR-Mageuzi wa mikoa ambao watatoa mwongozo na hatma ya chama hicho ndani ya Ukawa, ambayo ni kifupi cha Umoja wa Katiba ya Wananchi.
Vyama vya NCCR-Mageuzi, CUF, NLD na Chadema viliunda Ukawa wakati wa Bunge la Katiba vikipinga mwenendo wa vikao vya chombo hicho cha kutunga Katiba, na baadaye viongozi kusaini makubaliano ya kushirikiana kwenye Uchaguzi Mkuu ujao kwa kusimamisha mgombea mmoja kwenye nafasi za urais, ubunge na madiwani.
Tayari kamati inayoshughulikia utekelezaji wa azimio hilo imeshakutana na kukubaliana kugawana majimbo kwa asilimia 95, kwa mujibu wa viongozi wa Ukawa, lakini kumekuwapo na hali ya sintofahamu kwenye asilimia iliyosalia, hali kadhalika changamoto ya kikatiba katika kupata mgombea mwenza na waziri mkuu.
Habari zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa miongoni mwa sababu za NCCR kutaka kujiondoa Ukawa ni kupewa majimbo machache ya uchaguzi kinyume na matarajio yao.
“Hoja nyingine ni kutoandaliwa kwa kanuni za kuongoza umoja huo mpaka sasa na hadi sasa majimbo 13 hawajafikiwa mwafaka,” alisema mpashaji habari wetu.
“Wanachama walitarajia kupata kati ya asilimia 10 na 15 ya majimbo yote, lakini mpaka sasa tumepata asilimia 3.4 tu kati ya majimbo 239 na hakuna matumaini ya kupata zaidi ya hapo kwa hivyo kuna wasiwasi wa wanachama kuazimia kujitoa.”
Hata hivyo, mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alipoulizwa kuhusu masuala hayo, pamoja na kukiri kuwapo kwa kikao Jumamosi, alikanusha madai ya chama hicho kutaka kujitoa Ukawa.
Alisema kikao hicho kitajadili hali ya kisiasa nchini na Uchaguzi Mkuu, lakini akasema suala la mgombea urais bado linajadiliwa ndani ya Ukawa.
Akizungumzia suala hilo Mbatia alisema, “Siyo kweli, hakuna mtu yeyote NCCR mwenye fikra ya kujitoa ndani ya Ukawa. Halmashauri Kuu haijaitishwa kwa ajili ya kujadili kujitoa Ukawa. Sisi ni waasisi wa Ukawa na NCCR ni chama cha maridhiano pia ni chachu ya kuleta mabadiliko ya Katiba tangu mwaka 1991 na kitajadili hali ya kisiasa nchini na uchaguzi wa ndani ya chama kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Kuhusu mgawanyo wa majimbo, Mbatia alisema: “Kwenye makubaliano yoyote duniani kuna kupata na kupoteza. Ukawa si ya NCCR, Chadema, CUF wala NLD, ni mali ya Watanzania.”
Alisema Watanzania wanataka kuona Ukawa ikipiga hatua na viongozi wa vyama hivyo wanaweza wasiwepo lakini umoja huo ukaendelea kuwapo kwa kuwa ni injini ya kuwaunganisha, na NCCR haina ubavu wa kujitoa.
Kuhusu mgawanyo wa nyadhifa nyingine ndani ya umoja huo, Mbatia alisema: “Tutatekeleza matakwa yote ya kisheria kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania na sheria ya uchaguzi na tutashiriki uchaguzi ipasavyo. Hayo ni mambo madogo ambayo tutayakamilisha hivi karibuni na kuueleza umma wa Watanzania.”
“Unaona CCM wanavyosuguana au Chadema wanavyosuguana. Hebu fikiria chama kimoja kina katiba yake na bado kinasuguana sasa Ukawa ina vyama vinne, misuguano ni lazima itakuwapo, tena mikubwa zaidi. Kinachotakiwa hapa ni hekima, amani na umoja ili tujenge maeleweno ya pamoja kwa maslahi ya Watanzania wote.”
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya vyama vinavyounda Ukawa vinaeleza kuwa moja ya hoja zilizotolewa na kujadiliwa iwapo mgombea urais atatoka kwenye vyama nje ya CUF chenye nguvu Zanzibar, ni uwezekano wa kada wake mmoja kuhamia chama kitakachotoa mgombea urais kwa uwazi ili apitishwe kuwa mgombea mwenza, wakiamini kuwa akiwa huko atalinda maslahi ya CUF, ambayo pia kitakuwa kimetoa mgombea urais wa Zanzibar.
Juni Mosi mwaka huu, aliyekuwa mwenyekiti Kitengo cha Vijana wa NCCR-Mageuzi, Deo Meck alitoa madai yanayofanana na hayo, lakini baadaye alivuliwa wadhifa wake kwa kuzungumza mambo ya chama katika vyombo vya habari wakati si msemaji.
Katibu mkuu wa NCCR, Mosena Nyambabe alisema katika kikao hicho wajumbe watatoa mwongozo wa ushiriki wao ndani ya Ukawa.
“Tunachoratajia ni maoni watakayokuja nayo wajumbe wa mkutano kutoka kwa wanachama mikoani, kutueleza hali ya ushawishi, mwitikio na mategemeo yao ndani ya Ukawa,” alisema Nyambabe.
Kuhusu hoja ya mgombea urais, Nyambabe alisema NCCR-Mageuzi haina tamaa ya kulazimisha kusimamisha mgombea wa nafasi hiyo.
Hata hivyo, alisema endapo chama hicho kitaridhishwa na uwakilishi wa majimbo kinaweza kuunga mkono mgombea wa chama chochote atakayesimamishwa.
Kauli ya Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe hakutaka kuzungumzia suala la mgawanyo wa madaraka.
“Nisingependa kuzungumza vitu ambavyo hatujavifanyia uamuzi na kuviweka hadharani. Muda mwafaka ukifika, tutawaeleza na sasa siwezi kuvipakua hadharani vitu ambavyo vinajadiliwa katika vikao.”
Mbowe pia alizungumzia mgawanyo wa majimbo akisema suala hilo linasubiri Tume ya Taifa ya Uchaguzi kukamilisha ugawaji majimbo.
“Hatuwezi kugawa majimbo kwa sasa wakati NEC haijajua kuna majimbo mangapi ya uchaguzi. Sisi tutagawa vipi wakati hatujui mapya ni mangapi? Wakishatangaza na sisi ndiyo tunaweza kusema jambo.”
Licha ya vigezo sita vya kupitisha mgombea wa jimbo na urais kuegemea zaidi Chadema, utata umeendelea kujitokeza huku baadhi ya wanachama na viongozi wakisema hoja siyo vigezo pekee bali ni maridhiano.
Migogoro ndani ya Ukawa
Dalili za mgogoro ndani ya Ukawa zilianza kuonekana katika matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Katika nafasi ya wenyeviti wa mtaa, CCM ilichukua jumla ya mitaa 2,116. Vyama vingine na nafasi zao kwenye mabano ni Chadema (753), CUF (235), NCCR - Mageuzi (8), ikionyesha wazi kutosimisha mgombea mmoja katika maeneo yote nchini.
Matokeo ya kuanguka Ukawa katika maeneo mengi ya ushindi wa CCM ilielezwa na Naibu Katibu Mkuu CUF-Bara, Magladena Sakaya kuwa ni sababu ya kutokubaliana kwa baadhi ya wanachama kusimamisha mgombea mmoja.
Mbali na hatua hiyo, katika uchaguzi wa kura ya maoni ndani ya CUF, Wilaya ya Kinondoni, chama hicho kiliwapitisha Leila Hussen kuwakilisha Jimbo la Kawe na Mashaka Ngole kwa Jimbo la Ubungo huku Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo akisema majimbo hayo si mali ya Chadema.
Kutokana na hatua hiyo, NCCR-Mageuzi na NLD vilisema CUF imeanza kwenda kinyume na makubaliano ya Ukawa, ingawa chama hicho na Chadema vilieleza kuwa haikuwa kosa kufanya kura ya maoni kwenye majimbo hayo.
Lakini hivi karibuni Sakaya, katibu mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, makamu mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdalah Safari na Mbatia walimwambia mwandishi wa gazeti hili kwamba, pamoja na changamoto hiyo, muda uliobakia unatosha kuelimisha wanachama wa ngazi ya chini.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment