JAMES MBATI AENDELEA KUIBANA SERIKALI MISAMAHA YA KODI NA KUPOROMOKA KWA SHILINGI YA TANZANIA.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imehoji serikali kutochukua hatua madhubuti na za kuridhisha katika kukabiliana na kuporomoka kwa Shilingi ya Tanzania na pia upotevu wa mapato utokanao na misamaha ya kodi.
Imesema kwa mujibu wa tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania ya Oktoba 1, 2014, dola ya Marekani ilikuwa inauzwa kwa Sh. 1,674 lakini hadi kufikia Juni 5, 2015, dola hiyo imeuzwa kwa Sh. 2,054 za Tanzania, ikiwa ni ongezeko la asilimia 23.
Akiwasilisha hotuba ya kambi hiyo kuhusiana na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2015/16, Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani wa Wizara ya Fedha, James Mbatia, alisema thamani ya Shilingi ya Tanzania inaendelea kudhoofika kulinganisha na fedha za nchi nyingine zikiwamo nchi jirani kama Kenya, Rwanda na Burundi.
“Tunaomba serikali ituambie, je, imeshindwa kutafuta vyanzo vya mapato au kusimamia vyanzo vilivyopo kiasi kwamba imeamua kutegemea hali hii mbaya kiuchumi ili kuongeza mapato yake? Je, serikali ikituhumiwa kuwa imeporomosha shilingi kwa makusudi ili ikusanye mapato bila kuangalia athari zingine inaweza kukwepa tuhuma hizi?” Alihoji.
Alisema imeoneshwa kwamba thamani ya shilingi dhidi ya Paundi ya Uingereza imeshuka kwa asilimia 13 kwa kutumia takwimu za Benki Kuu na asilimia 24 kwa kutumia takwimu za kisoko dhidi ya Euro, ikiwa ni anguko la asilimia 8.
“Inasikitisha kuona hata nchi ya Burundi, ijapokuwa ipo kwenye misukosuko mingi lakini bado shilingi yetu imeanguka dhidi ya faranga yao kwa asilimia 20…hii ni aibu na fedheha kubwa,” alisema Mbatia.
Alisema athari za kushuka kwa shilingi ni wawekezaji kushindwa kuwekeza nchini kwa kuwa wengi hawapendi mazingira yasiyotabirika na athari nyingine ni kushuka ghafla kwa pato la taifa kutokana na kutegemea bidhaa zinazoagizwa nje.
MAFAO YA WASTAAFU
Mbatia alisema baadhi ya wastaafu wanalipwa fedha kidogo ambazo hazilingani na gharama za maisha ya sasa na kutoa mfano kuwa wapo wazee wanaolipwa Sh. 50,000 tu kwa mwezi.
“Hivi kweli mzee aliyetumikia hili taifa kwa uaminifu akiwa kijana mpaka amestaafu leo unamlipa sh. 50,000? Hu ni ukiukwaji wa haki za msingi za kuishi,” alisema.
Alisema Sheria ya Mafao kwa Watumishi wa Umma ya 199 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2005, kwa ajili ya viongozi wa saisa, inawapa fursa viongozi wastaafu wa ngazi za juu ambao ni marais, makamu wa rais, mawaziri wakuu, wakuu wa vyombo vya ulinzi na jaji mkuu, lakini wazee wengine wanashindwa kutendewa haki ambao wametumikia taifa kwa weledi na uadilifu mkubwa.
MATUMIZI YA FEDHA ZA UMMA
Alisema serikali imeonyesha udhaifu mkubwa kwa matumizi ya fedha za umma kwani hadi kufikia Machi 2015, takwimu kuwa bado miradi na mipango mbalimbali haijakamilika.
Aidha, alisema fedha za matumizi ya maendeleo kwa baadhi ya sekta ni pungufu kwa wastani wa asilimia 40 mpaka sasa.
Alisema nidhamu katika matumizi ya fedha za umma ni kichocheo kikubwa katika kuangamiza uchumi wa Tanzania kwani serikali imekuwa ikiweka mkazo katika matumizi ya kawaida yasiyokuwa ya msingi wala tija kwa umma.
Alisema miaka 10 iliyopita, serikali ilikuwa inakusanya wastani wa sh. bilioni 170 kwa mwezi, lakini hivi sasa inakusanya wastani wa Sh. bilioni 950.
“Cha kushangaza, hakuna kipindi (kama hiki) katika historia ya nchi yetu ambacho kumekuwa na malalamiko makubwa ya ukosefu wa fedha serikalini, mishahara kucheleweshwa, miradi ya maendeleo kukwama kwa sababu ya kukosa fedha.”
MISAMAHA YA KODI
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Ole (CUF), Rajab Mbarouk, ameitaka serikali kutoa maelezo kuhusu zaidi ya Sh. bilioni 24 zilizopotea kwa sababu ya misamaha ya kodi kama ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), inavyosema.
Akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha, kwa mwaka 2015/16, Mbarouk alisema misamaha ya kodi haijapewa kipaumbele katika makusanyo ya ndani ili kusaidia bajeti ya serikali.
Aidha, alisema zaidi ya Sh. bilioni 4.9 ziko nje kutokana na watu wanaokusanya kodi mbalimbali kutokuwa waadilifu na waaminifu.
Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Arumeru Magharibi (CCM), Goodluck Ole Medei, alisema kutokana na wakusanya mapato kutokuwa waaminifu, miradi mingi ikiwamo ya barabara, maji na umeme imekwama.
Alisema fedha nyingi zinazokusanywa hazipelekwi sehemu husika na matokeo yake kukwamisha shughuli za maendeleo.
Alipendekeza pia serikali irekebishe Sheria ya Manunuzi, ili yafanyike kwa njia ya mtandao kwa lengo la kudhibiti rushwa.
Akihoji kuhusu kukwama kwa mradi wa umeme wa upepo, Mbunge wa Singida Magharibi (CCM), Mohammed Missanga, alisema, mradi huo ungewezesha kutoa ajira kwa watu zaidi ya 2,000 na kuongeza megawati za umeme 300.
Kwa upande wake Mbunge wa Kigoma Mjini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, alitaka kujua kampuni za simu zinazoingiza faida kubwa na kutojiorodhesha katika Soko la Hisa.
“Wananchi wanashirikishwaje katika mitaji ya kampuni hizo kama hazijajiorodhesha kwenye soko la hisa,” alisema.
Mbunge wa Longido (CCM), Michael Laizer, alisema serikali iangalie sheria ya manunuzi kwani kuna tofauti kati ya jengo linalojengwa na serikali na lile linalojengwa na wananchi. Alishauri mapato ya serikali yaende sambamba na matumizi.
Akiunga mkono hoja hiyo, Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo, alisema serikali iweke mfumo utakaoonyesha kupatikana kwa gesi nchini kutaisaidia bajeti ya serikali kiasi gani.
Alisema bajeti ya kutegemea soda na kodi za wafanyakazi haiwezi kuikwamua nchi na umaskini. CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment