KATIBU MKUU WA CCM AWASHAWISHI WATANZANIA KUWAKATAA MAFISADI.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM ), Abdulrahman Kinana.
Watanzania kwa ujumla wao wametakiwa kupambana na mafisadi nchini ili kukomesha ubadhilifu wa fedha za umma badala ya kuacha kazi hiyo kwa serikali pekee.
Wito huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM ), Abdulrahman Kinana, wakati akihutubia mamia ya wananchi wa wilaya ya Geita wakati akihitimisha ziara yake ya siku saba mkoani hapa.
Alisema mafisadi hawana chama wala dini na wanapokuwa ndani ya CCM na vyama vya upinzani, hivyo wanatakiwa kupigwa vita na Watanzania wote bila kujali makundi wanayotoka.
"Msidanganyike wizi hauna chama, dini wala kabila, mwizi ni mwizi tu, hivyo ni vyema Watanzania tukashirikiana kuwafichua na kuwapiga vita ndani ya jamii,” alisisitiza.
Kauli hiyo ya Kinana ilikuja baada ya wachimbaji wadogo wa eneo la Mgusu kusema wamepewa na serikali fedha za ruzuku Sh. bilioni tatu ili waboreshe shughuli zao za uchimbaji lakini wamekuwa wakishawishiwa na wapinzani wasizikubali kwa madai kuwa watanyang'anywa maeneo yao.
Alisema baada ya kuzikataa fedha hizo zilipelekwa eneo jingine la uchimbaji la Rwamgasa hali iliyowanya wachimbaji hao kufanya kazi hiyo katika hali ngumu.
Wachimbaji hao walimuambia Kinana awasaidie kupata ruzuku hiyo ya serikali.
Kufuatia maelezo hayo, Kinana aliwataka Watanzania kuwa na desturi ya kupima maneno ya wanasiasa yanayozungumzwa majukwaani badala ya kuyaamini moja kwa moja na kuyafanyia kazi.
"Mlidanganywa msichukue hela wakati wao shughuli zao zinaendelea zenu zimesimama, kuweni na utaratibu wa kupima maneno yetu hata mimi msiniamini nipimeni kwanza kama ninachoongea kina faida kwenu," alisema Kinana. CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment