BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

ZIARA YA RAIS JAKAYA KIKWETE NCHINI INDIA YAZAA MATUNDA NA NEEMA KWA WAKULIMA WA TANZANIA, AKABIDHIWA MATREKTA MAKUBWA 10 NA KAMPUNI YA HOLLAND AGRICULTURE KAMA ZAWADI.


http://www.widoczki.com/widoczki/2/new-kombajn-holland.jpeg
Rais Dk. Jakaya Kikwete amepokea matrekta makubwa 10 yaliyotolewa na kampuni ya New Holland Agriculture ya nchini India, ikiwa ni zawadi aliyopewa kwa ajili ya mkulima wa Tanzania.


Matrekta hayo, aina ya TD 5.90 alikabidhiwa Rais Kikwete katikati ya wiki hii wakati wa ziara yake nchini India alipotembelea kiwanda cha kampuni hiyo kilichoko eneo la Greater Noida, nje kidogo ya mji mkuu wa India, New Delhi.

Kiwanda hicho, ambacho huzalisha matrekta ya kisasa 58,000 kwa mwaka, kimekuwa kikifanya biashara na Tanzania kuanzia mwaka 2011, na kimewahi kuliuzia Shirika la Biashara la Jeshi la Kujenga Taifa la SUMA JKT matrekta 700.

Aidha, mpaka itakapofika mwisho wa mwaka huu, imepangwa kuwa shirika hilo la JKT litanunua matrekta mengine 300 kwa ajili ya kuboresha na kuleta mageuzi katika kilimo cha Tanzania.

Tumeona jitihada za serikali za kuboresha nyenzo za kilimo kwa kupunguza kodi ya pembejeo za kilimo pamoja na kutoa fursa kwa wafanyabiashara kuingiza matrekta nchini kwa gharama nafuu, hatua ambayo kwa kiwango kikubwa imeboresha uzalishaji wa mazao ya kilimo nchini.
https://pbs.twimg.com/profile_images/563341704283959297/qILV9GY-.jpeg Asilimia 80 Watanzania hasa wanaoishi vijijini wanategemea sana kilimo, lakini bado wanatumia jembe la mkono.

Kusema ukweli kilimo cha aina hiyo hakiwezi kumwondoa mkulima kutoka katika lindi la umaskini kwani nguvu kubwa anayoitumia haitakuwa na uwiano na mazao anayoweza kuyapata.

Ziara ya Rais Kikwete nchini India ni fursa kubwa ya kuimarisha sekta ya kilimo nchini. Ni dhahiri kuwa baada ya ziara hiyo, utakuwapo msukumo mpya na kasi ya uwekezaji katika sekta ya kilimo, hasa ikizingatiwa kwamba tayari kupitia Rais Kikwete mwenyewe, alishatoa tamko lililojulikana kama ‘Azimio la Kilimo Kwanza, lililobeba nguzo kumi.

Tamko hilo alilolitoa Agosti 3, 2009 mjini Dodoma, lilisisitiza kwamba kwa maendeleo ya Tanzania, kilimo ni karibu kila kitu. Na kwamba kilimo hutegemewa na asilimia 80 ya Watanzania kimaisha huku kikichangia asilimia 26.7 ya pato la taifa. Kwa mantiki hiyo, kilimo ni uti wa mgongo wa taifa letu.

https://umaskiniafrica.files.wordpress.com/2011/08/tulime.jpg Zinapotolewa taarifa za uboreshaji wa kilimo kwa maana ya kuongeza nyenzo za uzalishaji kama upatikanaji wa zana za kisasa, mfano matrekta, kwa mkulima wa kawaida hizo ni habari njema sana.

Kilimo ni kiungo muhimu cha sekta mbalimbali katika kuchangia kutimiza malengo ya kukuza uchumi wa taifa. Na hakika, hatuwezi kufuta umasikini bila ya kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo.

Tunapongeza juhudi za Rais wetu katika kuvalia njuga suala hili la kukuza uchumi kupitia uboreshaji wa kilimo.

Na hili yafaa libebwe kwa mzigo na viongozi wengine wenye dhamana katika sekta hii ili taifa liondoke hata lilipo kutoka utegemezi hadi kujitosheleza wenyewe katika kila nyanja ya maendeleo.

Tunaamini kuwa mahusiano ya kibiashara kati ya kiwanda hicho na taasisi za uzalishaji hapa nchini kama SUMA JKT yataimarishwa zaidi ili wakulima waendelee kunufaika kwa teknolojia ya kilimo na uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo.

Tunatambua kuwa kilimo chetu ni duni, tunahitaji kuweka mikakati ya kujikwamua kutoka katika hali duni ya nyenzo za kilimo ili tuzalishe zaidi na kupata ziada ya kuuza kwa wahitaji.

Na hiyo itawezekana kwa kutumia teknolojia ya matumizi ya matrekta hayo ya kulimia pamoja na matrekta makubwa ya kuvunia mazao (harvesters).

Pia tunatambua jitihada za Rais Kikwete za kuimarisha uchumi wa nchi kupitia kilimo, na ndio maana katika kipindi kifupi, serikali yake imewezesha upatikanaji wa matrekta zaidi ya 700 ambayo yameuzwa kwa wakulima kwa njia ya fedha taslimu pamoja na mikataba ya mikopo nafuu.

Ingawa matrekta hayo ni idadi ndogo ikilinganishwa na mahitaji halisi, bado tunaamini kuwa yatasaidia wakulima wengi kupiga hatua muhimu na kupunguza kasi ya umaskini miongoni mwa wakulima nchini.

Ni imani yetu kuwa milango zaidi ya uwekezaji katika kilimo itafunguliwa na maboresho ya uzalishaji wa bidhaa za kilimo yatafanyika ili hatimaye wakulima waweze kuzalisha kwa ziada ili kuondokana na umaskini. CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: