BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

LOWASSA HAKUNA ANACHOWAZA ZAIDI YA KUONGOZA NCHI YA TANZANIA KATIKA NAFASI YA URAIS.


 

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amesema anasali sana ili akabidhiwe kijiti cha kuendesha nchi kwa kasi ya mchakamchaka wa maendeleo.


Lowassa alisema hayo alipowasili mkoani hapa akitokea Tabora na kupokelewa na umati mkubwa wa watu katika uwanja wa ndege, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya.

Lowassa amekuwa kada wa tatu wa CCM kati ya waliotangaza nia ya kugombea urais kupitia CCM kufika katika mkoa huo kutafuta wadhamini. Waliotangulia kufika ni Makongoro Nyerere na Mohamed Gharib Bilal.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa idadi ya wanachama waliojitokeza kumdhamini katika mbio zake za kusaka urais, alisema endapo atakabidhiwa kijiti hicho cha urais atahakikisha anaiendesha nchi kwa kasi ya maendeleo.

“Mzee mwinyi alifanya makubwa, Mkapa pia alifanya makubwa, Kikwete naye pia amefanya makubwa, Mwalimu Nyerere ndio usiseme, nasali ili kijiti hichi nikabidhiwe mimi ili niendeshe hii nchi mchakamchaka wa kimaendeleo,”alisema Lowassa.

Alisema anajua umaskini wa Kigoma na hajasimuliwa na mtu na nia ya kugombea urais ni kutokana na kuchoshwa na hali ya umaskini.

Aidha, aliwahimiza wakazi wa Kigoma wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura na pia katika kipindi cha uchaguzi wajitokeze kwa wingi kupiga kura.

“Siri ya uchaguzi huu ni kupiga kura, wale wote mliojiandikisha hakikisheni mnajitokeza kwa wingi kupiga kura,” alisema.

Aliwashukuru wanachama hao kwa kujitokeza kwa wingi kumdhamini na kusema kuwa imani huzaa imani.

Kwa upande wake, Katibu wa wilaya ya Kigoma Mjini, Nohoti Kibaji, alisema jumla ya wanachama 11,250 wamejitokeza kumdhamini katika mkoa huo.

“Katika wilaya ya Kigoma mjini amepata wadhamini 2,550, Kigoma vijijini 2,550, Buhingwe 1,350, Kasulu 2,550, Uvinza 900, Kibondo 900 na Kakongo 450,”alisema Katibu huyo.

Naye Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba, alisema watu wa Kigoma wapo mstari mmoja na wapo tayari kuhesabiwa na Lowassa.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, alisema Lowassa anavuna matunda yake ambayo yametokana na kujali rasilimali watu na anabebwa na sifa zake za kiutendaji.

“Huu ni ushahidi kuwa Edward Lowassa anaona matunda yake aliyowekeza kwenye rasilimali watu na ndio mtaji mkubwa alionao, na hakuna mtu ambaye amenunuliwa kuletwa hapa,” alisema Mgeja. CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: