BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MGOMBEA URAIS NDANI YA CCM AOMBA CHAMA KISIMPITISHE MLARUSHWA VINGINEVYO ATAJIONDOA.

http://api.ning.com/files/QmRFQRFpoATkG0L2pXVIFSfdoYQDFpqEHimOxHpAdVF1Fbsu4zsrk57zon8wwsmUbD0H1rRCFHp18fqrmYMuV49buypbzn5u/makamba.jpg

Januari Makamba.

Dar es Salaam. Makada wa CCM waliotangaza nia au kuchukua fomu za kuomba kupitishwa na chama hicho kuwania urais, wameeleza jinsi rushwa, ufisadi na udhaifu katika ukusanyaji kodi huku wakijinadi kuwa wao ndiyo wataondoa uovu huo iwapo watapitishwa kushika nafasi hiyo ya juu kisiasa.


Lakini hakuna hata mmoja aliyeiponda Serikali kwa kushindwa kudhibiti rushwa, ambayo baadhi walishasema kuwa imekithiri hata kwenye chama hicho tawala, huku mmoja akisema kuwa iwapo CCM itampitisha mlarushwa, atajiondoa.


Kati ya waliotangaza nia na kuchukua fomu, makada 11 ni mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Nne wakiwamo mawaziri waandamizi walioshika nafasi za juu na waliofanya kazi katika awamu zote nne.


Pia wamo makada waliokuwamo kwenye Baraza la Mawaziri la Serikali ya Awamu ya Nne, lakini wakaondoka kwa sababu tofauti, huku kundi jingine likihusisha watendaji wakuu wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa.


Lakini bado tatizo hilo la rushwa limekuwa likitumiwa na makada hao wa CCM wanaowania urais wakati wakijinadi kwa wanachama wao kwamba watafumua mfumo uliopo, kusuka upya sheria na kuimarisha taasisi za fedha ili watuhumiwa wakubwa wa rushwa wafikishwe kortini na kufungwa, badala ya kuwakamata walarushwa wadogowadogo pekee.


Katika hotuba zao wakati wanatangaza nia mbele ya umati wa wafuasi wao na mbele ya waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu, makada hao, mbali ya kueleza mikakati tofauti ya namna ya kuimarisha uchumi wamekosoa mfumo wa sheria kwamba unawalinda mafisadi wakubwa ambao hawakamatwi hadi kwa kibali maalumu.

http://taarifa.co.tz/wp-content/uploads/2014/08/bunge_katiba.jpg
Samuel Sitta.


Kwa mfano, akitangaza nia ya kuwania urais kijijini kwao Butiama, Charles Makongoro ambaye ni mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alisema anaomba kibali cha kuisaidia CCM ikomeshe rushwa, na atakapoingia madarakani, ili asiwaangushe Watanzania, anahitaji chama imara kisicho na shaka kama ilivyo sasa.


“Kosa la Rais Jakaya Kikwete ni kuwapenda sana marafiki zake. Kwa bahati mbaya, baadhi ya marafiki zake hao ni vibaka,” alisema Makongoro ambaye ni mbunge wa Afrika Mashariki.


Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe aliwaambia wafuasi wake mkoani Lindi kwamba ili kutekeleza utawala bora, hawezi kukaa kimya kuona rushwa, ubadhirifu, ufisadi vikichukua nafasi katika utawala wake.


“Ninawatumia salamu mapema, sitakuwa na kigugumizi kwa wanaotesa Watanzania. Nitahakikisha Watanzania wanachukia rushwa na kutakuwa na sheria kali dhidi ya mtoa na mpokeaji rushwa. Kama ni watumishi wa umma, watakwenda na maji...,” alisema mbunge huyo wa Mtama.


Ahadi ya kukomesha rushwa pia ilitolewa na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta aliyesema kwamba anataka kulifanyia Taifa mambo matano, ikiwa ni pamoja na kutenganisha biashara na siasa na kusimamia maadili ya viongozi wa umma.


“Ili kukomesha tatizo la rushwa, hatuna budi kutunga sheria itakayotenganisha biashara na uongozi,” alisema Sitta kwenye Ikulu ya Wanyanyembe iliyopo Itetemia, Tabora.


Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba alisema akifika Ikulu, ili kupambana na rushwa, “nitafanya mabadiliko ya kisheria, kimfumo, kitaasisi na kijamii ikiwamo kuipa meno Takukuru kuwa na mamlaka kisheria ya kuwashtaki watuhumiwa wa rushwa moja kwa moja mahakamani”.

http://mtanzania.co.tz/wp-content/uploads/2015/06/Bernard-Membe.jpg
Bernard Membe.

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira alionyesha kukiri kuwa miongoni mwa makada waliojitokeza kuwania urais, wamo wenye kashfa za rushwa, lakini akajitenga nao kujionyesha kuwa hana doa hilo.


“Ili kukabiliana na changamoto hizi kubwa, itakuwa lazima kwa chama chetu kumteua mgombea ambaye hana historia ya kuhusishwa na ufisadi, iwe kwa kutuhumiwa tu au kuhusika kweli. Mgombea anayejua historia ya nchi yetu, pale ilipo na kule inakopaswa kuelekea,” alisema waziri huyo mkongwe na kuongeza:


“Kumbukeni sijatajwa katika kashfa kama za Escrow, EPA, Richmond na nyinginezo.”


Wasomi wawashangaa
Lakini kauli na ahadi hizo za makada hao wa CCM wanaotaka kuingia Ikulu zimewashangaza wachambuzi waliofuatwa na Mwananchi ili kutoa maoni yao kuhusu hoja za wagombea.


Mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu), Profesa Gaudence Mpangala alisema wengi waliotangaza nia ya kuwania urais wanatoka kwenye mfumo wa rushwa, hivyo itakuwa kazi ngumu kwao kuiondoa. “Tanzania imefikia ngazi ambayo rushwa imekuwa mfumo wa utawala. Ikifikia hatua hiyo kuindoa ni kazi kubwa kwa sababu kupiga vita mfumo si suala dogo, hawa watiania walishindwa huko serikalini, watawezaje sasa?” alihoji.


Alisema wengi kati ya wagombea hao wanatoka katika mfumo wa rushwa ambao wameujenga wenyewe, hivyo si kazi rahisi kuimaliza kwa sababu kuna kulindana na kustahimiliana.


“Kulindana ni utamaduni wa mfumo huo wa rushwa. Ndiyo wameujenga na walikuwa ndani ya mfumo, ndiyo maana wanashindwa kueleza watatumia mbinu gani


kuondoa mfumo huo,” alisema.
Alisema anahitajika mtu shupavu kuiondoa rushwa hapa nchini kwa sababu imeshaota mizizi kwenye mfumo wa utawala, na kwamba kusema tu wataimaliza hakuna ukweli wowote.


“Ufisadi unaofanywa na viongozi wa Serikali, vigogo na wanasiasa zina athari kubwa kwa uchumi wa nchi hii,” alisema Profesa Mpangala.


Mawazo hayo yanalingana na ya mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Hamad Salim ambaye alisema ni vigumu kwa wanaotaka kuwania urais kuimaliza rushwa kwa sababu wote wanafanya kazi katika mfumo uliojaa rushwa.


“Wao wenyewe wanaingia madarakani kupitia mfumo wa rushwa, sidhani kama wataweza kuung’ata mkono ambao unawalisha. Kama mchakato mzima wa kuingia madarakani kama vile kuchukua fomu, kupiga kura, kutafuta wadhamini wote umejaa rushwa, wataweza kuiondoa?” alihoji.


Alisema ahadi wanazozitoa watia nia ni vigumu kutekelezeka kwa sababu wanapambana na mfumo wao wenyewe na kazi ya kuumaliza ufisadi si ya mtu mmoja wala ya siku moja.


Salim alisema inashangaza baadhi ya watangazania kukusanya watu wanaowaunga mkono, kuandaa kampeni na kuandaa watu wa kuwashangilia.


Alisema watangazania hao wanatoa ahadi zao kama kampeni tu na wakiingia madarakani hawatafanya kazi kulingana na walichoahidi bali kwa kuangalia ilani ya CCM.


Mchambuzi wa masuala ya siasa wa UDSM, Dk Benson Bana aliwataka watangazania hao kuacha kutumia kigezo cha rushwa kama njia ya kupata kura na badala yake wazungumzie sera nyingine.


Dk Bana alisema Watanzania hawatamchagua kiongozi kwa sera zake za kutaka kuondoa rushwa kwani nao wanafahamu kuwa CCM imejaa rushwa.


“Watanzania hawamchagui mtu kwa kigezo cha kupambana na rushwa, hicho ni kimbelembele tu, waache kimbelembele,” alisema.


Dk Bana pia alisema watangazania hao waiache Takukuru ifanye kazi yake na wasiwadanganye wananchi kuwa wao ni mabingwa wa kupambana na tatizo hilo.


Lakini mkufunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha(IFM) kitivo cha kompyuta na mifumo ya hesabu, Dk Eliamani Sedoyeka aliliangalia tatizo la rushwa kuwa ni silka na hivyo ni vigumu kuthibitisha iwapo mgombea ana au hana tatizo hilo.


Dk Sedoyeka alisema kiongozi anayesema atapambana na rushwa anatakiwa kupimwa kwa rekodi yake ya uongozi kwa kuangaliwa iwapo aliweza kukemea, kuadhibu, au kukataa rushwa katika mazingira yoyote yale.


“Kwa mfano wapo watu wanajiweka karibu na matajiri, wanapewa fedha na matajiri za kufanya kampeni, je watakuja kulipa vipi hisani za matajiri watakapoingia madarakani? Hayo ndiyo mazingira,” alisema


Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa UDSM, Dk Alexander Makulilo alisema mapambano ya rushwa si ya mtu mmoja wala chama kimoja kwani Tanzania imekithiri kwa rushwa kwa kiasi kikubwa.


“Tatizo la rushwa ni kubwa na ni la jumuiya nzima. Kwa namna moja au nyingine kutoka 2005-2012, Takukuru kuna tuhuma 43,000. maana yake ni kuwa tatizo ni kubwa,” alisema


Dk Makulilo alisema hata taasisi nyingi nchini zinanuka rushwa na hata zile za kupambana na rushwa nazo ni dhaifu wakati na sheria nazo ni dhaifu.


Alisema wagombea wengi wameshindwa kupambana na rushwa na hata hawa wa sasa wataendeleza kile kile na hakuna uhakika kama watalimaliza tatizo hili.


“Bado hatujapata uongozi kama wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye uongozi wake haukuweza kuwavumilia wala rushwa. Alipambana na rushwa kivitendo,” alisema.


Imeandikwa na Joster Mwangulumbi na Florence Majani.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: