Zanzibar. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wamemzuia Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kuhudhuria shughuli ya kuvunja Baraza hilo itakayoongozwa na Rais Dk Ali Mohamed Shein leo.
Uamuzi huo ulitolewa baada ya Spika wa Baraza hilo, Pandu Ameir Kificho kutoa utangulizi kwa wajumbe akiwataka watengue kanuni ili viongozi wa kitaifa watakaohudhuria shughuli hiyo waweze kuingia ukumbini badala ya kukaa sehemu ya kawaida ya wageni waalikwa.
Baada ya kutoa utangulizi, Spika Kificho alianza kuwahoji wajumbe wanaokubali viongozi wa kitaifa waruhusiwe kuingia ndani ya Ukumbi wa Baraza kwa kuwataja wakiwamo Rais wa Zanzibar, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, mpambe wa Rais na kuungwa mkono kwa kupigiwa makofi na sauti za ndiyo.
Hata hivyo, alipomtaja Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad wajumbe wote waliokuwapo katika Baraza hilo, ambao wote ni wa CCM, walikataa wakisema kwa sauti “hapana,” kitendo ambacho kilimfanya Spika kurudia kutamka jina hilo kwa zaidi ya mara tatu na majibu yalikuwa hapana.
Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein (kulia) akisalimiana na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharifu Hamad
Hatua ya wawakilishi kumkataa Maalim Seif, imekuja siku moja baada ya mawaziri na wajumbe wa CUF kutoka nje ya Baraza wakisusa kujadili na kupitisha muswada wa sheria wa bajeti kuu ya matumizi ya Serikali ya mwaka wa fedha 2015/16 wakipinga pamoja na mambo mengine, mchakato unaoendelea sasa wa uandikishaji wapigakura katika Daftari la Kudumu.
“Mnakubali kutengua kanuni kuruhusu viongozi wa kitaifa kuhudhuria katika shughuli yetu ndani ya ukumbi? Wageni wetu ni Rais wa Zanzibar, mpambe wake, Jaji Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais,” alihoji Spika Kificho lakini alipingwa baada ya kulitaja jina la Makamu wa Kwanza wa Rais.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed aliwasilisha hati ya Serikali kuhusu marekebisho ya kanuni za Baraza.
Waziri Aboud alisema, Rais wa Zanzibar atakagua gwaride maalumu la Polisi kabla ya kuhutubia Baraza hilo saa 9.30 alasiri na kuwataka wajumbe wote kufika kabla ya kuwasili kwa Rais.
Kuhusu uamuzi wa kumkataa Maalim Seif, Aboud alisema upo katika mamlaka ya wajumbe kwa mujibu wa kanuni za Baraza hilo na kwamba hatua itakayofuata ni Spika kumwandikia barua Maalim Seif ya kutohudhuria shughuli hiyo ili kulinda uamuzi wa baraza hilo.
“Baraza ni chombo cha kikatiba, Serikali hatuna uwezo wa kuliingilia na kanuni ndivyo zinavyosema. Wageni ambao ni viongozi wa kitaifa lazima utengue kanuni kwa kuwauliza wajumbe kama wanakubali au kukataa,” alisema.
Waziri Aboud alisema SMZ haitaongeza muda wa Baraza ili kutoa nafasi ya Mwakilishi wa Kwa Mtipura (CCM), Hamza Hassan Juma kuwasilisha hoja binafsi ya kutaka wananchi waulizwe kama wanataka kuendelea na mfumo wa sasa wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) au la akisema kwa mujibu wa ratiba ya kikao cha bajeti, muda umemalizika na kumtaka kuangalia hoja yake katika siku za baadaye.
Azimio lazua mjadala
Kaimu Mnadhimu wa CCM, Ali Salum Haji ambaye pia ni Mwakilishi wa Kwahani, alisema wajumbe walifikia hatua ya kumzuia Maalim Seif kuhudhuria shughuli hiyo akisema ni Katibu Mkuu wa CUF, hivyo kitendo cha mawaziri na wawakilishi kususia Baraza hilo, kwa vyovyote, kulikuwa na baraka zake. “...hatujasikia kauli yoyote kutoka kwake ya kuwakemea na kama tungemruhusu ingeonekana anawachuuza wenzake.”
Hata hivyo, alisema kama Maalim Seif anataka kuhudhuria, anaweza kuingia katika ukumbi wa wageni unaotumiwa kufuatilia matukio ya baraza hilo lakini si kujumuika na viongozi wengine walioalikwa ambao watakuwa ndani ya ukumbi.
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF, Ismail Jussa Ladhu alisema wamesikitishwa na tukio hilo, lakini hawajashangazwa kwa sababu wanaofanya hivyo ndio waliokuwa wakipinga kuanzishwa kwa SUK.
Alisema tangu kuundwa kwake, SUK ilipata misukosuko mikubwa ikiwamo baadhi ya mawaziri na wawakilishi wa CCM kuwahamasisha wananchi wa majimbo yao kupiga kura za hapana wakati wa Kura ya Maoni ya kuchagua kuanzishwa kwa mfumo huo mwaka 2010.
“Kinachotokea wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu, kinaleta ufa ndani ya Serikali ya pamoja na tayari tumeanza kuchukua hatua mbalimbali kuvilalamikia vyombo vinavyohusika na dhamana ya uandikishaji, polisi na jumuiya za kimataifa,” alisema Jussa.
Alisema inasikitisha wajumbe wa Baraza wameshindwa kujadili hoja iliyojitokeza ya wao kususia kikao cha bajeti ili kujua ukweli wake.
Jussa alidai kuwa tangu kuanza kwa uandikishaji, kumekuwa na mambo yanayofanyika kinyume na sheria yakiwamo watoto chini ya umri wa miaka 18 kuandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, vyombo vya ulinzi na usalama kutumika kutisha watu pamoja na kuibuka kwa watu wenye silaha wakiwa wameficha nyuso usoni (ninja) na wengine wakivaa vinyago.
Alisema matatizo yanayojitokeza, hivi sasa, yamechangiwa na utata mkubwa katika uandikishaji wananchi kwenye Daftari la Kudumu na Usajili wa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi.
Akizungumzia hatua ya wajumbe wa CUF kususia vikao, Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar, Awadh Ali Said alisema walikuwa sahihi kwa vile utaratibu waliotumia ni moja ya njia za kisiasa za kutoa hisia zao kidiplomasia.
“Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi anatumikia mabwana watatu kwa wakati mmoja, jimbo na wananchi, chama chake cha siasa na maelekezo yake na Serikali, ndiyo maana Tume ya Mabadiliko ya Katiba tulisema mawaziri wasiwe wabunge au wawakilishi ili kutenganisha majukumu yao,” alisema Awadh ambaye alikuwa Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema kwa kuwa wananchi ndio waathirika wa mambo ya uandikishaji na usajili wa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, mwakilishi hawezi kukaa kimya hata kama ni waziri, kwa vile huo ndiyo wajibu wake.
Hata hivyo, alisema kitendo cha kuzuiwa kwa Maalim Seif kushiriki katika shughuli ya Baraza kinaweza kudhoofisha SUK kwa sababu wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu, Serikali inatakiwa kuwa na umoja pamoja na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wananchi wake.
“Wawakilishi walitakiwa kujadili hoja au malalamiko yaliyotolewa na wenzao ikiwezekana waunde tume ya kufuatilia na kuchunguza ili kubaini ukweli wa mambo, badala yake wamejadili kuondoka kwao badala ya chanzo cha wao kususia kikao hicho ndani ya Baraza la Wawakilishi,” alisema mwanasheria huyo.
Hata hivyo, alisema wakati bado unaruhusu kwa viongozi wa vyama vyote vya CCM na CUF kukaa pamoja na kujadili kasoro zinazojitokeza ili kuivusha Zanzibar salama.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment